ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 16, 2012

Baraza la Katiba sio Uamsho B, asema Profesa

Mjumbe wa Baraza la Katiba la Zanzibar ,kutoka ZLS Abdalla Juma akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani kuhusu kuanza kwa mchakato wa Pili wa Utoaji wa Elimu ya Katiba kwa Wananchi wa Zanzibar utakao anza kesho katika Ukumbi wa Salama Holl Bwawani Mjini Zanzibar.
Mjumbe wa Baraza la Katiba la Zanzibar ,kutoka ZLS Abdalla Juma akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza kwa mchakato wa Pili wa Utoaji wa Elimu ya Katiba kwa Wananchi wa Zanzibar utakao anza kesho katika Ukumbi wa Salama Holl Bwawani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Program za Baraza la Katiba Zanzibar Prof,Abdull Sharif akifafanua masuala yalioulizwa na Waandishi wa Habari kuhusiana na kuanza kwa mchakato wa Pili wa Utoaji wa Elimu ya Katiba kwa Wananchi wa Zanzibar utakao anza kesho katika Ukumbi wa Salama Holl Bwawani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Program za Baraza la Katiba Zanzibar Prof,Abdull Sharif akiwaonesha Waandishi wa Habari Vitabu vya Katiba vilivyoandikwa kwa njia nyepesi ilikufahamu Wananchi wakati wa kuanza kwa mchakato wa Pili wa Utoaji wa Elimu ya Katiba kwa Wananchi wa Zanzibar hapo kesho katika Ukumbi wa Salama Holl Bwawani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar Professa Abdull Shareef akiwaonesha Waandishi wa Habari Vitabu vya Katiba vilivyoandikwa kwa njia nyepesi ili kuweza kufahamika kwa Wananchi wakati wa kuanza kwa mchakato wa Pili wa Utoaji wa Elimu ya Katiba kwa Wananchi wa Zanzibar hapo kesho katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar. Pembeni yake ni Salma Said

NA Salma Said, Zanzibar.
BARAZA la Katiba la Zanzibar limesema mchakato wa utoaji wa elimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu ya tatu umeanza tena kwa wananchi wote katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Professa Abdul Sharif aliwaambia waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari ya (MAELEZO) Zanzibar, kwamba mchakato huo wa utoaji wa maoni utaanzia kwa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kufanyika kungamano kubwa leo katika hoteli ya Bwawani litakalowajumuisha wananchi mbali mbali.Hata hivyo Baraza la Katiba lilikanusha kuwa na mitazamo kama ya Uamsho na kusema kwamba kawaida wazanzibari wanapotoa maoni sawa huwa wanashabihishwa na chama au kikundi fulani lakini alikanusha kuwa wao ni Uamsho na kusema kwamba wazanzibari wamekuwa na maoni sawa katika suala la kutaka mamlaka ya Zanzibar.

“Tatizo kwa Zanzibar mtu anapotoa maoni yakawa yanafanana au kushbihiana na taasisi nyengine basi huwa anaambiwa yeye ni Uamsho, lakini jambo la kushangaza ni kuwa maoni kama hayo ya Uamsho yametolewa nata na watu wakubwa serikalini maana hata Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Nahodha alisema mbele ya tume ya katiba kuwa anapendekeza Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili na tena yeye kenda mbali zaidi alisema kuwe na mabunge mawili,” alisema Professa Shareef.

Alisema Awali Jumuiya ya Uamsho ilikuwa na khofu na baraza la katiba likiamini kwamba ni wasaliti kwa kuwa linakubali kuingia katika mchakato wa katiba lakini baada ya kukaa pamoja na kuongea wakafahamu kwamba baraza la katiba halina msimamo na wala halifanyi kazi za serikali bali lipo huru katika kazi zake.

“Uamsho walikuwa na khofu na sisi na mwanzo walikuwa wakitwambie kuwa ni wasaliti na walidhani tunafanya kazi na serikali lakini sisi hatufanyi kazi na serikali kabisa sisi ni taasisi huru zenye kutoa elimu kwa wananchi bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote,” aliongeza.

Professa Shareef alisema wananchi wengi wanafahamu mambo ya katiba yao ingawa baadhi yao wahawezi kutenganisha vipengele na kuvielewa lakini wanafahamu baadhi ya mambo kama ni kikwazo ndani ya katiba yao huku akitoa mifano ya wafanyabiashara wanapotoleshwa kodi mara mbili wanapokwenda Tanzania Bara huwa wanajua kuwa hilo ni tatizo.

“Hatupendi kusema wananchi hawatambui katiba yao kwa sababu wanajua mambo mengi mfano watu wanapokwenda kule Bara na biashara zao huku Zanzibar wameshalipa kodi na wakifika kule wanalipishwa tena sasa hapo wanajua kuwa tatizo hilo linatokana na mfumo uliopo katika katiba ila hawajui ni ibara ya ngapi inasema kuwa jambo hilo kama ni la muungano au sio muungano,” alisema.

Professa alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari kutaka kujua iwapo watajitokeza sasa katika jamii hawataonekana kuwa wao ni Uamsho B na kuletamigingano mengine kati yao na serikali, Professa Shareef alisema wapo watu watakaodhania hivyo lakini kwa kuwa ni tabia za kibinaadamu wao watahakikisha wanatoa elimu na kufanya kazi zao kama kawaida kwa kuzingatia sheria na kanuni za tume ya katiba inavyoelekeza.

Baraza la Katiba Zanzibar limeundwa na taasisi za kiraia ikiwemo Jumuia nne za kijamii ambazo ni Zanzibar India Ocean Reseach (ZIORI) Chama Cha Wanasheria (ZLS) Kituo cha Huduma Zanzibar (ZLSC) na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA).

Professa Shareef alisema baada ya kuona kuna haja ya kupanua wigo walizualika taasisi nyengine kama Jumuiya ya Walemavu Zanzibar, Zanzibar Youth Forum (ZYF), Chama Cha Waandishi wa Habari Wanazake (TAMWA), na Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA)

Professa Shareef alisema utoaji wa elimu ya katiba ulioanza 2010 ni mchakato endelevu na utaendelea na ratiba zake katika awamu hii ya tatu hadi April mwaka 2014 hadi kupatikana kwa katiba mpya, ambapo awamu ya kwanza na ya pili zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaelimisha wananchi katika maeneo mbali mbali.

“Baraza la katiba lilianza kazi muda mrefu na tumewaelimisha wananchi wengi katika suala la katiba na kazi zetu tunazifanya kwa uwazi na huwa tunachapisha vitabu ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kwani tunataka wananchi waweze kufahamu katiba yao,” alisema Professa.

Alisema lengo la utoaji huo wa elimu ni kuwafanya wananchi wote waweze kutoa maoni yao kwa kujua wanapofika katika tume ya katiba ambapo tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi hivi Novemba 19 mwaka huu katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Lengo ni kuendeleza mchakato wa kutoa taaluma kwa wananchi ili kuweza kushiriki katika kutoa maoni yao yatakayosaidia katika uundwaji wa katiba mpya”alisema Profesa Shareef.

Mjumbe wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLC), Abdalla Juma Mohammed wao kama wanasheria wanatambua ugumu uliopo wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa suala la katiba ni gumu kufahamika katika jamii kiurahisi.

Alisema wamechukuwa hatua hiyo baada ya kujuwa kwamba mambo ya katiba yanahitaji ufafanuzi mkubwa kutokana na lugha inayoandikwa katika katiba inakuwa ya kitaalamu zaidi na ni vugumu kufahamika kwa mara moja na watu wa kawaida ambao ndiyo wengi ikiwemo wa vijijini.

Akifafanua zaidi alisema baraza la katika litakuwa likizunguka sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba kwa ajili ya kufanya mikutano na kutoa elimu kuhusu katiba lakini kamwe halitakuwa likishindikiza na kutoa msimamo wake.

‘Sisi kazi yetu kubwa kutoa elimu kuhusu katiba na mchakato wa marekebisho ya katiba kwa lengo la kuona tunapata katiba nzuri hatuwalazimishi watu wachague mfumo gani sisi tunatoa elimu katika mifumo tulionayo na kuonesha changamoto zake,” alisema Juma.

Alisema wananchi wanapaswa kuwa na misimamo yao baada ya kupata taalum hiyo ya katiba na kazi ya kuchagua mfumo wautakao ni maamuzi ya wananchi wenyewe lakini lengo kila mwananchi afahamu anachokwenda kuchangia katika tume ya katiba.

Juma akizungumzia utendaji wa kazi zao alisema wanafanya kazi kwa kufuata taratibu za tume ya katiba ya kupeleka barua ya kuitaarifu tume ya katiba labla hawajamua kuanza kutoa elimu katika maeneo ambayo wanahitaji kufanya mikutano yao.

Tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano inatazamiwa kuanza kazi ya kukusanya maoni kwa wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wiki ijayo ukiwa mkoa wa mwisho kati ya mikoa mitano ya Zanzibar

No comments: