Tuesday, August 7, 2012
CAG aanza kuchunguza madudu Tanesco
NI PAMOJA NA MADAI YA MATUMIZI MABAYA YA OFISI DHIDI YA MHANDO
Geofrey Nyang’oro
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema ofisi yake imeanza ukaguzi wa tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando.
Julai 14 mwaka huu, Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilimsimamisha kazi Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Harun Mattambo kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Utouh aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba ofisi yake imekabidhiwa kazi hiyo na tayari imeshaanza na imefikia pazuri. “Ni kweli suala hilo nimeshakabidhiwa na kazi hii tayari imeshaanza na imefikia pazuri. Kikao cha kwanza kimekaa Jumamosi iliyopita na mimi nimeshafika kuwahakiki maofisa wangu wanaoshughulikia hilo,” alisema Utouh na kuongeza kuwa kazi hiyo inaweza kukamilika ndani ya siku 60 kuanzia sasa.
Tuhuma zilizopo
Tuhuma za ufisadi Tanesco, zilianzia katika ripoti ya CAG ya mwaka huu ambayo ilionyesha gharama za ununuzi ziliongezeka kwa mwaka jana, kutoka Sh300 bilioni hadi 600 bilioni.
Baada ya sakata hilo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ilitaka hatua zichukuliwe dhidi ya Bodi na Watendaji wa Tanesco na kuhoji ongezeko hilo kubwa la gharama za ununuzi.
Lakini wiki mbili kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, bodi hiyo iliitisha kikao cha dharura Julai 13, mwaka huu kujadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya shirika hilo na kuamua kwamba tuhuma dhidi ya Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa kina.
“Hivyo, Bodi iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini.”
“Pamoja na uamuzi huo, Bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli za utendaji na uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama kawaida,” ilisema taarifa hiyo.
Sakata hilo lilipamba moto bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kwa 2012/13. Akiwasilisha Bajeti hiyo, waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alisema mbali ya tuhuma za kupanga mgawo wa umeme kama mkakati na kampuni za mafuta, Mhando pia anadaiwa kuidhinisha zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kwa kampuni ya mkewe, Eva Mhando. Profesa Muhongo alisema zabuni hiyo ni zaidi ya Sh800 milioni na kwamba, Eva alitumia kampuni ya Santa Clara na Mhando aliidhinisha pasipo kutangaza mgongano wa kimasilahi. Tuhuma hizo na nyingine zilihusisha baadhi ya wabunge na kumfanya Spika, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Nishati na Madini baada ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
CAG atangaza mikakati ya UN
Katika hatua nyingine, Utouh jana alitumia mkutano huo na waandishi kufafanua jukumu la ukaguzi katika Umoja wa Mataifa (UN) na kusema, atatimiza jukumu hilo akiwa nchini na hatahamia New York, Marekani. “Baada ya kutangazwa kuteuliwa kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa wapo watu waliosikitika kuwa nitaondoka nchini na kwenda New York,” alisema Utouh na kuongeza;
“Kuna watu waliamua kusema kwa masikitiko makubwa na wengine wachache wakafurahia kuwa sasa vita ya ufisadi inayopiganwa na ofisi yangu itarudi nyuma. Wananchi waelewe kuwa vita ya ufisadi ni ya Watanzania wote wapenda amani na maendeleo, hivyo basi Utouh ataendelea na kazi yake,” alisema.
Utouh ambaye amekabidhiwa mashirika na taasisi zilizo chini ya UN, kwa ajili ya ukaguzi likiwamo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ofisi yake imeteua maofisa 60 kwa ajili ya jukumu hilo.
Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni Shirika la Misaada ya Wokozi kwa Wapalestina (UNRWA), Shirika la Kusimamia Amani Congo (MONUSCO), Shirika la Kusimamia Amani Haiti (UNTAMH) na Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa Kimataifa ya Yugoslavia (ICTY).
Taasisi nyingine ni Mahakama ya UN ya Mauaji ya Rwanda (ICTR), iliyopo Arusha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UNW), Kundi la Kulinda Amani Liberia (UNMIL) na Kundi la Kulinda Amani Somalia (AMILSON).
“Tumeteua maofisa 60 na tayari wameshapatiwa mafunzo na kuanza kazi katika maeneo yaliyoainishwa, watumishi wawili kati yao watakaa nchini Marekani wakiniwakilisha na wengine watakuwa wakienda katika maeneo mbalimbali na kurudi nchini,” alisema Utouh.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake