Monday, August 13, 2012

NAMNA YA KUBADILI MAUMIVU YA MAPENZI KUWA FURAHA

BILA shaka mpenzi msomaji umzima buheri wa afya na muda huu unanifuatilia katika busati letu zuri la mahaba, mahali tunapojuzana na kuelimishana mambo kadha wa kadha yahusuyo mapenzi na uhusiano. Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu tuijadili mada yetu ya leo kama inavyojieleza hapo juu.
Ni ukweli usiopingika kuwa katika zama hizi za sayansi na teknolojia, maumivu ya mapenzi yameongezeka maradufu. Kile tunachoamini kuwa ni maendeleo, kinazidi kuzitesa hisia na nafsi zetu na suala la kutendwa, kuumizwa, kuvunjika mioyo au kusalitiwa, linaonekana kuwa fasheni siku hizi.
Kinachowasumbua wengi ni kushindwa kuelewa nini cha kufanya baada ya kuangukia katika dimbwi la maumivu ya kimapenzi. Hebu kila mtu ajiulize: 

Umewahi kukuta SMS ya mapenzi kwenye simu ya mpenzi wako akimtumia mtu mwingine tofauti na wewe? Ulijisikiaje uliposikia mtu mwingine akiitwa majina mazuri ya kimapenzi  na mpenzi wako, pengine kuliko hata yale ambayo huyatumia kwako? Ulichukua uamuzi gani?
Kila mtu ataeleza anavyojua yeye lakini ukweli ni kwamba wengi hawajui kukabiliana na maumivu hata yale yanayosababishwa na maisha ya kawaida. Kwa kuwa maumivu, usaliti, kuvunjika kwa mioyo na uongo katika mapenzi ni jambo ambalo kwa kiasi kikubwa halikwepeki katika zama hizi, jambo la msingi ni kujua nini cha kufanya baada ya kutokewa na dhoruba hizo za kimapenzi.
Hebu msikilize msomaji wangu, Jane wa Ilala Bungoni jijini Dar, alivyokuwa analalama:
“Wiki nzima inaisha sasa, siendi kazini, chakula hakipandi, usingizi sipati wala sitamani kitu chochote, kitu pekee ninachokifanya ni kulia usiku na mchana, naomboleza na kulalama katika kila sekunde inayopotea mpaka natamani kujiua, sioni tena thamani ya kuishi, nayachukia mapenzi, nawachukia wanaume,” alisema Jane huku akilia kutokana na kutendwa na mwandani wake aliyemsaliti kwa kutoka na rafiki yake kipenzi.
Yawezekana Jane hayuko peke yake, wapo wengi ambao wanateswa sana na mapenzi lakini hawana sehemu ya kuyatoa maumivu yao, wanaumia ndani kwa ndani, miili yao inadhoofika kila siku, hawana furaha japokuwa wanapata mahitaji yote muhimu, chanzo kikuu kikiwa ni mapenzi.
Hapo ndipo ninapoona umuhimu wa kila mmoja kujua namna ya kusimama tena pale anapoangushwa na maumivu ya kimapenzi.
Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia kuyabadilisha maumivu yako ya kimapenzi kuwa furaha.

JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU
Hakuna jambo ambalo hutuliza fikra na hisia za mapenzi kama kukubali kumsamehe yule aliyekuudhi kabla hata hajakuomba msamaha na kuamua kusahau yote yaliyotokea. Yawezekana wengi mtasema haiwezekani. Inawezekana na wote waliojaribu mbinu hii walifanikiwa.
Marafiki, lazima kila mmoja aelewe kwamba unapokasirika au kuumizwa, anayeteseka siyo yule aliyekusababishia maumivu bali ni wewe mwenyewe. Hasira au maumivu ya kimapenzi huwa kama moto mkali ambao huitafuna taratibu nafsi ya mhusika.
Ukisamehe maana yake unaupa moyo na akili yako nafasi ya kupata sehemu ya kutulia na kuuzima moto ambao tayari ulishaanza kukolea ndani yako.

Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake