Saturday, February 2, 2013

Majambazi yamvamia Mchina yakitaka kumpora

Na Roman Mallya.
Watuhumiwa wa ujambazi waliokusudia kupora fedha kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni moja wamezua taharuki kwenye kituo cha mabasi Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kurusha risasi za moto zilizosababisha watu kukimbia ovyo kunusuru maisha yao.

Wezi hao waliokuwa na pikipiki juzi saa 3:00 usiku walivamia gari la Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hunting International, raia wa China Jung Won Jyo (44) kwa lengo la kumwibia fedha.

Baadhi ya abiria walikuwa na wakati mgumu kwa vile baadhi walikoswa koswa na magari wakati huo wakikimbia kujiokoa huko magari nayo yakikimbia kuondoka eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa mkasa huo aliosema ulihusisha watuhumiwa watatu waliokuwa kwenye pikipiki hadi jana walikuwa hawajakamatwa.

Alieleza kuwa walipofika kituoni hapo walilifuata moja kwa moja gari namba T 198 BRE aina ya Toyota Hiace lililokuwa limembeba Mkurugenzi Jyo likiendeshwa na Mohamed Seleman.
Alisema ndani ya gari hilo kulikuwa na mizigo ambayo majambazi hao walidhani ni fedha.
Kamanda alisema baada ya mkurugenzi huyo kufikishwa kituoni akitokea kazini kwake Sinza Makaburini, watuhumiwa hao walianza kufyatua risasi zilizosababisha tafrani kwa watu waliokuwa kituoni hapo.

Alisema pia walitumia jiwe kuvunja kioo cha mbele cha gari hilo kwa lengo la kuiba mali zilizokuwamo. "Licha ya kutumia silaha za moto lakini watuhumiwa hawa waliambulia simu mbili aina ya Samsung… hatukupata namba ya pikipiki, ila polisi wangu walifika eneo la tukio" alisema na kuongeza:

"Eneo la tukio tumeokota risasi na ganda la risasi iliyotumika ninachosema ni kwamba wananchi watambue kuwa wizi wa kutumia pikipiki upo hivyo wachukue tahadhari kwa kutoa taarifa mapema …," alisema na kuongeza kuwa hakuna aliyejeruhiwa
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake