Advertisements

Sunday, July 1, 2012

Ikulu: Msafara wa Rais haukurushiwa mawe, ni uzushi

Ikulu imekanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari (sio NIPASHE) kuwa juzi msafara wa Rais Jakaya Kikwete ulirushiwa mawe na kulazimika kusimama kwa muda katika eneo la Namanga, Tegeta jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana, imesema taarifa hizo ni uzushi na upotoshaji wa makusudi na makosa makubwa ya taaluma ya uandishi wa habari.
"Msafara wa Mheshimiwa Rais haukusimama, wala kusimamishwa ama kutupiwa mawe katika tukio hilo la Tegeta," ilisema taarifa hiyo.
Ilisema ni bahati mbaya kuwa upotoshaji huo wa makusudi bado umeendelea hata baada ya tukio hilo kutolewa maelezo mazuri ya kutosha na ya kina na maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Tanzania akiwemo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamanda Charles Kenyela.

"Ni kweli kuwa jana (juzi), majira ya saa nne asubuhi, msafara wa Mheshimiwa Rais Kikwete ulipitia katika eneo la Namanga, Tegeta, Dar es Salaam, ukienda Bagamoyo ambako Mheshimiwa Rais alizindua Hosteli ya kisasa ya Stella Maris ya Shirika la Holy Ghost Congregation la Kanisa Katoliki katika eneo la Msalabani, mjini Bagamoyo.
Aidha, baada ya kuzindua Hosteli hiyo, Rais Kikwete alifungua Mkutano wa 20 wa International General Chapter wa Shirika hilo ambao ni wa kwanza kufanyika Barani Afrika katika miaka 309 iliyopita tokea Shirika hilo lilipoanzishwa mwaka 1703 nchini Ufaransa na Claude Poullart des Places.
Hakuna wakati wowote, ama wakati wa kwenda Bagamoyo ama kurudi kutoka Bagamoyo msafara wa Mheshimiwa Rais ulisimama, hata kwa sekunde moja, kwenye eneo la Namanga, Tegeta, ama eneo jingine lolote isipokuwa nyumbani kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Mheshimiwa Steven M. Wassira ambako Mheshimiwa Rais alipitia kuhani msiba wa mama yake Mheshimiwa Wassira katika eneo la Masaki, Dar es Salaam." ilifafanua taarifa hiyo.
Imesema hakuna jiwe hata moja lililorushwa kuelekezwa kwenye msafara wa Rais ambao baada ya kuona vizuizi vimewekwa barabarani ulipitia pembeni mwa barabara hiyo ya Bagamoyo na kuendelea na safari yake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: