Wednesday, September 12, 2012

Askari aliyetekwa akutwa na majeraha


Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe

Askari wa Bandari jijini Dar es Salaam anayedaiwa kutekwa, Corneli Kufaizalu, amepatikana Mafinga, wilayani Mufindi, mkoani Iringa akiwa na majeraha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, jana alithibitisha kupatikana kwa askari huyo juzi na kwamba amelazwa katika hospitali moja huko Mafinga ambayo hata hivyo, hakuitaja kwa maelezo kuwa ni kwa sababu za kiusalama.

Kabla ya taarifa za kupatikana kwa askari huyo, wafanyakazi wa Bandari jijini Dar es Salaam waliitisha mkutano wa kujadili tukio la kutekwa kwa mwenzao na kuazimia kumsaka katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.



Askari huyo alitekwa Septemba 8, mwaka huu baada kushiriki katika operesheni ya kukamata watu waliovamia bandari usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kwa lengo la kuiba madini ya shaba na mafuta ya petroli.

Kutekwa kwa askari huyo kulizua taharuki na maswali mengi miongoni mwa wafanyakazi wa Bandari ambao walieleza kuwa utendaji wao wa kazi umeanza kuwa mgumu.

Miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuhusika katika tukio la wizi wa mafuta ni askari waliokuwa doria ambapo taarifa hizo zilielezwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Jumamosi iliyopita.

Viongozi na wafanyakazi wa bandari walisema kuwa watu waliomteka askari huyo walitoa masharti kwamba watamuachia iwapo tu wenzao  waliokamatwa wakati wa mapambano kati ya polisi wa bandarini na wezi katika tukio hilo wataachiwa huru.

Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, juzi  alisema Septemba 8  mwaka huu majira ya saa 8:00  usiku eneo la Shedi No. 7, polisi waliwakamata watu 14 kwa kosa la kuvunja kontena na kuiba vipande 19 vya madini ya shaba, mafuta ya petrol lita 360 na diseli lita 60.
Vitu vilivyoibwa ni vipande vya madini ya shaba, mafuta ya petrol lita 360 na diseli lita 60.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake