WIKI hii nimeamua kuuzungumzia utawala bora. Katika kuzipekua pekua kurasa za historia zinazohusiana na utawala bora nimeikuta risala moja iliyoandikwa zaidi ya miaka elfu iliyopita ambayo watawala wa leo wanapaswa wawe wanaipitia pitia mara baada ya mara.
Barua hiyo iliandikwa na Imam Ali bin Abi Talib aliyekuwa binamu na mkwe wa Mtume Muhammad (swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie). Yeye alikuwa khalifa (mtawala) wanne wa Waislamu baada ya kufariki Mtume na barua hiyo alimwandikia Malik al Ashtar aliyekuwa mmoja wa wafuasi wake wakuu na amiri jeshi wa majeshi yake.
Malik alikuwa shujaa na kwa ujasiri wake alipewa lakabu ya ‘chui shupavu.’ Imam Ali alimwandikia risala hiyo alipomteua awe Gavana wa Misri.
Risala hiyo ina mafunzo mengi kuhusu jinsi utawala unavyopaswa uwe. Abdul Masih Ataaki yule Mkristo mashuhuri wa Kiarabu aliyekuwa pia hakimu, mshairi na mwanafalsafa aliyefariki mwanzoni mwa karne ya 20 amezielezea kanuni za utawala zilizomo kwenye risala hiyo kuwa ni adhimu zaidi kushinda zile za Mtume Musa (Moses) na za Hammurabi, mtawala wa Babylon aliyeandika kanuni za sheria kwenye majiwe 12 yaliyowekwa hadharani ili kila mmoja ayaone na kuyasoma. Kanuni yake moja iliyo maarufu ni ile isemayo: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’
Barua hiyo ya Imam Ali ina maneno yanayokaribia elfu kumi. Hapa nitajaribu kudokoa dokoa machache tu yaliyoandikwa katika barua hiyo ya waadhi kuhusu utawala bora.
Kwa hakika mwandishi mwenyewe hakuyaita hayo kuwa ni waadhi au wasaha bali aliyaelezea kuwa ni maamrisho.
Alianza kwa kumjulisha Malik kwamba anampeleka awe gavana katika nchi iliyoshuhudia tawala nyingi kabla yake. Baadhi ya tawala hizo zilikuwa njema na nyingine zilikuwa za kimabavu, za ukandamizaji na za kikatili. Aliendelea kumwambia kwamba watu wataupima utawala wake Malik kama yeye alivyozipima tawala nyinginezo na watamkosoa kama yeye Malik alivyowakosoa au kuwasifu watawala wengine.
Imam Ali aliyadhukuru mambo mengi katika barua yake. Kati ya hayo ni kuwako kwa matabaka katika jamii, umuhimu wa ukusanyaji wa kodi, mahusiano ya mtawala na wafanyabiashara na watasinia, uovu wa magendo, jinsi ufisadi unavyouchimba ustawi wa jamii, aina gani ya watu mtawala anaostahiki wamzunguke na wepi wa kuwahepa. Alimwambia Malik kwamba jambo linalopasa kuufurahisha sana moyo wa mtawala ni kuona kwamba nchi yake inaendeshwa kwa misingi ya usawa na haki na kwamba raia wake wanampenda.
Kuvumilia dini tofauti: Kuhusu hili Ali bin Abi Talib aliandika hivi: Miongoni mwa raia mna watu wa aina mbili: wale wenye kufuata dini kama yako na hao ni ndugu zako, na wale wenye dini nyingine, nao ni binadamu kama wewe.
Watu walio katika makundi yote hayo wana udhaifu uleule na mapungufu yaleyale yanayowasibu wanadamu; wanafanya madhambi, wanajiingiza katika mambo maovu ama kwa makusudi au kwa ujinga bila ya kukusudia na bila ya kutambua ubaya uliokithiri wa matendo yao. Waokoe kwa rehema na huruma yako na kwa kiwango kilekile ambacho unamtarajia Mungu akurehemu na akusamehe.
Kusamehe na Kusahau: Usione haya (au aibu) kusamehe na kusahau. Usikimbilie kuwaadhibu watu na wala usifurahie au kuona fahari kwamba una nguvu za kutoa adhabu. Usikasirike na kupandisha hamaki haraka kwa makosa ya unaowatawala. Hasira na hamu ya kulipiza kisasi haitokusaidia katika utawala wako. Katu usijiambie, “Mimi ndiye Bwana wao, mtawala wao na kwamba lazima wanitii kwa unyenyekevu” kwa sababu fikra kama hiyo itakufanya uchanganyikiwe akili, itakufanya ujinate na uwe na kiburi…
Haki ni bora: Watu wataifurahia sera yenye msingi wa haki. Kumbuka kwamba maudhi ya watu wa kawaida, walalahoi na wa tabaka za chini yana uzito zaidi kushinda sifa za watu muhimu, na ukiwaudhi wakubwa wachache unaweza ukasamehewa ikiwa umma kwa jumla na wengi wa raia wako wanaridhika nawe.
Hakikisha una mahakama aminifu: Lazima uwachague majaji wenye tabia njema na umahiri wa hali ya juu wenye kusifika kwa weledi wao…wasiwe mafisadi, wenye tamaa au waroho. Majaji hawa wateuliwe bila ya upendeleo wa aina yoyote;la sivyo, basi kutakuwako udhalimu, ufisadi na utawala mbovu.
Walipe uzuri ili waweze kukidhi mahitajio yao na wasiwe na haja ya kuombaomba au kukopa au kuingia katika mambo ya ufisadi. Yafanye mahakama yasiwe chini ya shinikizo zozote au tashwishi yoyote ya serikali, yasiwe na woga au mapendeleo, majungu au ufisadi.
Ufukara husababisha maangamizi: Ikiwa nchi ina ufanisi na ikiwa watu wake wanajiweza basi itakubali tena kwa furaha kujitweka mzigo wowote. Umasikini wa watu ndio sababu hasa ya kuteketea na kuangamia kwa nchi na sababu kubwa ya umasikini wa watu ni tamaa ya mtawala wao na maofisa wake kujirundikia utajiri na mali kwa njia za halali au haramu.
Huwa wanachelea kupoteza vyeo vyao au madaraka yao na nguvu zao za utawala na wanakuwa na pupa ya kujinufaisha katika muda mfupi walionao. Hawajifunzi somo lolote kutoka historia ya mataifa.
Kuwa na umma: Lazima ujichunge usijitenge na umma. Usiweke pazia la fahari ya uongo baina yako na wale unaowatawala. Kujidai kama huko na kuonyesha mbwembe na fahari kwa kweli ni kuonyesha hisia za udhalili na majivuno. Matokeo ya mwelekeo kama huo ni kwamba unakuwa huzijui hali za raia wako na matukio halisi yanayotokea katika nchi.
Amani huleta neema: Iwapo adui wako atataka muandikiane mkataba wa amani kamwe usikatae kwa sababu amani itakuondoshea wasiwasi na wahaka na itawapatia watu wako ufanisi na neema.
Imam Ali alimnasihi Malik asiwaruhusu walio woga kuwa washauri wake kwa vile watamtisha asichukue hatua za kijasiri. Kadhalika alimuonya asiwaamini na kuwapa uwaziri wale waliokuwa mawaziri wa watawala wa kimabavu waliomtangulia na walioshiriki katika ukatili wa watawala hao.
No comments:
Post a Comment