Sheikh Azzan Khalid Hamad na Sheikh Mussa Juma Issa wakitoka Mahakama Kuu Vuga muda mfupi baada ya kusomesha shitaka lao ambapo wanarudishwa rumande baada ya kunyimwa dhamana,
Wakili wa Uamsho akerwa wateja wake kunyolewa ndevu
VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar wamefikishwa tena mahakamani jana chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi kwa kusaidiana na vikosi vya serikali ya Zanzibar huku Mawakilishi wao wakiendelea kulalamikia serikali kukiuka haki za binaadamu na utaratibu mzima wa kisheria wa uendeshaji wa mashtaka dhidi ya wateja wao.
Mawakili wa viongozi hao watatu ambao ni Abdallah Juma na Suleiman Salum wakiongozwa na Salim Tawfik waliiambia mahakama chini ya Hakimu George Kazi kuwa wateja wao tangu kukamatwa kwao siku 17 zilizopita wamekuwa hawatendewi haki ikiwa pamoja na kunyimwa fursa zote wanazostahiki kupata kama watuhumiwa malalamiko ambayo yalitolewa juzi katika mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe.
Miongoni mwa ukiukwaji wa haki za wafungwa hao ni pamoja na kubadili nguo ambapo tangu walipokamatwa hawajaruhusiwa kubadilisha nguo, kulazimishwa kunyolewa ndevu, kukatazwa kuonana na jamaa zao, pamoja na kutengwa kila mmoja katika chumba maalumu chini ya ulinzi mkali.
Mambo mengine ambayo yameelezwa mahakamani hapo ni kulazwa chini ya sakafu, kujisaidia ndani ya ndoo (mtondoo), na kunyimwa fursa ya kufanya ibada jambo ambalo linakwenda kinyume na katiba kuhusu haki ya kuabudu na kufungiwa ndani ya vyumba saa 24 mambo ambayo hayapaswi kufanyiwa kwa sababu bado ni watuhumiwa hawajatiwa hatiani na ni kinyume na haki na binaadamu na kinyume na katiba.
Wakinukuu baadhi ya vifungu vya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1988 inayotoa fursa ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria, haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, mawakili hao wamedai kuwa wateja wao wamekuwa wakikosa haki hizo na kutendewa tafauti na watuhumiwa wengine waliopo rumande.
“Haki za washitakiwa hawa zinavunjwa wazi wazi na maofisa wa Vyuo vya Mafunzo na serikali kwa ujumla, hawa raia kama raia wengine wanapaswa kupatiwa haki zao zote za msingi wanazostahiki kwani hapo ni watuhumiwa lakini wanafanywa kama wameshatiwa hatiani Mheshimiwa”, alidai Wakili Salum Taufiq.
Wakili Tawfik aliiomba mahakama pamoja na serikali kuacha kuvunja sheria na haki za watuhumiwa hao kwa sababu ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na mahakama haipaswi kunyamazia ukiukwaji huo unaotendeka dhidi ya watuhumiwa.
“Mheshimiwa wateja wetu hawana fursa ya kusali sala ya Ijumaa na wenzao, hawana vitabu vya dini wakati tunafahamu hawa ni viongozi wa dini, hata ndevu wamenyolewa ili kuwadhalilisha na wamefanyiwa kwa makusudi ili kuwavunjia heshima zao katika jamii wakati ni kinyume na katiba kwani kama tunavyofahamu kufuga ndevu kwa muislamu ni sunna na ni ibada lakini kumnyoa ndevu ni sawa na mkristo kumvua msalaba”, alisema mahakamani hapo Wakili huyo.
Akijibu malalamiko hayo upande wa mashtaka kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtama Zanzibar, ukiongozwa na Ramadhan Nasseeb walionekana kutorishika na tuhuma hizo za kukiuka haki za watuhumiwa na kutaka upande wa utetezi wa watuhumiwa kufungua kesi ya madai kupinga hayo kwa sababu kesi dhidi ya watuhumiwa ni kesi ya jinai.
“Sisi kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hatupendelei kuona haki haitendeki pamoja na ukiukwaji wa haki za binaadamu unaodaiwa hapa sisi ni wajibu wetu kuhakikisha vyombo vya sheria vinavyohusika vinatekeleza sheria na kufuata katiba lakini pamoja na hilo, naiomba mahakama malalamiko haya yanayotolewa na upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao hizi katika mahakama husika kwa vile hoja zao hizo zimegusia ukiukwaji wa Katiba na hii ni kosa ya jinai sasa wamefungue kosa ya madai” alisema Nasseeb.
Jopo la Wanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), wengine ni Rashid Fadhil na Raya Issa Mselem, umeiomba mahakama kwamba, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Hivyo, waliiomba mahakama hiyo kuliahirisha shauri hilo, na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, ili iweze kupatikana muda wa ziada wa kuendelea na upelelezi huo.
Naseeb alidai Mahakama hapo kwamba Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye kusimamia na kusikiliza mashauri yote ya ukiukwaji wa Katiba yanayowasilishwa mbele yake kwa ajili ya kutolewa maamuzi na hivyo kuwataka watuhumiwa wafungue kesi ya madai.
Kwa upande wake Mwanasheria wa serikali, Raya Issa Mselem aliiambia mahakama hiyo isiyatilie maanani hoja hizo za upande wa utetezi kwa madai kuwa hapo si pahala pake na kusisitiza kufuata taratibu za kisheria kwa kufungua kesi ya madai.
“Mheshimiwa maombi yao yatupiliwe mbali, wapewe maelekezo maalumu ya kuona wapi haki za washitakiwa zitapatikana hapa tupo katika kesi ya jinai na hayo malalamiko yao ni ya madai kwa hivyo wafuateutaratibu”, alidai Mwanasheria huyo wa serikali Raya.
Akijibu hoja hizo Wakili Tawfik alisema watuhumiwa wamevunjiwa haki zao za msingi na hakuna sehemu nyengine ya kupatikana haki zaidi ya mahakamani na hivyo kuiomba mahakama kuzingatia hilo kwani wateja wake hawana hamu ‘intrest’ ya kufungua kesi ya madai.
“Mheshimiwa wateja watu wamevunjiwa haki zao za msingi mambo mengine hayahitaji kujua katiba wala nini kumvunjia mtu haki yake mfano kumnyoa ndevu na wao ni waislamu na ni viongozi wa dini na kufuga ndevu ni sunna na ni sehemu ya ibada kwao wao hilo linafahamika na halihitaji kujua katiba katika hilo kila mmoja anajua kama hapo haki imevunjwa, na tunaposema kwamba wamevunjiwa haki zao hatuna intrest ya kufungua kesi ya madai ya kutaka warejeshewe ndevu zao au wadai fidia kwa kunyolewa ndevu lakini tunachotaka kusema haki zao zinavunjwa na mahakama isimamie hilo” alisema Tawfik wakati akibishana katika vifungu vya sheria na wanasheria wenzake wa serikali.
Viongozi wote wanane wanashitakiwa kwa matukio mbali mbali ya uharibifu wa mali, uchochezi, uvunjifu wa amani pamoja na kupanga nyama za kumficha Sheikh Farid, wamerudishwa rumande baada ya kunyimwa dhamana ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim kuwafungia dhamana washitakiwa hao kwa maslahi ya umma, chini ya kifungu cha 19 (1) (2) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana kuendelea na kesi yao hiyo, wakitokea rumande ya Chuo cha Mafunzo kilimani, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)waliovaa mavazi ya kujihami wakiwa na silaha nzito nzito ambapo kesi yao imesikilizwa bila ya kuwepo jamaa na familia zao.
Hakimu baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ambaye pia ni Mrajis wa Mahkama kuu Zanzibar George Kazi amesema atatoa uamuzi wa malalamiko hayo Novemba 20 siku ambayo imepangwa kutajwa kesi hiyo.
Washitakiwa hao ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni, Mselem Ali Mselem (52) wa Kwamtipura, Mussa Juma Issa (37) mkaazi wa Makadara, na Azzan Khalid Hamdani (48) mkaazi wa Mfenesini Unguja
Wengine katika kesi hiyo ni Suleiman Juma Suleiman (66) Mkazai wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) mkaazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakari Suleiman (39) Mkaazi wa Tomondo na Ghalib Ahmada Omar (39) mkaazi wa Mwanakwerekwe Unguja.
Muda mfupi baada ya kuakhirishwa kwa kesi hiyo, washitakiwa hao waliingizwa katika gari ya Polisi yenye nambari za usajili PT 1891 ya OCD Mjini, ikiambatana na gari yenye nambari PT 0873 ya FFU Mjn (M), PT 1449 Polisi ZPA 0001, PT 1407 ya Ufundi/Ujenzi na PT 2086 ya FFU KAS (U) kwa ajili ya safari ya makaazi yao ya muda ndani ya Chuo cha Mafunzo.
Washitakiwa wote hao wanakabiliwa na mashitaka ya uvunjifu wa amani, ushawishi wa kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na shitaka la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, kosa hilo lililokuwa likimkabili Azzan Khalid Hamdani pekee yake.
Awali mahakamani hapo washitakiwa hao walisomewa mashitaka ya uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002, kwa kuhusishwa na matukio yaliyotokea Oktoba 17 na 18 mwaka huu kuanzia saa 12:00 za asubuhi hadi usiku wa manane.
Katika shitaka hilo, kupitia barabara tofauti zilizomo ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja walidaiwa kuharibu barabara, majengo, vyombo vya moto ikiwemo na pikipiki na magari, na walifanya hivyo bila ya kuwepo sababu za msingi za kuharibu na kuteketeza kinyume cha maslahi ya umma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi 5,000,000 Millioni.
Shitaka la pili lililokuwa likiwakabili ni la ushawishi na uchochezi, ambapo ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa baina ya Mei 26 hadi Oktoba 19, 2010 walifanya mikutano katika maeneo tofauti yakiwemo Lumumba, Msumbiji, Fuoni Meli sita na Mbuyuni, ambayo kwa nyakati tofauti walishawisi na kuchochea watu kufanya makosa.
Makosa waliyodaiwa kufanywa ni kuweka vizuizi barabarani kwa kutumia mawe,, makontena ya kuhifadhia taka, matawi ya miti, mapipa ya mafuta, kuchoma maringi ya magari, kuharibu majengo tofauti, magari na kusababisha huduma muhimu za jamii za serikali kuweza kuharibwa na kusimamisha watu kufanya shughuli zake.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa shitaka la mwisho kwa washitakiwa wote hao lilikuwa ni la kula njama, ambapo sehemu tofauti zisizojulikana pamoja na muda wake ndani ya wilaya ya Mjini Unguja, kwa pamoja walidaiwa kula njama ya kusababisha Sheikh Farid Hadi Ahmed kujificha katika sehemu ambazo hazijulikani na kupelekea uvunjifu wa amani katika jamii kwa siku kadhaa.
Na shitaka la nne ambalo linamkabili Sheikh Azzan Khalid peke yake ni kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, pamoja na kumtolea maneno ya kashfa na matusi Kamishna wa Polisi wa Zanzibar.
Matusi hayo ya Sheikh Azzan ilidaiwa kuwa alimwambia Kamishna huyo kuwa mjinga, jambo ambalo mahakama ilidaiwa kuwa lingeliweza kusababisha uvunjifu wa amani chini.
Mashitaka yote hayo hawakutakiwa kujibu chochote mara baada ya kusomewa mahitaka yao mahakamani hapo na badala yake watajibu mahakama Kuu mara baada ya upelelezi wake kukamilika, kutokana na kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za aina hiyo. Juzi katika mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe wahutumiwa wote hao walipewa dhamana lakini yenye masharti magumu kuyatekeleza.
Masharti waliopewa katika mahakama ya wilaya ni kutakiwa kuwasilisha shilingi millioni moja taslim kwa kila mmoja wao, na kuwa na wadhamini watatu wawe wafanyakazi wa serikali ambao kila mmoja pia anatakiwa kuwasilisha kiwango kama hicho cha fedha jumla shilingi Millioni 4 kila mtuhumiwa) pamoja na kuwa na kitambulisho cha mzanzibari mkaazi, au pati ya kusafiria pamoja na barua ya kiongozi wa mtaa (Sheha).
No comments:
Post a Comment