Monday, August 6, 2012

Kamati ya Lowassa yajitosa mgogoro na Malawi


Fredy Azzah na Geofrey Nyang'oro
SUALA la mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Malawi na Tanzania, limezidi kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kutaka kupewa maelezo juu ya mgogoro huo.
Malawi na Tanzania zote zilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na mipaka inayotambulika sasa kwa sehemu kubwa, ni ile ambayo iligawanywa wakati wa Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/1885.
Hata hivyo, ikiwa sasa ni takriban muongo mmoja tangu nchi hizo mbili zipate uhuru, Malawi katika siku za karibuni imeibua mjadala mzito unaotishia uhusiano wa kidiplomasia na eneo la mpakani na Tanzania, ikisema Ziwa Nyasa lote liko katika ardhi yake.
Akizungumzia mgogoro huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo,Edward Lowasa alisema baada ya kupata taarifa rasmi ya hali ilivyo katika mpaka huo, itakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa tamko lake.

“Tutatoa tamko letu baada ya kupata taarifa rasmi kutoka kwa vyombo vinavyohusika, kwanza tujue hali ikoje, mambo kama haya hayaendi haraka,” alisema Lowassa.
Lowassa hakusema taarifa hizo wameomba kutoka kwenye vyombo gani, badala yake alisisitiza kuwa wametaka vyombo vinavyohusika kuwapa taarifa rasmi juu ya suala hilo.

JWTZ, wasomi wazungumzia
Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa lipo juu ya uwezo wake.
“Hilo jambo lipo juu ya uwezo wangu, siwezi kulizungumzia tuna mipaka ya taarifa gani tunaweza kutoa kwa vyombo vya habari. Siyo kila jambo linatangazwa, mengine yanakwenda kimyakimya,” alisema na kusisitiza: “Siyo kila jambo tunalofanya ni lazima tuseme... mengine yana hasara zake.”
Lakini, Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa, Profesa Abdallah Safari alisema suala la mipaka ya nchi linasimamiwa na sheria za kimataifa ambazo alisema lazima ziheshimike.
Profesa Safari ambaye pia ni mwanasheria alisema sheria hizo za kimataifa zinaitambua mipaka iliyowekwa na wakoloni wakati wa Mkutano wa Berlin uliofanyika mwaka 1884, hivyo lazima kila nchi iheshimu.
“Wakoloni walivyogawa mipaka, Tanzania na Malawi kwa upande wa Ziwa Nyasa ulikuwa ni katikati ya ziwa hilo na Malawi wanaelewa. Wanachofanya ni uchokozi tu wa kutafuta vita visivyokuwa na sababu,” alisema Profesa Safari na kuongeza:
“Kuna wakati kulikuwa na mgogoro kama huu kati ya Libya na Chad. Kulikuwa kuna eneo lililokuwa na mafuta, Libya ikataka kulichukua lakini mwisho Chad ilikuja kushinda kwa sababu eneo lilikuwa lao kwa mujibu wa mipaka ya kikoloni. Kwa hiyo hata hili la kwetu mipaka rasmi ni ile iliyowekwa na mkoloni katikati ya Ziwa Nyasa,” alisema.
Alisema katika baadhi ya mipaka iliyotenganishwa na mito, ipo baadhi ambayo huwa na tabia ya kuhama na kwenda upande mmoja, lakini tatizo kama hilo halipo kwa Ziwa Nyasa hivyo, Malawi haina sababu yoyote ya kuleta usumbufu.
“Kwa maana hiyo, naweza kusema tu kuwa, Malawi wanachotafuta ni uchokozi kwa sababu hizi sheria za kimataifa wanazifahamu,” alisisitiza Profesa Safari.
Kwa upande wake, Profesa Mwesiga Baregu ambaye amebobea katika eneo hilo la uhusiano wa kimataifa alisema ni vyema nchi zote zikaendelea kuzungumza na kumaliza suala hilo.
Alionya nchi zote kutochukua hatua za kijeshi akisema mazungumzo ndiyo njia bora zaidi ya kumaliza suala hilo.
“Nchi zote ziepuke hatua zozote za kutumia jeshi, kwa sababu hatua za kufanya hivyo zitakuwa na madhara siyo tu kwa Tanzania na Malawi ila katika nchi zote za SADC,”  alisema Profesa Baregu.
Profesa Baregu alisema endapo hakutakuwa na matunda katika mazungumzo kati ya Malawi na Tanzania, ni vyema suala hilo likafikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice- ICJ).

“Jambo kama hili lilishatokea kati ya Cameroon na Nigeria, walikuwa wakigombea  eneo lenye utajiri mkubwa tu wa mafuta, mgogoro ule ulimalizwa na ICJ ambapo Cameroon walionekana ndio wenye haki,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alitaka mgogoro huo wa utatuliwe kwa njia ya majadiliano huku akisisitiza kuwa sheria za kimataifa zinapaswa kuzingatiwa.
Profesa Lupumba alisema sheria ziko wazi kuwa nchi zinazotenganishwa na bahari au ziwa mpaka wake huwa katikati ya eneo la maji na kwamba kama hilo litazingatiwa hakuwezi kuwa na mgogoro tena baina ya pande hizo mbili.

Onyo la Sitta 
Wiki iliyopita, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, akitoa kauli ya Serikali kuhusu Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alisema Tanzania iko tayari kwa lolote kuhusu mpaka huo.
Zambi alisema vyombo vya habari vya Malawi na vya Tanzania vimemkariri mmoja wa makatibu wakuu wa Malawi, akieleza kwamba Ziwa Nyasa lipo nchini mwake kwa asilimia 100, hali ambayo inahatarisha uhusiano wa nchi hizo.
“Ni vyema Serikali ikatoa maelezo juu ya hali ya Ziwa Nyasa ili wananchi wa Mbeya na wabunge hapa tuelewe, maana kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mpaka wa ziwa hili na hatujui kilichofikiwa,” alisema.
Alisema taarifa za katibu huyo zinatia wasiwasi na hofu kwa wananchi wa Mbeya ambao wanatumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema suala hilo atalipeleka serikalini ili Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alitolee ufafanuzi na taarifa kamili.
Hata hivyo, Sitta, alisema Serikali imeshtushwa na taarifa hizo kwa kuwa mazungumzo kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa yanaendelea.
Alionya kwamba Tanzania ipo tayari kwa uchokozi wowote kwa kuwa inafuata sheria za kimataifa hivyo akawataka wananchi wa Mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, ambayo inapakana na ziwa hilo kuendelea na shughuli zao za kiuchumi ziwani humo.
Sitta alisema kauli rasmi ya Serikali kuhusu jambo hilo itatolewa bungeni leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake