Monday, August 6, 2012

Bei ya Okwi Ulaya bil. 1, Yanga bil. 3/-

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, hawezi kujiunga na Yanga kwa sababu uongozi wa klabu yake hauko tayari kuona jambo hilo linatokea.

Jambo hilo limethibitishwa na mkanganyiko wa viwango vya bei ya kumuuza Mganda huyo anayetarajiwa kuwasili nchini leo vilivyotajwa jana na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.



Akizungumza jana kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Simba uliofanyika kwenye bwalo la Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema kuwa Okwi bado ni mchezaji halali wa klabu hiyo na kama Yanga wanamuhitaji watoe Dola za Marekani milioni 2 (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 3.2), kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya bajeti nzima ya klabu ya Simba kwa mwaka 2012/13.

Hata hivyo, Simba imesema inatarajia kumuuza Okwi kwa Euro 600,000 (sawa na Sh. bilioni 1.1) kwa klabu ya Austria ya Redbull Salzburg endapo 'dili' lake litakamilika.
Viwango tofauti vya bei ya mchezaji huyo, vinamaanisha kwamba Simba iko tayari kumuuza Okwi kwa bei poa Ulaya kuliko kumuona anajiunga na Yanga.

Rage alisema kuwa anaamini Okwi hawezi kukataa ofa ya mshahara wa Euro 30,000 (sawa na Sh. milioni 57) kwa mwezi nchini Austria na kujiunga na watani zao, Yanga ambao wanasemekana wako tayari kumpa mshahara wa Sh. milioni 2.5 kwa mwezi endapo atakubali kujiunga nao.

Mwenyekiti huyo alisema pia katika kuendelea kuijenga Simba, Agosti 9 wanatarajia kumpokea mshambuliaji mpya kutoka Stella Abdijan ya Ivory Coast, Sihaone Abdulaziz ambaye klabu yake imemtoa kwa mkopo ili apate uzoefu wa mechi za kimataifa.

"Simba ni sehemu ya kupika vipaji, jana nimesaini fomu za Messi (Ramadhani Singano) anaenda Austria kufanya majaribio, huko Austria tunatarajia kufanya nao makubaliano ya kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo," alisema Rage.

Wakati huo huo, Rage aliwapa Yanga hadi Ijumaa wawe wamelipa Sh. milioni 60 kwa ajili ya uhamisho wa beki, Kelvin Yondani na endapo haitafanya hivyo watapeleka mashitaka yao CAF na baadaye FIFA kwa sababu wanaamini beki huyo ni mali yao.

"Haiwezekani karatati sita za mkataba ziseme Yondani alisaini mwaka 2011, na moja inayotaja ameingia mkataba mwaka 2012 iwe ndio sababu ya kutoutambua mkataba, lile lilikuwa ni kosa la kiuchapaji, tutafika hadi FIFA," alisisitiza Rage.

Alisema pia uongozi wa Simba ulisikia kilio cha mashabiki wa timu hiyo na ndiyo maana imefanikisha kumsajili beki wa kati wa APR ya Rwanda, Mbuyi Twite ili kuimarisha safu ya ulinzi.

Alisema pia Simba na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara ziko katika mazungumzo na mdhamini wa ligi hiyo kuongeza dau ambapo wataboresha mambo mbalimbali ikiwamo zawadi ya bingwa wa ligi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake