Na Flora Mwingia
Mpenzi msomaji, leo tujadili suala moja ambalo nimeona linahitaji mchango na maoni yetu katika kulipatia suluhisho. Tunaliona jambo la kawaida lakini ni aina ya kansa inayozitafuna familia zetu na hivyo kujenga usugu kwa vizazi vijavyo.
Ipo baadhi ya misemo inayolenga makuzi na malezi ya mtoto kwa mfano; “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”, “Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu”, “Mtoto akinyea kiganjani, hukikati, utakinawisha”, “Samaki mkunje angali mbichi… akikauka hakunjiki” na kadhalika.
Misemo hii inatoa changamoto kwa mzazi na hasa mama ambaye muda mwingi anakuwa na mtoto au watoto nyumbani ikilinganishwa na baba ambaye huwa katika mihangaiko kikazi.
Hivi karibuni, wiki mbili zimepita tangu nitoke kijijini ambako nilikwenda kwa mapumziko ya mwaka. Nilipata fursa ya kutembelea ndugu, jamaa na marafiki na kubadilishana mawazo kuhusu maisha ya kila siku.Naam. Nikiwa nyumbani alinijia mwalimu wa shule ya Msingi pale jirani akitaka nianike uozo katika moja ya shule ambayo tatizo la ulawiti kwa wanafunzi wa kiume limeshamiri sana.
Akaniambia kwamba kwa wakati ule aliitwa mmoja wa wazazi wa mtoto anayelawitiwa na wenzake aweze kujieleza mbele ya Afisa elimu kuhusu tuhuma hizo na jinsi anavyolifahamu suala hilo.
Nami nikata nimuone mzazi huyo nizungumze naye. Alipokuja niliongea naye kwa kirefu juu ya tatizo hilo.(Nitalimulika kwa kina katika NIPASHE Jumapili toleo lijalo Feb.17).
Katika mazungumzo yale, mama yule ambaye kijana wake ndiye aliyedaiwa kulawitiwa, alishangaa kukosa ushirikiano toka kwa mama wa mmoja wa vijana waliosadikiwa kuwa na mchezo wa kumlawiti mwanae.
“Nilishangaa sana kwa kutopata ushirikiano…watoto wote wawili, yule wa kwangu na yule mwenzake walipoulizwa walikiri kushiriki tendo lile la ulawiti, lakini mama wa kijana aliyemlawiti wa kwangu akawa akamtetea wa kwake eti hakuhusika…iliniumiza sana, ilibidi niende kuripoti polisi”, alisema mama huyu kwa uchungu mkubwa.
“Tena cha ajabu zaidi, kwa aibu baada ya mwanawe kukiri, alimhamisha kwenda kusikojulikana ili asionekane pale kijijini. Mimi nilisema kama wamehusika wote na wamekubali mbele ya wazazi, waadhibiwe bila upendeleo ila mama wa kijana aliyekuwa akimuumiza yule wa kwangu akamtetea eti hakuhusika…mbona wote walikiri?”.
Mpenzi msomaji, hiyo ni sehemu tu ya uhondo wa kisa kizima nitakachokusimulia NIPASHE Jumapili ya Feb 17, usikose nakala yako.
Nilitanguliza swali katika kichwa kilichobeba makala hii kwamba “kwanini mama humtetea mwanae hata kwa kosa baya? Tayari msomaji wangu umeona simulizi hiyo fupi hapo juu jinsi mama yule alivyosimama kidete kumtetea mwanae eti hakutenda kosa wakati mtoto mwenyewe anakiri.
Hili ni tatizo, wapo wazazi wagumu katika kuamua matatizo au makosa waliyofanya watoto wao. Mzazi unatakiwa kuwa msuluhishi na siyo mchechezi. Mzazi unatakiwa kutenda haki katika kupatia ufumbuzi jambu fulani na siyo kutetea maasi, makosa yaliyo dhahiri.
Wakati mwingine jambo dogo laweza kuwa kubwa kutokana tu na busara kutozingatiwa. Mzazi anajua kabisa kosa hili amelifanya kweli mwanae lakini atamtetea kwa nguvu zake zote. Hivi ni kwanini?
Nilidhani kwa suala kama hilo nililozungumzia hapo juu kuhusu mama kumtetea mwanae anayedaiwa kumlawiti mwenzake, baada ya watoto wenyewe kukiri kwamba walishiriki tendo lile, wazazi wale wangeitisha kikao kwa kuwashirikisha uongozi wa kijiji, polisi na Afisa Elimu, kisha kuwaonya na kuwaelimisha athari zake.
Na baada ya hapo uwepo ufuatiliaji wa karibu wa nyendo za watoto hao kuona kama wamejirekebisha au la. Hakuna sababu ya wazazi kukwepa jukumu la kupatia ufumbuzi matatizo ya watoto wao na badala yake kujengeana uhasama.
Kwa mujibu wa mama aliyelalamika mwanae kulawitiwa, mzazi(mama) wa kijana anayelalamikiwa alionyesha kujenga chuki eti familia yake imedhalilishwa. Je, mama huyu anayo machungu ya dhati dhidi ya mwanae na watoto wa wanawake wenzie? Je, anajua wajibu wake katika kulea, kulinda na kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto wa taifa hili?
Serikali imeweka kipaumbele kuhusu ustawi wa watoto wetu. Na ndiyo maana kwa makusudi ikaunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ambayo imepewa pamoja na mambo mengine jukumu la kuandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania mwaka 1996 ikiwa ni hatua muhimu ya kuwapatia watoto haki zao.
Katika kitabu cha sera hiyo toleo la pili la mwaka 2008, wajibu wa wadau umeainishwa vema ukurasa wa 40. Kifungu cha 68 kuhusu wajibu wa familia na jamii, imeelezwa bayana kwamba zina wajibu wa kuleta mabadiliko ya tabia, mila na desturi.
Kwa mantiki hiyo, zitahusika kikamilifu katika kutekeleza masuala ya uhai, ulinzi na maendeleo ya mtoto kwa kuimarisha mila na desturi; kushiriki katika malezi ya pamoja ambayo yanazingatia upendo na dhana ya kuwa mtoto wa mwenzio ni wako, pamoja na kutoa huduma kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Kadhalika wazazi, walezi wanao wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya matukio ya hatari kama vile ajali barabarani, ubakaji, unyanyasaji, utelekezaji, utoroshaji, uuzaji wa watoto na utupaji wa watoto.
Mpenzi msomaji, huo ndio muongozo wa familia na jamii kuhusu malezi ya watoto wetu. Je, wazazi wanazingatia hayo? Hao wanaotetea watoto wanaotenda makosa ya dhahiri badala ya kuwarekebisha wanawatendea haki?
Mimi naishia hapa msomaji wangu nikuachie nawe kama unayo maoni uchangie tuelimishane. Na ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.
Wasalaam.
2 comments:
Hilo ni tatizo kubwa sana hasa wazazi wa siku hizi, ingawa na wale wazee wa zamani wameanza kuwaiga wazazi wa kizazi hiki hasa pale mtoto anapokuwa na uwezo kidogo hata akifanya kosa anatetewa, kwa kweli inabidi tujirekebishe hiyo tabia ya kulawiti haifai kabisa na tusifikiri kwa kuwatetea watoto kwa hiyo tabia ni kuwapenda bali ni kuwatia katika dhambi kubwa sana na hukumu yake ni mbaya sana kwa Mungu .
Raha ya milele uumpe ee bwana na mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani, amina
Post a Comment