ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 29, 2012

Jaji chande aikwepa kesi ya Lema

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande amejitoa kusikiliza rufaa ya kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, badala yake nafasi yake imechukuliwa na Jaji Bernard Luanda.
Kujitoa kwa jaji mkuu kumekuja ikiwa zimebaki siku tano kusikilizwa upya kwa rufaa hiyo Desemba 4, mwaka huu, baada ya awali Mahakama ya Rufani, kuona rufaa hiyo ilikuwa na dosari.
Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajiburufaa kuwa rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge Lema na vilivyotumika katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa hiyo.
Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya kanuni hiyo, dosari hizo zinaweza kurekebishwa.
Jaji Chande ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu katika kesi hiyo akiwamo Salum Massati na Natalia Kimaro.
Jaji Mkuu aliingia kwenye kesi hiyo akichukua nafasi ya Jaji Mbarouk Salim Mbarouk aliyekuwa amepangwa awali, ambaye sababu za kuondolewa hazikuwekwa wazi.
Wakili wa  Lema, Method Kimomogoro alithibitisha kuwa amepata taarifa kuwa jaji mkuu hatasikiliza rufaa hiyo na badala yake Jaji Luanda ndiye atachukua nafasi yake.
“Ni kweli jaji mkuu hatakuwapo kusikiliza rufaa ya Lema nimewasiliana na Msajili Dar es Salaam ameniambia hatokuwepo kwenye hilo jopo,” alisema Kimomogoro na kuongeza:
Hata hivyo, Wakili Kimomogoro alisema “Huu ni utaratibu wa kawaida wa mahakama kwa kuwa huenda jaji mkuu akawa amesafiri au ana shughuli nyingine.”
Wakili wa wajiburufaa, Alute Mughwai alisema hajapata taarifa kama Jaji Mkuu ameondolewa kwenye jopo hilo kwa kuwa huo si utaratibu wa mahakama kutoa taarifa hizo.
“Mahakama huwa haitoi taarifa, zinawekwa (taarifa) kwenye ubao wa mahakama siku ambayo rufaa inasikilizwa,” alisema.
Aliendelea, “Jaji yeyote atakayepangwa sisi hatuna tatizo kwa kuwa wote ni majaji, wewe uko huko Dar na mimi niko huku bara (Arusha), hivyo unaweza ukazipata taarifa zaidi huko kwa kuwa ndiyo uko jikoni Dar.”
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma alipoulizwa kuhusu suala hilo hakukataa wala kuthibitisha.
Awali alikana kuwa na taarifa kuwa rufaa hiyo imeshapangiwa tarehe ya kusikilizwa na jopo la majaji, huku akihoji ni ratiba gani hiyo inayoonesha hivyo.
Baadaye alisema kuwa hawezi kueleza jambo lolote kuhusu rufaa hiyo kwa mtu ambaye si mhusika.
“Unafuatilia rufaa ya Lema kwani wewe ni mhusika? Wewe si mhusika katika kesi hiyo wala si wakili wa Lema. Mimi siwezi kukueleza lolote, maana mimi siwajibiki kwako, nawajibika kwa Lema, kwanza wewe nilishakwambia lakini bado tu.” alisema Maruma.
Lema mwenyewe alisema hajui kwa nini Jaji Mkuu amejitoa, lakini akaeleza kuwa anajua wanyonge wataendelea kumwomba Mungu ili afanikiwe kwa kuwa hana mashaka na hatua hiyo iliyofikiwa.
“Mimi sikuzaliwa kuwa mbunge na ubunge kwangu siyo ajira, hivyo sina mashaka na kutokuwepo kwa Jaji Mkuu kwenye kesi yangu,”alisema Lema.
Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kutokana na kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu  wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Baadaye alikata rufaa Mahakama ya Rufani, kupitia kwa wakili wake, Method Kimomogoro kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, huku akitoa hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
Tarehe ambayo rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la  majaji watatu Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Natalia Kimaro  na  Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande (kiongozi wa jopo), wakili wa wajiburufaa, Alute Mughwai, aliweka pingamizi la awali.
Katika pingamizi hilo, wakili Mghwai aliiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa ina kasoro za kisheria na za kikanuni huku akibainisha hoja tatu za kuunga mkono pingamizi hilo.
Hoja hizo za pingamizi la awali zilikuwa ni pamoja na kuchanganywa au kutofautiana kwa vifungu vya Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 2010, kati ya hukumu iliyomvua ubunge na hati ya kukaza hukumu hiyo.
Pia hoja nyingine ni kwamba hati ya kukaza hukumu hiyo haikuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe ambayo  hati hiyo ilitolewa.
Hoja ya tatu ilikuwa ni mtindo wa kuandika hati ya kukaza hukumu, kwa kutokuandika maneno, “imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa mahakama.”
Hata hivyo, katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja moja ya pingamizi hilo, kuwa tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria ni dosari ambayo inaifanya hati hiyo isiwe halali na ikatupilia mbali hoja nyingine mbili kuwa hazina msingi.
Mwananchi

No comments: