ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 30, 2012

Jinsi watawala wanavyowatumia wasomi wetu


Rais wa Zainzibar Dkt. Shein, wakipongezana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zainzibar Maalim Seif na Rais mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Karume, kwenye baraza la Idd, 2010

TAKRIBAN nchi zote za Kiafrika zimeshuhudia jinsi baadhi ya raia wake walivyojilimbikizia utajiri mkubwa na fedha nyingi mno wakiwa katika vivuli vya utawala. Baadhi yao ni watawala wenyewe…
Wengine wanawatumia hao watawala au mfumo uliopo wa utawala kujipatia mali hizo. Mara zote njia wanazozitumia huwa si za halali.
Hali hiyo haikuanza leo wala jana barani Afrika. Ibn Khaldun aliyefariki dunia 1406 aliyaona hayo zama zake. Bwana huyo alizaliwa Tunis na mababu zake walitokea Hadhramaut, Yemen Kusini.
Miongoni mwa fani alizosomea utotoni mwake ni isimu ya lugha ya Kiarabu, hisabati, mantiki na falsafa. Aliandika kitabu chake cha mwanzo akiwa na umri wa miaka 19. Ibn Khaldun anatambuliwa kuwa ndiye baba wa uandishi wa historia, wa elimu-jamii (sosiolojia) na wa sayansi ya uchumi.
Baada ya kuipata taalimu yote aliyojaaliwa kuipata Ibn Khaldun alifanya kazi serikalini akishika nyadhifa kadhaa za kisiasa pamoja na uwaziri. Wakati mmoja alikorofishana na mtawala Ibn Amar Abdullah na akaamua kuhama Tunis na kwenda Granada, Hispania, ambako alishika nyadhifa kubwa kubwa chini ya Sultan Muhammed wa tano. Siku hizo Hispania ilikuwa dola ya Kiislamu. Baadaye Sultani alimrejesha kwao Ibn Khaldun baada ya kuzuka uhasama baina ya waziri wake mmoja na Ibn Khaldun.
Aliporudi Afrika Ibn Khaldun alikaribishwa kwa mikono miwili na mtawala na akateuliwa waziri mkuu. Kutokana na muda wake mrefu katika duru za watawala Ibn Khaldun aliona mengi. Moja aliloliona na kulitaja ni kwamba ufisadi na udikteta ni pacha.
Na si lazima pawepo ufisadi wa kupora mali. Wanachofanya madikteta wengine — na huo pia ni aina ya ufisadi — ni kuwatunukia akina ‘hewalla bwana’ vyeo vikubwa wasivyostahili na mishahara minene au manufaa na marupurupu mengine.
Wanapoonyesha dalili ya kwenda kinyume na mtawala au hata pale mtawala anapokuwa na shaka nao basi vibarakala akina ‘hewalla bwana’ hupokonywa ulwa waliotunukiwa.
Katika mfumo huo mtawala analazimika kila mara kuwa na kitu cha kuwapa vibarakala au hata kuwapokonya walicho nacho ili hao watawala waweze kuidhibiti dunia yao.
Ufisadi wa aina hiyo hutokea hata katika nchi za kidemokarasia. Hivyo, si ajabu kwamba ufisadi wa aina zote umekithiri katika nchi zetu tangu wimbi la demokrasia lianze kung’uruma barani Afrika. Hii leo takriban kila nchi inaiigiza kivyake dhana hiyo.
Juu ya hayo si nyingi ya nchi za Kiafrika zilizo na mfumo wa demokrasia iliyokomaa. Nchi nyingine zimekuwa zikijitia tu katika mkumbo wa demokrasia kwa vile zilikuwa hazina hila ila kujifanya kuukubali mfumo huo. Ziliukubali shingo upande mfumo huo kutokana na mashinikizo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Kuna wenye kuipima demokrasia kwa kigezo cha uchaguzi lakini hicho ni kigezo kimoja tu. Tena kina mushkili wake kwani hata hicho kinatakiwa kiwe na sifa fulani. Kati ya sifa hizo ni kwamba uchaguzi uwe huru, wa haki, uliofanywa kwa uwazi kabisa na uwe wa kuaminika na wenye matokeo yasiokanika.
Ikiwa tutakitumia kigezo hicho cha uchaguzi na sifa hizo tulizozitaja basi ni nchi chache za Kiafrika zinazostahiki kuitwa za demokrasia halisi.
Katika miaka toka ya 1960 hadi 1990 mtindo uliokuwapo ni kwa serikali za Kiafrika kubadilishwa kwa njia ya mapinduzi ambayo mara nyingi yaliwaua viongozi. Baada ya muda walioua nao pia wakiuawa kwani kulikuwa hakuna mfumo mbadala wa kubadilishana madaraka.
Mtindo huo wa kupinduana haukuwa ukiendeshwa na wanakwaya wa kanisani. Ulikuwa ni mfumo wa kikatili ulioendeshwa na makatili.
Mtindo huo uligeuka na kuwa kama mila ya Afrika. ‘Udikteta wa Kiafrika’ ukawa unatumia mantiki ya kikatili na ya umwagaji damu. Lakini kila pale demokrasia ilipotia mizizi medani huwa si tena uwanja wa kunyakua madaraka.
Siku hizi kwingi Afrika madaraka hupatikana kwa yaliyomo kwenye madebe au visanduku vya kura na si kwa mtutu wa bunduki. Na Afrika hatuna upungufu wa visanduku vya kura. Taksiri iliyopo ni kwamba visanduku hivyo huwa ama vimekwishajazwa kura kabla ya wapiga kura kutumbukiza kura zao au hujazwa baadaye kwa kura za bandia. Hapo ndipo penye tatizo. Hapo ndipo tunapoweza kutofautisha baina ya demokrasia halisi na ile ya shaghalabaghala.
Kwa hivyo haitoshi nchi kujinata kwamba inafuata demokrasia. Katiba za nchi nyingi za Kiafrika zinasema kwamba zinaufuata mfumo huo. Lakini katika nchi hizo kuna pengo kubwa baina ya nadharia na vitendo, baina ya kilichomo ndani ya katiba na kinachotendwa na serikali na wakubwa wake.
Katika nyingi ya nchi za Kiafrika demokrasia imegeuzwa na kuwa tamthilia. Na sisi raia tumekuwa waigizaji wa tamthilia ya kidemokrasi. Watawala wetu ni wasanii mahiri. Wametuwekea majukwaa na yote yanayohitajika katika majukwaa hayo pamoja na maneno yote ya Kimagharibi yanayohitajika katika tamthilia hiyo pamoja na wahka na hali ya mshawasha inayozuka wakati wa kuhisabiwa kura.
Sisi tumezoea kuhamaki magazeti ya nchi za Magharibi yanapozielezea chaguzi zetu kuwa kama soko linalofunguliwa katika vipindi maalumu aghalabu vya miaka mitano mitano.
Pengine magazeti hayo yanasema kweli kwani chaguzi katika baadhi ya nchi zetu ni mzaha na viongozi wetu ni machale. Wakati mwingine chaguzi zetu zinakuwa mithili ya dansi kubwa ya vinyago. Ngoma inapomalizika visanduku vya kura hujazwa kura ambazo hakuna aliyezipiga.
Katika nchi zinazofanya uchaguzi wa bandia serikali huwa na uwezo wa kuwakashifu wasomi kwa kuwafanya wayakubali matokeo ya uchaguzi na hata kuwafanya wayathibitishe hadharani matokeo hayo. Hivyo wasomi hao hulainishwa laisa kiasi. Makali yao ya kuusema ukweli yanazimuliwa, wanageuzwa vibarakala na inapohitajika huhongwa marupurupu ya utawala.

No comments: