Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kauli iliyotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuwa anakusudia kumshtaki Rais bungeni ni yake binafsi na kwamba chama makini hakiwezi kutoa msimamo huo mzito bila kufanya tafakari makini.
Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kueleza kuwa anakusudia kupeleka bungeni hoja maalum ya kumshtaki Rais ikiwa atashindwa kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa Katiba katika uteuzi wa majaji.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi, alisema hakuna kikao chochote cha chama kilichomuidhinishia Lissu kutoa tamko hilo.
“Chama chochote makini cha siasa hakiwezi kuchukua maamuzi kama hayo bila kufanya tafakari ya kina kuhusiana na jambo hilo…kama halitafanikiwa jambo kama hilo litakidhalilisha chama. Ni vizuri jambo lolote ambalo chama kinakusudia kulifanya liungwe mkono na wananchi,” alisema.
Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alisema katika kikao cha chama hicho watakachokaa wakati wowote kabla ya mwishoni mwa mwaka, watatoa tamko kwamba matamko yote lazima yapate ridhaa ya chama husika.
Alisema suala hilo linahitaji kuungwa mkono na wabunge kutoka vyama vingine kwa kuwa idadi ya wabunge wa Chadema ni 48 tu wakati idadi ya wabunge wanaohitajika kutia sahihi katika hoja ili ipelekwe bungeni ni 72.
Idadi ya wabunge wote kutoka vyama vya upinzani ni 91.
Kuhusu Lissu kulizungumzia jambo hilo ambalo lilifanyiwa kazi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na bado halijawasilishwa bungeni, Arfi alimtaka Mbunge huyo kufuata sheria za nchi.
Alisema Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inataka kutotolewa hadharani kwa jambo lolote lililojadiliwa faragha na kwamba anayekiuka anakabiliwa na kosa la jinai.
Hata hivyo, alisema Lissu kama walivyo wabunge wengine anayo haki ya kuzungumzia jambo lolote ili mradi havunji kanuni na sheria za nchi.
LISSU AJIBU
Lissu alipoulizwa kuhusiana na jambo hilo, alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, suala la kupeleka hoja binafsi ni la Mbunge mwenyewe na wala sio chama.
“Kama yeye (Arfi) anaamini ni vyema tuache majaji wafanye kazi hivyo hivyo bila kuwa na elimu inayostahili hayo ni yake mimi siwezi kusema kitu,” alisema Lissu.
Juzi Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hoja hiyo anakusudia kuiwasilisha katika mkutano ujao wa Bunge wa Februari mwakani iwapo Rais hatafuta uteuzi wa majaji hao.
“Tunamtaka Rais afute uteuzi wao haraka iwezekanavyo kama hatafuta uteuzi basi sisi kama Kambi ya Upinzani tutaanzisha mchakato wa kumshitaki,” alisema na kuongeza: “Tunaenda kuandaa hoja maalumu na hoja hiyo inatakiwa kusainiwa na asilimia 20 ya wabunge (wabunge 72 na zaidi).”
Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, alidai kusudio hilo linatokana na taarifa waliyoipata kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, amekataa kutoa taarifa ya uchunguzi wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi dhidi ya tuhuma alizozitoa bungeni kuhusu ukiukwaji wa uteuzi wa majaji.
Lissu alisema Oktoba 30, mwaka huu wabunge walifanya kikao cha ndani ili kuzungumzia ratiba ya kikao cha Bunge na Spika alipoulizwa kuhusu taarifa mbili za ripoti za uchunguzi kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya wajumbe waliokuwa Kamati ya Nishati na Madini na ile ya kwake, alikataa na kusema ni za kwake na kwamba halazimishwi kuzitoa na yeye ndiye atakaye jua atazitoa wakati gani.
Katika Mkutano wa Bunge Julai 13, mwaka huu, Lissu alisema baadhi ya majaji walioteuliwa na Rais hawana sifa, uwezo na wala hawakufaa kushika madaraka ya Jaji Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, kauli ambayo ilimsababisha ashitakiwe kwenye Kamati ya Ngwilizi.
Lissu aliwataja kwa majina majaji wanane akisema wanafanya maamuzi yanayowapendelea jamaa zao wa karibu na wengine hawajui kuandika hukumu.
Juzi Lissu alimtaka Spika kutoa matokeo au taarifa ya Kamati ya Ngwilizi ili Bunge lifahamu ukweli ni upi baada ya yeye kutoa ushahidi kwenye Kamati hiyo.
“Kwa maoni yangu, ushahidi wa nyaraka nilizowapa hawawezi kusema nilichosema ni uongo,” alisema na kuongeza:
“Kama majaji wetu hawana sifa, hawana maadili si suala la kuachwa na Spika wala waandishi wa habari kuripoti.”
Alihoji kuwa Jaji ambaye hana hata shahada ya sheria anakaaje mahakamani kutoa haki.
Alisema baadhi ya majaji wameongezewa mkataba kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment