Monday, August 6, 2012

Membe kupasua jipu leo




Wakati leo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, atawasilisha bungeni bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa 2012/13, Watanzania wanasubiri kusikia mambo mazito kutoka kwake.

Moja ya mambo ambayo Waziri Membe anatarajiwa kuyasema ni kuyumba kwa uhusiano kati ya Tanzania na Malawi, baada ya nchi hiyo kudai kuwa inamiliki Ziwa Nyasa kwa asilimia 100.

Suala hilo liliibuka bungeni Alhamisi iliyopita baada ya Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Godfrey Zambi, alipoomba mwongozo wa Spika akieleza kuwa vyombo vya habari vya Malawi na vya Tanzania, vimemkariri mmoja wa makatibu maofisa waandamizi wa Serikali ya Malawi, akieleza kwamba Ziwa Nyasa lipo nchini mwake kwa asilimia 100, hali ambayo inahatarisha uhusiano wa nchi hizo.



“Ni vyema serikali ikatoa maelezo juu ya hali ya Ziwa Nyasa ili wananchi wa Mbeya na wabunge hapa tuelewe, maana kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mpaka wa ziwa hili na hatujui kilichofikiwa,” alisema.

Alisema taarifa za katibu huyo zinatia wasiwasi na hofu kwa wananchi wa Mbeya ambao wanatumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema suala hilo atalipeleka serikalini ili Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alitolee ufafanuzi na taarifa kamili.

Hata hivyo, Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni, Samuel Sitta, alisema serikali imestushwa sana na taarifa hizo kwa kuwa mazungumzo kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa yanaendelea.

Alionya kwamba Tanzania ipo tayari kwa uchokozi wowote. Hata hivyo, Sitta alisema kauli rasmi ya serikali kuhusu jambo hilo itatolewa bungeni leo na Waziri Membe.

Mabli ya hilo, pia Waziri Membe anatarajiwa kuzungumzia taarifa kwamba kuna Watanzania kadhaa wakiwemo wanasiasa na wafanyabiashara ambao wameficha fedha kiasi cha Sh. bilioni 300 katika benki kadhaa nchini Uswisi.

Hivi karibuni Membe alihojiwa katika kipindi cha dakika 45 na Kituo cha Televisheni cha ITV na kueleza mambo kadhaa, vikiwemo vitendo vya ufisadi nchini na kuahidi kuwataja hadharani wahusika. 

Katika mahojiano hayo, Waziri Membe kadhalika aliahidi kwamba atawalipua watu wote waliohusika katika wizi wa rada ambayo Tanzania iliuziwa na kampuni ya BAE System ya Uingereza mapema miaka ya 2000.

Waziri Membe pia alisema kuwa kuna watu 11 ambao wanaiyumbisha nchi na kuahidi kwamba atawataja kwa majina katika siku za karibuni.

Hiyo itakuwa fursa nzuri kwa Waziri Membe wakati wa kujibu hoja mbalimbali za wabunge watakaochangia hotuba yake kuwataja watu hao kama alivyoahidi.

Baada ya bajeti ya Waziri Membe kupitishwa, kesho wabunge watajadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira.

Bajeti hiyo inatarajiwa kutawaliwa na mjadala mkali wa sheria mpya ya mafao ambayo inawazuia wafanyakazi wanaoacha kazi kutochukua mafao yao kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii hadi kufikia miaka 55 na 60.

Dalili za kuzuka kwa mjadala mkali zimejionyesha baada ya Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM), kutoa hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe bungeni kwa kuwa linawaumiza wafanyakazi.

Pia Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alimwandikia Katibu wa Bunge, akitaka hoja binafsi ili suala hilo lijadiliwe bungeni.

Wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi, wanasiasa, wanaharakati na makundi mbalimbali ya jamii, wanaipinga sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge Aprili, mwaka huu kwamba ni ya ukandamizaji.

Baadhi ya wafanyakazi kwa mfano, mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, wiki iliyopita waligoma na kuilazimisha menejimenti kuufunga mgodi huo kwa saa 48.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, kikao cha Bunge hakitakuwepo Jumatano ili kupisha wabunge kuungana na wakulima nchini kusherekea sikukuu ya Wakulima maarufu kama Nane Nane.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Alhamisi itakuwa zamu ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, huku Ijumaa na Jumamosi zitatumiwa na   wabunge kuichambua hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake