Teodoro Nguema Obiang akiwa amesimama mbele ya kasri lake
Toleo la 276
9 Jan 2013
TEODORO Nguema, mtoto wa Rais wa Equatorial Guinea, ana jumba mjini California, Marekani, lenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 30. Pia ana ndege yake binafsi ya aina ya Gulfstream jet na anamiliki aina kwa aina ya magari ya kifahari.
Kadhalika Teodoro ametumia kiasi cha dola milioni moja na laki nane kununua baadhi ya vitu vilivyokuwa vikimilikiwa na mwimbaji Michael Jackson. Unakaa na kujiuliza: amepata wapi fedha za kujinunulia vitu vyote hivyo? Tunajuwa kwamba yeye ni waziri lakini mshahara wake ni dola za Marekani 81,600 kwa mwaka….
Mtoto wa Rais mwingine wa Kiafrika mwenye kuogolea kwenye bahari ya fedha ni Isabel dos Santos, bintiye Rais wa Angola. Isabel (40) ananukia uturi na wakati huohuo ananuka tuhuma za ufisadi. Inakisiwa kuwa ana utajiri wa thamani ya dola za Marekani milioni 500.
Ingawa Isabel ana shahada ya uhandisi kutoka Chuo cha King’s College, London, na alianza kujihusisha na biashara tangu awe na umri wa miaka 24 ni wazi kwamba asingaliweza kuupata utajiri wote alionao sasa lau asingelikuwa binti wa Rais Eduardo dos Santos.
Kama ilivyo Tanzania na baadhi ya vigogo vya CCM, ufisadi nchini Angola umekuwa zaidi ukihusishwa na baadhi ya viongozi wa chama kinachotawala cha MPLA.
Ufisadi ulianza kufurutu ada Angola kama miaka 10 au 15 hivi iliyopita. Umezidi kutia mizizi kwa sababu utawala wa chama cha MPLA unategemea vitendo vya ufisadi ili uweze kuendelea.
Nchini Angola ufisadi umekuwa ukihusishwa sana na biashara ya mafuta yanayochimbwa nchini humo na kuuzwa na serikali. Kwa hakika, kampuni ya taifa ya mafuta, Sonangol, ndiyo moja ya mihimili mikuu ya serikali.
Mara kwa mara, Manuel Vicente, Mkuu wa Sonangol, ambayo ndiyo kampuni kubwa ya umma nchini humo, amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa wa Angola. Wengine wanaotajwa naye ni Jenerali Helder Manuel ‘Kopelipa’ Vieira Dias ambaye ni mshauri wa kijeshi wa Rais pamoja na kuwa waziri na Jenerali Leopoldino Fragoso do Nascimento, mkuu wa idara ya mawasiliano ya Rais.
Watatu hao wanatuhumiwa kujipatia utajiri wenye thamani ya mabilioni ya dola za Marekani kwa njia za kifisadi. Moja ya njia walizotumia ni kuyabinafsisha mashirika ya umma kwa faida yao. Si kwamba mashirika hayo yalikuwa yakila hasara. La.
Katikati ya walaji rushwa na mafisadi wa wanaotuhumiwa Angola ni mwenyewe Rais wa nchi. Kuna wasemao kwamba hana budi kuwako katikati ya duru ya ufisadi kwa vile yeye na chama chake kama nilivyokwishagusia, wanautegemea ufisadi ili kuweza kuendelea kutawala. Wengine wanasema kwa kejeli kwamba nchini Angola ufisadi ni ‘taasisi’ ya aina yake na kwamba hiyo ndiyo taasisi kuu yenye kuiendesha nchi.
Kwa jumla bara letu la Afrika limepata sifa mbaya kwa sababu ya ufisadi uliokithiri na unaowahusisha au kuwagusa baadhi ya viongozi wa nchi zetu. Kelele kubwa zimekuwa zikipigwa ndani na nje ya Afrika dhidi ya ufisadi na hatimaye kuna dalili nzuri kwamba asasi za kiraia, makampuni, taasisi za umma na hata baadhi ya serikali za Kiafrika, zimekuwa zikichukua hatua madhubuti za kupiga vita ufisadi.
Sote tunazijuwa athari za ufisadi kwa maendeleo ya nchi zetu. Tunaelewa jinsi ufisadi unavyochangia kuzifanya nchi zetu ziwe masikini, zikose maendeleo, zikose barabara, zikose maji safi, umeme na hata madeski skulini.
Kuna maswali mengi tunayopasa kujiuliza tunapoutafakari ufisadi. Kwa mfano, nini hasa ufisadi? Nini historia yake, akina nani wanaoathirika nao, nini kinachoupa nguvu na nini kinachouzuia?
Hayo ni baadhi tu ya maswali yanayojadiliwa katika kitabu kipya kuhusu ufisadi duniani. Kitabu hicho (‘Global Corruption: Money, Power and Ethics in the Modern World’) kimeandikwa na Laurence Cockroft, mtu ambaye kwa muda mrefu amekuwa katika safu ya mbele ya wale wenye kupiga vita ufisadi. Kimechapishwa na shirika la uchapishaji la Uingereza la I.B.Tauris.
Cockroft ni mmoja wa waasisi wa ile asasi ya kimataifa ya kupiga vita ufisadi, Transparency International, na kwa muda mwingi alikuwa mwenyekiti wa tawi lake la Uingereza.
Cockroft anaijua vyema Tanzania ambako aliwahi kufanya kazi katika miaka ya 1960 na baadaye amekuwa akishughulika na miradi kadha wa kadha ya maendeleo nchini humo.
Uzuri wa kitabu cha Cockroft ni kwamba kina mada mbalimbali za kuzichambua katika kuangalia nini kinachoupa nguvu ufisadi. Kwa mfano kinauchambua ‘uchumi uliofichika’ — huu ni uchumi usio rasmi ambao takwimu zake hazijulikani na unaorahisisha malipo ya hongo kulipwa bila ya kujulikana.
Kinaangalia pia jinsi fedha ambazo aghalabu hupatikana kwa njia za kifisadi zinavyotumiwa kisiasa. Kwa hili amekitaja chama cha CCM na jinsi baadhi ya viongozi wake walivyojitajirisha kutokana na shughuli za kukipatia fedha chama hicho.
Cockroft amejaribu kuonyesha kwamba ufisadi si ugonjwa wa Afrika pekee, bali ni wa dunia nzima; umeambukiza kwingi na ufisadi wa Afrika uko chanda na pete na ufisadi katika madola makubwa ya Marekani na barani Ulaya.
Ametoa mifano mingi ya ufisadi katika nchi kadha wa kadha zisizo za Kiafrika na za Kiafrika. Tanzania imejaa tele. Mingi ya mifano hiyo tunaijuwa. Lakini kitabu chake kinachemsha bongo si kwa mifano aliyoitoa bali kwa simulizi zake kuhusu jinsi ufisadi unavyofanya kazi katika sehemu mbalimbali duniani na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuuzuia.
Hiki ni kitabu muhimu kwa yeyote yule anayetaka kuelewa jinsi ufisadi unavyokuwa na mitandao yake na jinsi mitandao hivyo inavyowahusisha wengi walio madarakani katika nchi zenye chumi zilizoendelea na pia katika nchi kama zetu ambazo bado zinasotasota zikitafuta maendeleo.
Barani Afrika wako wababe kadhaa wanaoshika panga kupambana na ufisadi. Cockroft amewataja watatu tu walio maarufu sana: Nuhu Ribadu wa Nigeria, John Githong’o wa Kenya na Zitto Kabwe wa Tanzania. Amemsahau mwandishi na mwanaharakati wa Angola Rafael Marques ambaye maisha yake yamo hatarini kwa kazi anayoifanya ya kuufichua ufisadi wa Angola.
2 comments:
Uchambuzi mzuri sana. Wewe kama mswahili na Mtanzania kwanini umeweza kuthubutu kuwataja kwa majina mafisadi wa nchi nyingine lakini hukuweza kumtaja kwa jina fisadi hata mmoja wa Tanzania?.
Naungana na mleta maoni wa kwanza hapo juu. Tuanze na huyu rais wetu. Mtoto wake Ridhiwani ana miliki miradi kibao na ana malori ya mizigo karibia 200 kama siyo zaidi. Je, Ridhiwani hizi hela alizipataje wakati JK alitokea familia ya kimasikini?
Post a Comment