Monday, February 4, 2013

MIAKA 36 YA CCM: JK aomba umoja


Rais Jakaya Kikwete, awawataka viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujenga umoja na mshikamano huku akisema kuwa anataka kukiacha chama hicho kikiwa imara na nchi yenye maendeleo.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana mjini Kigoma alipokuwa akihutubia maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma, kauli yake mbiu ilikuwa ni ‘Umoja ni Ushindi’.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisisitiza umoja na mshikamano ndani ya CCM ili kukijenga chama hicho sambamba na utekelezaji wa ahadi walizowaahidi wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.Alisema ni jambo la kushangaza kuona ndani ya chama hicho baadhi ya viongozi na wanachama hawasalimiani na wengine hawazungumzi pamoja, hali ambayo alisema ni hatari katika kukiendeleza chama.

Alisema mpaka sasa chama kimepoteza majimbo matano, ambayo hata hivyo, hakuyataja kwa sababu ya mifarakano na kutoelewana miongoni mwa wanachama na viongozi.

Rais Kikwete pia alikitahadharisha Chama kuwa na wanachama wenye imani nusu nusu kwa kusema kuwa kwa kufanya hivyo watahatarisha uhai wa Chama, hivyo aliwasihi viongozi kuwa makini na wanachama wa namna hiyo.

Alisema katika kipindi chake cha uongozi, dhamira kubwa aliyonayo ni kuiacha nchi katika hali ya maendeleo na amani iliyokuwapo kwa miaka takribani 50 tangu utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema mpaka sasa CCM ina wanachama wapatao milioni 6.4 idadi ambayo alisema ni ndogo katika kujihakikishia ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015, hivyo alikitaka chama kuongeza idadi ya wanachama na kufikia milioni nane hadi 10.

Alisema tangu nchi ipate uhuru, kuna mafanikio mengi yaliyopatikana na kuletwa na CCM ikiwamo ujenzi wa barabara mkoani Kigoma, ujenzi na uboreshwaji wa njia ya reli, sekta ya elimu na afya.

Aidha, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa siasa nchini kuacha kushabikia chuki zinazoleta hatari ya umwagaji damu na ukosefu wa amani bali wajenge sera za kuimarisha utulivu wa nchi na siyo kukumbatia siasa za kuangamiza jamii yote.

Pia alisema siasa za mifarakano zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, siyo nzuri badala yake wajenge amani iliyotawala nchini na kulipa sifa taifa.

“Viongozi wenzangu wa siasa, tuijenge amani yetu, kama kiongozi anaona ni sifa kutangaza kwa umma ‘lazima damu itamwagika’ kwanini usitumie kisu kukata ngozi yako kama unaona rahisi kusema damu itamwagika badala ya kuwatanguliza watoto wa wenzako wasio kuwa na hatia na kuwaangamiza huku wewe ukiwa umetulia, tuache uchochezi wa kuvuruga amani tafadhali,” alisema na kuongeza:

“Nawasihi wanachama na wananchi wenzangu msikubali kutumiwa na viongozi wasiokuwa na uchungu, watatuangamiza Watanzania tusiokuwa na hatia, tujivunie na kuimarisha usalama na amani ya nchi yetu, pia tuendelee kujenga chama chetu kwa faida ya taifa zima.”

Mbali na chuki za kisiasa, Rais alizungumzia migogoro ya kidini inayohatarisha usalama wa nchi na wananchi wote huku akiwataka wazee kukutana na viongozi wa dini zote ili kila kiongozi afanye mazungumzo na waumini wake.

“Viongozi wa dini zote wa Kiislamu na wa Kikristo, wakizungumza na waumini wao, lazima amani itapatikana. Hakuna mshindi, wote tutakuwa tumeshinda na hivyo utulivu utachukua nafasi yake katika nchi yetu,” alisema na kuongeza:

“Nilizungumzia na ninarudia tena kwamba kama viongozi wa Kiislamu na wa Kikristo watarudisha utaratibu wa kuongea na waumini kila mmoja akizungumzia upande wake tutashinda tu.”


Waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana; Naibu Katibu Mkuu CCM bara, Mwigulu Nchemba; Katibu wa Uhusiano wa Kimataifa Dk. Asha-Rose Migiro na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Wengine ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye; Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa, Sadifa Juma Khamis; Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wabunge, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), wenyeviti wa mikoa na wawakilishi wa vyama rafiki.

Naye Waziri Mwakyembe alisema kwa sasa serikali inapambana na tatizo la urushwaji wa tiketi katika stesheni kuu ya Mkoa wa Kigoma.

Alisema kwa jana alisimamia uuzwaji wa tiketi 700 na kubakiza tiketi 200, na kusema kuwa endapo tatizo hilo likijitokeza tena, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watendaji wakuu wa stesheni hiyo ikiwamo kuwafukuza kazi.

Alisema mpaka sasa serikali imefanikiwa kurejesha huduma ya usafiri wa treni iliyosimama kwa muda mrefu.

Alisema ifikapo Juni mwaka huu, usafiri wa ndege kwa wakazi wa Kigoma utakuwapo na utafanywa na shirika la Precision na Air Tanzania kwa gharama nafuu.

VURUGU ZAIBUKA DODOMA
Vurugu kubwa zilizotokea jana katika mkutano wa CCM mjini Dodoma wa maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Vurugu hizo zilitokea katika mkutano huo uliofanyika kwenye kiwanja kilichopo karibu na baa inayojukana kama Mwanga na watu takribani sita wanadaiwa kujeruhiwa kwa mawe.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Saad Kusilawe, vurugu hizo zilitokea jana asubuhi katika viwanja hivyo.

Alisema wakati Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, akihutubia katika mkutano huo, walitokea wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakitaka kuondoa bendera iliyokuwa imesimikwa kiwanjani hapo.

“Tuliwaeleza kuwa wasubiri tumalize mkutano wetu na kisha watasimika bendera yao, lakini walikataa na ndipo kukatokea kutoelewana,” alisema.

Alisema vurugu hizo zilitulizwa na Polisi waliokuwa wakilinda mkutano huo na baadaye waliendelea kuhutubia mkutano huo ambao ulitanguliwa na maandamano ya mshikamano.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Dodoma, Stephen Massawe, alisema eneo walilohutubia CCM lilikuwa ni tawi lao la siku nyingi.

“Wanachama wa CCM walikuja na kushusha bendera yetu katika tawi letu, tulipohoji walianza kutupiga kwa mawe,” alisema Massawe.

Alisema eneo hilo linalotumika kuegesha teksi ni kijiwe cha Chadema na mara zote bendera ya chama hicho huonekana ikiwa imesimikwa.

Alidai kuwa wanachama wanne wa chama chake walijeruhiwa kwa mawe na kuwa kada mmoja alishonwa nyuzi saba katika zahanati binafsi ya Upendo iliyopo katikati ya mji baada ya kupigwa mawe.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema juzi CCM walikwenda kuwaomba Chadema washushe bendera yao katika eneo hilo ili walitumie kufanya mkutano wa jana.

Hata hivyo, Chadema walikataa kufanya hivyo, hali iliyowafanya viongozi wa CCM kushusha bendera hiyo juzi usiku na jana kusimika za kwao.

Walisema wakati wakiwa katika mkutano huo, walijitokeza wanachama wa Chadema wakiwa wameshika bendera nyingine ya chama chao na kukaa pembeni katika eneo la mkutano.

Walisema baada ya viongozi wa CCM kubaini kuwa karibu na mkutano huo kulikuwa na wanachama wa Chadema, waliwataka kuondoka eneo hilo kwa kuwa si mkutano wao.

Lakini wakati CCM ikisisitiza waondoke katika eneo hilo, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, aliwataka wanachama wenzake kuwaacha wanachama hao ili wasikilize sera za CCM.

Mmoja wa mashuhuda hao, alisema kuwa baada ya muda kidogo wanachama hao walivamia mkutano huo na kutaka kusimika bendera yao na ndipo vurugu zilijitokeza na watu kuanza kurusha mawe hovyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema vijana wake (polisi), bado wanakusanya taarifa za tukio hilo ili kufahamu chanzo, watu wangapi walijeruhiwa na waliokamatwa.

“Ndiyo vijana wako mitaani huko wanakusanya taarifa ili tujue chanzo na mambo mengine,” alisema Kamanda Misime.

Hata hivyo, kwa mujibu wa habari kutoka katika eneo hilo, wanachama wawili wa Chadema wanadaiwa kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu katika mkutano huo.

Imeandikwa na Hellen Mwango, Gwamaka Alipipi, Dar, Sharon Sauwa, Dodoma na Jacton Ngelly, Kigoma.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake