Monday, August 13, 2012

Balozi wa Kenya: Majeruhi hakusahaulika Muhimbili




Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, amesema kuwa siyo kweli kuwa raia wa Kenya, Mary Wambui, mmoja wa majeruhi wa ajali ya Ijumaa iliyoua watu 12, alisahaulika katika Hospitali ya Muhimbili wakati wengine walipohamishiwa Nairobi kwa matibabu zaidi, ila alikuwa chumba cha upasuaji wakati wenzake wanaondoka.

Balozi huyo alisema Mary Wambui, alikuwa miongoni mwa majeruhi watano walioumia sana, alipelekwa chumba cha upasuaji kutokana na kukabiliwa na tatizo la kupumua lakini baada ya operesheni hiyo, alisafirishwa juzi saa 10:00 jioni kwenda Nairobi.



Hata hivyo, Balozi huyo alisema majeruhi aliyebakia Muhimbili hadi sasa ni Jane Wambui Mbugwa, ambaye ameumia uti wa mgongo na bado anahitaji uangalizi kwa wiki moja zaidi.

Jana gazeti hili lilimkariri Ofisa Habari wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha, akisema majeruhi mmoja aliyemtaja kwa jina la Mary Mungai, kuwa alisahaulika Muhimbili wakati wenzake walipoondolewa kupelekwa Nairobi kwa matibabu zaidi kwa amri ya Rais wa Kenya, Mwai Kibaki.

Balozi huyo alisema mabasi yaliyopata ajali yalikuwa na abiria 84, kati yao 14 waliojeruhiwa watano hali zao zikiwa mbaya zaidi wakiwamo Mary Wambui na Jane Wambui Mbugwa.

Ajali hiyo ilitokea Ijumaa katika kijiji cha Makole karibu na eneo la mto Wami mkoani Pwani ikihusisha mabasi mawili yaliyokuwa yanasafirisha wanakwaya kutoka Kenya na malori mawili.
Watu 12 walikufa katika ajali hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake