ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 27, 2013

Mali za mfanyabiashara aliyekamatwa kwa tuhuma za ujambazi zakamatwa


Sakata la Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kunasa watuhumiwa wa mtandao wa majambazi jana lilisababisha kundi la wakazi wa Jiji la Mbeya kujikusanya eneo Mwanjelwa katika maeneo ya maduka ya nguo, ili kumwona mfanyabiashara maarufu wa eneo hilo, Ghati Mbilinyi (32), aliyekamatwa na Polisi akihusishwa na mtandao huo.
 
Umati huo ulijitokeza baada ya Polisi kuongozana na mfanyabiashara huyo kwenda dukani kwake kwa ajili ya kufanya upekuzi na kuchukua baadhi ya mali zinazodaiwa kuwa ni za wizi kama kielelezo wakati atakapofikishwa mahakamani.
 
Mbilinyi akiwa chini ya ulinzi mkali, aliamuliwa kukusanya bidhaa karibu zote zilizokuwa ndani ya duka lake na kuzipakia katika gari la Polisi kisha kuondoka nazo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema kuwa walilazimika kwenda dukani kwa mtuhumiwa huyo na kuchukua mali zake kutokana na maelezo yake baada ya kukiri kuwa anajihusisha na matukio ya kupora mali na kufanya mauaji.
 
“Ni kweli kwamba tumelazimika kwenda na mtuhumiwa mwenyewe hadi dukani kwake na kuchukua mali alizokuwa nazo, tumefanya hivyo kutokana na mazingira yanayoonekana kuwa alikuwa anajihusisha na matukio ya ujambazi ya uporaji, utekaji, na mauaji,” alisema Kamanda Diwani.
 
Hata hivyo alisema kuwa Jeshi la Polisi halisemi moja kwa moja kuwa mali zote alizokuwa nazo ndani ya duka zilitokana na uporaji, lakini mtuhumiwa mwenyewe alitaja baadhi ya mali alizozipata kwa kufanya uhalifu.
 
Akizungumzia hatma ya watuhumiwa 13 wanaoshikiliwa na Polisi kwa kujihusisha na mtandao huo, Diwani alisema tayari watuhumiwa saba wamesafirishwa kwenda mkoani Iringa ambako ndiko watashtakiwa kwa tuhuma za kuteka na hatimaye kuwaua wamiliki wa gari lililokuwa likisafirisha mali za wafanyabiashara wa Mbeya.
 
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wengine sita waliobakia mkoani hapa.
 
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya juzi lilitangaza kunasa mtandao watuhumiwa wa ujambazi uliokuwa ukifanya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, ambao uliwahusisha askari mmoja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mmoja wa Kikosi Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Mbeya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: