Wednesday, September 12, 2012

SIRI ZA WAPENZI KUTOKUCHOKANA!

NINA furaha sana moyoni. Hii ni kwa sababu ninakwenda kukupa kitu kizuri sana ambacho kitakusaidia katika maisha yako ya uhusiano. Kwa hakika hutajutia muda wako kusoma ukurasa huu.
Marafiki zangu, ukisoma kichwa cha habari kwa haraka, unaweza kuona kama mada ni ya kawaida sana, ambayo imezoeleka katika jamii yetu. Let me tell you something; it’s not as simple as many people think. There is a big thing which you are going to learn.
Kuchokana ni tatizo kubwa tena linalogharimu uhusiano wa wengi. Wanashindwa kufanya mambo mengine ya msingi kwa sababu ndani ya nyumba hakuna furaha. Hakuna maelewano. Kama yapo ni ya kuigiza tu.

Kwa nini yote hayo? Wamechokana. Kitu kikubwa kwako ni kutuliza ubongo wako sawasawa kuweza kupokea kitu cha kipekee na cha tofauti kabisa. Je, unahisi kumchoka mpenzi wako? Unadhani mwenzi wako amekuchoka? Leo unakwenda kupata ufumbuzi.

KUCHOKANA NI NINI HASA?
Unaweza kutafsiri vyovyote uwezavyo. Kila mmoja anaweza kuwa na maana yake kwa mtazamo wake, lakini mwisho maana huwa ni moja tu, kuchokana! Kimsingi ni neno linalotokana na kuchoka.
Wengi wanafahamu vyema maana ya uchovu. Hapa kwenye All About Love, tafsiri moja rahisi ni kumuona mwenzako wa kawaida. Kumzoea kupita kiasi na kuhisi wa kawaida tu (kumshusha thamani).
Ukimchoka mpenzi wako ni vigumu hata kuhisi kukutana naye faragha. Wa nini? Unamchukulia wa kawaida tu, kama sehemu ya maisha yako, lakini si muhimu wala wa kipekee kama ilivyokuwa mwanzo. Umenipata ninachozungumzia? Tuendelee kujifunza. 

NI KWELI WAPENZI HUCHOKANA?
Wapo  wasioamini kama kuna suala la wapenzi kuchokana. Kama wewe ni mmoja wapo, unawaza tofauti sana rafiki yangu. Kuchokana kupo kwenye mapenzi. Kuna sababu kadha wa kadha zinazosababisha hali hiyo, lakini nyingi ni zile za kujisahau zaidi!
Tatizo hili huwaathiri zaidi wanandoa (hasa waliopata watoto), wale ambao hawana, tatizo huanza kujitokeza katika umri wa ndoa wa kuanzia miaka miwili na kuendelea.
Kwa mapenzi ya siku hizi, hata miezi sita tu ya mwanzo wa ndoa, wenzi huanza kuchokana kwa sababu mbalimbali. Unajua kinachotokea baada ya wenzi kuchokana? Darasa linaendelea...

HALAFU...?
Matokeo ya yote hayo hapo juu si mazuri. Ni usaliti. Ukimchoka mume/mke wako, maana yake huwezi kuwa naye, utajilazimisha inapobidi. Kama mwanaume akimchoka mkewe ni hatari zaidi, maana anaweza kukaa kimya bila kutaka kukutana naye, wakati yeye akiendelea na mambo yake huko nje.
Mwanamke kwa sababu ameumbwa na woga, si mwepesi kuwa wa kwanza kutaka faragha na hapa ndiyo chanzo cha yeye kusaka pumziko nje ya ndoa yake. Mwanaume anasaliti na mke naye anasaliti. Unaona matatizo hayo?
Mazoea ninayoyazungumza hapa huzorotesha ubora wa tendo la ndoa. Kwa kuwa mnaonana wa kawaida, hata faragha yenu haiwezi kuwa ya mahaba. Kwa mtindo huo ni dhahiri kwamba, kila mmoja atakuwa anabaki na kiu yake na huenda akafikiria kutafuta mahali pa kuikata!
Habari mbaya zaidi ni kwa wanawake ambao wengi hubaki na maumivu kwa muda mrefu. Nimeshakutana na kesi za namna hiyo mara nyingi sana. Ngoja nitakupa mifano mitatu tu ya haraka.
WASIKIE HAWA...

Msomaji wa kwanza:     
Kaka Shaluwa mimi nina mpenzi wangu, nimedumu naye kwa miaka mitatu sasa. Tatizo kubwa ni kwamba mwenzangu hajawahi kumaliza haja zangu hata siku moja.
Kila siku amekuwa akifurahia peke yake na kuniacha kama nilivyokuwa mwanzoni. Tatizo ni nini? Naomba msaada wako.

Msomaji wa pili:     
Hi kaka Shaluwa. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24, nina mpenzi wangu, mtu mzima kidogo. Tuna miaka miwili tangu tumeoana. Tumebahatika mtoto mmoja wa kiume. Tatizo ni kwamba sijawahi kufurahia tendo hata mara moja.
Nimeshawaza kutoka nje, lakini naogopa maana nampenda sana na ninaogopa akijua anaweza kuniacha. Tafadhali kaka, nisaidie kuokoa ndoa yangu.

Msomaji wa tatu:    
Habari. Mimi ni mama nina umri wa miaka 34, nina watoto wanne, naishi Tabora na mume wangu. Nina tatizo katika ndoa yangu. Mume wangu hanipi starehe faragha. Huwa ananirukia mara moja tayari...ananiacha nipo vile vile.
Nini tatizo kaka yangu? Naomba unisaidie tatizo hili tafadhali. Sitaki kutoka nje ya ndoa yangu, bado nampenda sana mume wangu. Nifanyeje?

UMEJIFUNZA NINI?
Bila shaka kupitia maelezo yao kuna vitu umejifunza. Kipo kitu zaidi cha kuzungumza marafiki zangu. Wiki ijayo tutaendelea na mada hii. Ahsante kwa kunisoma, usikose.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, amendika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

1 comment:

  1. nishakutana na kesi hizi kwa baadhi ya marafiki zangu wanawake/wanaume, ila jee huwa mnaongea? labda mwenzio hajui unapenda nini.tukumbuke kuwa hakuna mapenzi matamu kama ya kuanza na romance, wengine wanafikiri romance ni kunyonyana ndimi tu! la hasha! kuna vitu vingi tu vyakufanya ili kufurahia tendo hilo. Na usafi wa mwili pia unatakiwa.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake