ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 5, 2012

Lissu awasha moto

  Ataka Serikali ya Tanganyika irudi
  Asema Zanzibar ilijitangazia uhuru
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakabiliwa na hatari kubwa ya kuvunjika kutokana na kitendo cha Zanzibar kujitangazia uhuru, na kwa hiyo ni wakati mwafaka sasa wa kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.

Msemaji wa Kambi kwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Tundu Lissu, alisema hayo wakati akitoa maoni ya kambi hiyo kuhusu Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa mwaka 2012/2013, bungeni jana.



Alisema misukosuko ambayo imeukumba Muungano tangu mwaka 1964 hailingani na hatari kubwa inayoukabili hivi sasa.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema jambo hilo waliwahi kumueleza pia Rais Jakaya Kikwete katika waraka wao wa Novemba 27, mwaka jana.

Alisema hatari ya kuvunjika kwa Muungano inatokana na mabadiliko makubwa ya kikatiba yaliyofanyika katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kutokana pia na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Hii ni kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya mwaka 2010, inaashiria tafsiri mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inahoji misingi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kama nchi moja, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, na mambo muhimu ya Muungano,” alisema Lissu na kuongeza:

“Katiba ya sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko waraka wa mwafaka kati ya vyama viwili (CUF na CCM) vilivyokuwa mahasimu.”

LISSU ATAKA TAMKO LA SERIKALI

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alichambua vifungu mbalimbali vya Katiba ya sasa ya Zanzibar na kuitaka serikali kutoa tamko bungeni sababu zilizoifanya kuiruhusu Zanzibar kujinyakulia mamlaka juu ya mambo ya ulinzi na usalama ambayo alisema kwa historia yote ya Muungano yamekuwa ni mamlaka pekee ya serikali ya Muungano.

Alisema Katiba mpya ya Zanzibar siyo tu kwamba imetangaza uhuru wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya makubaliano ya Muungano, sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la serikali ya Muungano.

Lissu alisema jambo hilo limefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwapo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar.

“Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila ya kura ya maoni ya Wazanzibari,” alisema Lissu.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi nakadhalika, ambayo yamekuwa mambo ya Muungano na Sheria ya Muungano siyo mambo tena ya Muungano hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua kwa kura ya maoni kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano.

“Huku ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru. Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani,” alisema Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu, kwa mtazamo wa Katiba ya Zanzibar, Watanzania hawana tena nchi moja inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano, bali wana nchi mbili.

Alisema kwa mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi nakadhalika, siyo tena mambo ya Muungano kwa sababu kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake.

Pia alisema Watanzania wana marais wawili, wakuu wa nchi wawili na viongozi wa serikali wawili.

Alisema mambo yote hayo yanakiuka moja kwa moja makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

Lissu alisema kwa upande mwingine kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua wakuu wa mikoa wa Zanzibar.

Alisema pia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania licha ya kuwa moja ya mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar.

“Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru, huu ni wakati mwafaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika,” alisema Lissu na kuongeza:

“Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano siyo tu una serikali kamili, Bunge kamili, mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya.”

Alisema wanatambua kwamba sheria ya mabadiliko ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi mikuu ya kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano.

Lissu alisema hata hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga kuendelea kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema kwamba wale wanaopinga Muungano nao wajitokeze kutoa maoni yao kwa tume.

Kutokana na hilo, aliitaka serikali kutoa kauli mbele ya Bunge namna gani maoni ya wale wanaotaka alichokiita “kiini macho” cha Muungano kiishe yatashughulikiwa na tume ambayo imepewa jukumu kisheria la kuhifadhi na kukidumisha kiini macho hicho.

Alihoji ni kipi kitakachoizuia tume hiyo kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba sheria inaielekeza tume kuratibu na kukusanya maoni na kutoa mapendekezo ya kuhifadhi na kudumisha Muungano.

Awali, Lissu alisema umefika wakati kwa serikali kuweka wazi nyaraka mbalimbali zinazohusu historia ya Muungano na mapato yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu.

Alisema suala hilo ni muhimu kwa kuzingatia kwamba mataifa ya Magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.

VURUGU ZA Z’BAR

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema vurugu na machafuko yanayotokea visiwani Zanzibar, yanadhihirisha kwamba juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali kupata suluhisho la kero za Muungano hazijazaa matunda.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fakharia Khamis Shomar, alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa mwaka 2011/2012 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013, bungeni jana.

Fakhari, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo aliwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Pindi Chana.

“Kamati inaishauri serikali kuonyesha dhamira ya dhati na kulichukulia suala la Muungano kama suala nyeti ili matatizo yaliyopo yapate ufumbuzi kwani hivi sasa imekuwa siyo kero tena bali bughudha kwa pande zote mbili za Muungano,” alisema Fakharia.

Aliitaka serikali kutoa ufafanuzi ni kwanini suala la wafanyabiashara wa Zanzibar bado limeendelea kuwa kero kwa kutozwa kodi mara mbili na taasisi zinazotoza kodi.

Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakitozwa kodi mara mbili licha ya serikali kuieleza kamati mwaka jana kuwa kero hiyo imepatiwa ufumbuzi.

Fakharia alisema katika taarifa hiyo kwa kamati, serikali ilieleza pia kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini na kukamilisha utaratibu wa forodha kupitia kituo chochote cha forodha ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hazipaswi kulipa kodi mara mbili.

Alisema kamati pia inaamini kuwa suala la mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada katika nchi za nje bado ni kero, hasa kwa upande wa Zanzibar, hivyo akaiomba serikali kulitolea ufafanuzi jambo hilo.

Pia aliitaka serikali kuzipitia upya sekta zote zinazoonekana kuwa na matatizo ili kupata suluhisho kwa manufaa na ustawi wa Muungano.

Vilevile, aliitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazofanya  mawaziri wa fedha wa pande zote mbili za Muungano kushindwa kukutana na kushauriana kuhusu hatua zilizofikiwa na pande mbili katika kushughulikia mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha.

Alisema sheria inayotaka taarifa kupelekwa kwa mawaziri wa fedha ibadilishwe ili taarifa hizo zipelekwe bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuridhiwa.

Kuhusu kazi ya Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano kuzishauri serikali zote mbili juu ya masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa mapato, alisema kamati inasikitika agizo hilo halijatekelezwa kwa sababu, ambazo hazikuwekwa wazi mbele ya kamati.

Awali, akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2012/2013, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema hoja mbili kati ya 13 zilizojadiliwa na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), zilipatiwa ufumbuzi.

Alisema hoja zilizobaki ziko katika hatua mbalimbali za kuishughulikiwa.

Alizitaja hoja zilizopatiwa ufumbuzi kuwa ni pamoja na ile inayohusu ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na inayohusu Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo wa SMT.

Hoja nyingine ambazo ziko katika hatua za kutafutiwa ufumbuzi alizitaja kuwa ni pamoja na ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje na utafutaji na uchimbaji wa mafuta ya gesi.

Nyingine ni ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano, hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, marekebisho ya sheria ya usajili wa vyombo vya moto, kodi ya mapato inayozuiwa na Kodi ya Mapato ya Ajira (Paye) na malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.

Aliliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 53 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.



 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Too little, too late.