Friday, August 10, 2012

Vigogo CCM sasa kunyang'anywa kadi


  Moto mkali dhidi yao wawashwa
  Wadaiwa kuvunja sera ya chama
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi
Ni kama tayari kuna makubaliano ya kuwajibishana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya utoaji wa maoni ya Katiba mpya, kutokana na kauli za kukinzana juu ya aina ya Muungano wanaoutaka.

Wakati vitisho vya kuwafukuza uanachama viongozi na wanachama wake wanaopinga mfumo wa Muungano wa serikali mbili vikiibuka Zanzibar, mjini Dodoma nako wabunge wa CCM waliitisha mkutano na waandishi wa habari jana na ajenda ikawa ni hiyo hiyo, kufukuza uanachama wanaoupinga sera ya Muungano wa serikali mbili.

Katika matukio yote mawili, viongozi waandamizi wa Chama, wakiwamo walioko katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa sasa wamewaambia viongozi na wanachama hao kuwa ni afadhali wakarejesha kadi za uanachama badala ya kusubiri kufukuzwa na chama.



Akifungua mkutano Mkuu wa Jimbo la Kitope katika Mkoa wa Kaskazini Unguja jana Kisiwani Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliwataka wanaoupinga mfumo wa Muungano wa sasa wajiondoe CCM kabla ya kufukuzwa.

Balozi Seif alisema wanachama na viongozi ambao wameamua kwenda tofauti na sera ya chama hicho kuhusu mfumo wa Muungano na kwamba wamekuwa pia wakienda kinyume na Ibara ya 221 ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Balozi Seif ambaye pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC), alisema CCM ni chama tawala na kimepata ridhaa ya kuongoza nchi baada ya kuchaguliwa na wananchi, hivyo haiwezekani kutokea mwanachama au kiongozi akaenda kinyume cha sera yake.

Aliwataka wanachama wa chama hicho kuhakikisha kwamba Zanzibar inaendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa chini ya Muungano wa Tanzania.

“Wale wanaotaka kutuvurugia chama chetu na Muungano wetu waturejeshee kadi zetu, kwa nini wanachama hao wanasubiri mpaka wajadiliwe kwenye vikao vya chama au vile vikao vya maadili. Ya nini kutuvurugia chama chetu wakati nafasi za kung’atuka zipo wazi?” alihoji Balozi Seif huku akishangiliwa wajumbe wa mkutano huo.

Alisema Taifa hivi sasa linapita katika kipindi kigumu kutokana na kuibuka kwa vikundi vinavyofanya kazi ya kushawishi wananchi na hasa vijana kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani kitendo ambacho alisema ni kinyume cha misingi ya utawala wa sheria.

Aidha, alisema kwamba wanachama wa CCM lazima wawe makini kupitia uchaguzi mkuu wa chama kwa kuhakikisha wanachagua viongozi makini na waadilifu ambao watasadia kuimarisha umoja, amani na mshikamano.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba hivi sasa jamii inashuhudia matusi ya nguoni yanayoendelezwa na baadhi ya makundi ya watu dhidi ya viongozi wa serikali na chama, hali ambayo alisema kama jamii hiyo haitakuwa makini, Taifa linaweza kutumbukia katika fujo na hatimaye maangamizi.

“Tunakotoka kubaya, sote ni mashahidi kwa sababu familia na hata ndugu wa karibu walikuwa hawaulizani hali na hata maziko hawaendeani. Kwa kweli tusifikie tabia hii kuiruhusu irejee tena,” alisema Balozi Seif.

Alisema CCM Zanzibar kitaendelea kuunga mkono mfumo wa Muungano wa serikali mbili na kuwataka wanachama na viongozi wa CCM kuheshimu sera na katiba ya chama hicho.

WABUNGE NAO WACHARUKA


Hayo yakitokea Zanzibar, wabunge wa CCM kutoka Zanzibar wamewajia juu na kuutaka uongozi wa chama hicho kuwachukulia hatua ya kinidhamu baadhi ya viongozi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotaka kuuvunja Muungano.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa wabunge kutoka Zanzibar, Dk. Mohammed Seif Khatib akiwa amefuatana na wabunge wapato 30 kutoka visiwani, alisema wao kama wabunge wanashangaa kusikia viongozi hao wakitamka maneno makali ya kuvunjwa Muungano huku wakitazamwa.

Alisema wao kama wabunge waliopata ushindi kutokana na Ilani ya CCM inayotamka wazi kuunga mkono wa serikali mbili, wataendelea kutetea msimamo huo kwa sababu wanachoamini kama yatafanyika mabadiliko mbalimbali kwenye Katiba, hatimaye kila upande utapata haki yake ya msingi.

“Kuna baadhi ya viongozi wanashabikia kuvunjwa kwa Muungano, hilo sisi wabunge tunawaachia viongozi wa ngazi za juu kuhakikisha wanachukua hatua za kinidhamu ili kukomesha tabia hiyo,” alisema Dk. Khatib.

Dk. Khatib alisema wanaamini mfumo wa serikali mbili una faida kubwa kwa Zanzibar na watu wake ikiwa utawekewa mfumo wa kikatiba wa utekelezaji katika kuondoa kabisa kero hizo zilizoko katika Muungano.

Alisema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM waliotumia kuombea ridhaa kwenye majimbo yao, inaweka wazi kuhusiana na mfumo wa serikali mbili, hivyo kulingana na ilani hiyo wote kwa pamoja wanaunga mkono msimamo huo.

Hata hivyo, aliwataka wananchi wa Zanzibar kuaacha kujikita katika suala moja la Muungano wakati wanapotoa maoni yao juu ya Katiba mpya, kwani kuna maeneo mengine muhimu ambayo wanayaacha bila kuchangia.

Tamko hilo limekuja kufuatia baadhi ya wanasiasa, wakiwemo makada wakongwe wa CCM Zanzibar kutoa maoni yanayokwenda tofauti na msimamni wa chama hicho kuhusiana na mfumo wa Muungano.

Wiki iliyopita, mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibae, Ali Nassoro Moyo na Waziri Asiye na Wizara Maalum, Mansour Yusuf Himid, walisema kuwa Muungano wa sasa unakabiliwa na kasoro nyingi na kupendekeza uanzishwe Muungano wa mkataba.

Mbali na Moyo na Mansour, viongozi wengi wa Chama cha Wananchi (CUF) wamekuwa wakitetea Muungano wa mkataba ambao wanasema utasadia Zanzibar kuwa na bendera na kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).

Kadhalika, Jumiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kislamu (Jumiki) imeanzisha kampeni misikitini za kutaka Zanzibar kujitenga na Muungano.

Hata hivyo, tamko la Balozi Seif linakwenda kinyume cha maelekezo yaliyotolewa na Tume Warioba ambayo inakusanya maoni ya Katiba mpya, ambayo iliwatoa wasiwasi Watanzania wote na kuwataka watoe maoni yao kuhusu katiba bila woga.

Jaji warioba alisema kuwa tume yake itawasikiliza watu wote, wakiwemo wanaoupinga Muungano.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake