Friday, September 14, 2012

Hatma hekalu la Rwakatare Sept 20

Nyumba inayodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Dk. Getrude Rwakatare, ni miongoni mwa majumba ya kifahari yaliyojengwa kando ya mito ya Mbezi Beach, Mndumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko, jijini Dar es Salaam, ambazo zinatakiwa kubomolewa.

Hata hivyo, mpango wa kubomoa nyumba hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.5 umekwama kutokana na mahakama kuzuia. 



Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche, alithibitisha kuwapo kesi iliyofunguliwa na mmiliki wa jumba hilo.

Heche alisema kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, na itatajwa Septemba 20, mwaka huu.

Alisema mbali ya kufungua kesi hiyo, mmiliki wa jumba hilo ameweka pia pingamizi kuzuia kubomolewa kwa nyumba hiyo.

Awali, Heche alikaririwa akisema kuwa baadhi watu wanaomiliki viwanja katika maeneo hayo waliendelea kujenga majumba ya kifahari licha ya zuio hilo lilitolewa zaidi ya mara tatu.

Kwa mujibu wa watu waliokuwa katika eneo hilo, nyumba hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.5.

Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, Mchungaji Rwakatare hakupatikana kuzungumzia hatua yake ya kuamua kuweka pingamizi. Hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Halmashauri ya Manispaa Kinondoni imesema haikuhusika na ubomoaji wa majumba hayo na kusema NEMC ndiyo wanaohusika na ‘bomoabomoa’ hiyo.

Afisa Habari wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera, alisema katika zoezi hilo Manispaa walikuwa watazamaji tu.

Alisema kwa sababu hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Fortunatus Fwema, pamoja na watendaji wengine wa manispaa hawafahamu chochote kuhusu zoezi hilo.

“Hatukuiona ‘Stop Order’ (amri ya zuio) ikitolewa kutoka mahakamani, hatukupewa chochote wala hatukuambiwa kitu. Nenda NEMC ndiyo watakuwa wanajua kila kitu juu ya zoezi lile,” alisema Mhowera.

Majumba hayo yalibomolewa katika operesheni ambayo pia ilihusisha Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi, Julai 7, mwaka huu, lakini jumba hilo liliachwa kutokana na kuwapo zuio hilo.

Hatua hiyo ilichukuliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa tamko la Makamu wa Rais la mwaka 2004, ambalo lilitaja maeneo tengefu ambayo yalipaswa kuhifadhiwa, zikiwamo fukwe za bahari ambazo zina mikoko, ambayo ni mazalia ya samaki baharini.

Licha ya tamko hilo na sheria mbalimbali, maeneo ya fukwe za bahari yamekuwa yakivamiwa.

Katika kusimamia sheria na tamko hilo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Kitengo cha Hifadhi ya Misitu, NEMC pamoja na manispaa hiyo, ziliamua kuratibu bomoabomoa ya majumba hayo yaliyojengwa katika maeneo tengefu ya Bahari ya Hindi.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa NEMC, Dk. Robert Ntakamulenga, alikaririwa akisema nyumba 27 kati ya hizo 15 zikiwa zimekamilika ujenzi wake, nane uzio (fence) na nyingine katika hatua za awali za ujenzi, zilibomolewa.

Kazi ya kubomoa nyumba hizo ilifanywa na kampuni ya Majembe Auction Mart. Bomoabomoa hiyo ilianzia katika eneo la Hifadhi ya Mikoko, Mbezi Beach.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake