Tuesday, February 5, 2013

Dk. Nchimbi: Watakaoboronga Magereza wawajibike wenyewe

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imewaagiza wakuu wa magereza wa mikoa na watendaji wa jeshi hilo kukubali kuwajibika kwa makosa yatakayojitokeza magerezani badala ya kuacha mzigo huo aubebe Waziri au Kamishna Mkuu wa Magereza.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo kwa maafisa waandamizi  wa Jeshi la Magereza na kusema kamwe hatakubali kuwajibika kwa makosa yatakayojitokeza badala yake wataanza kuwajibishwa kwanza wakuu hao.


Alisema katika ziara ya hivi karibuni kwenye magereza, alibaini dosari kadhaa ambazo kama zitaendelea kujitokeza ni wazi kuna athari zitakazowaathiri wafungwa na mahabusu.
Dk. Nchimbi alisema kuwa kutokana na hali hiyo, ni wajibu kwa wakuu hao kuhakikisha dosari hizo zinaondolewa mapema.

“Mfano, unakuta kamba ishirini ndani ya magereza, kama zisipoondolewa na ukakuta mahabusu au wafungwa ishirini wamekufa, nani atawajibika?” alihoji Dk. Nchimbi na kuongeza:

“Nasema sitakubali kwa hili, tulifanya ziara ya kushtukiza, sasa ni tahadhari kwenu kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake.”

Kwa mujinu wa Dk. Nchimbi, kama taratibu zote za kuendesha magereza zikifuatwa ipasavyo, hakutakuwa na makosa yoyote.

Waziri Nchimbi  alitaka jeshi hilo kushirikiana na jamii mbalimbali ili kuhakikisha maadili yanakuwapo ili kupunguza kasi ya wahalifu ambao wengi wamekuwa wakitaka kupata kipato bila kufanya kazi.

Alisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa kati ya wafungwa 100 wanaofungwa na kutoka magereza, 30 wanarudia makosa na kwa hali hiyo inaonyesha kuwa jeshi hilo limefanikiwa kwa asilimia 70.

Aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha linawapa kazi wafungwa walioko magerezani ambazo  zitawasaidia baada ya kumaliza vifungo badala ya kuwapa kazi za kuwakomoa.

Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja, alisema lengo la kuanzisha dawati la jinsia katika jeshi hilo ni kuimarisha ufanisi katika mahala pa kazi kwa kutambua jinsia katika jeshi hilo.

Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa jinsia, jeshi hilo limeteua maafisa wakuu wa mikoa wanawake wawili na kufikia wanne.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake