Sunday, February 3, 2013
Poulsen asihadae Watanzania- Nipashe
Kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja orodha ya wachezaji 21 watakaokuwa katika nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki Jumatano dhidi ya Cameroon ambayo ni moja ya mataifa yanayoheshimika katika soka, si tu ya Afrika, duniani kwa ujumla.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza na Cameroon Dar es Salaam huku ikiwa imetoka kushinda 1-0 na kupoteza moja kati ya michezo yake miwili ya kujipima nguvu iliyopita dhidi ya timu za Zambia B na Ethiopia zilizoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Lakini cha kukumbukwa zaidi, na ingawa kimsingi ilikuwa ni timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars, vijana wa Poulsen wametoka kukosa japo nafasi ya tatu kwenye Kombe la Chalenji la mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, nchini Uganda, mwishoni tu mwa mwaka jana.
Pamoja na matokeo ya Taifa Stars kuonyesha kuwa ni timu ambayo, tunaona Nipashe, ipo katika hatua ya ujenzi na si ushindani dhidi ya timu kabambe za Afrika, Poulsen alidai juzi kuwa haoni sababu za kikosi chake kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2015.
Na kinachompa kujiamini huko?
Ni matokeo hayo dhidi ya Zamabia na Ethiopia, eti, ambayo sisi Nipashe, tunaona, kocha huyo aliyachagua ili kuwasahaulisha Watanzania kuwa alishindwa japo kuifunga Zanzibar iliyojaa wakali ambao kwake hawana uwezo kuwa kuitwa Taifa Stars akiwa na sehemu kubwa ya wachezaji 21 aliowaita kuikabili Cameroon.
Ahadi hii, kuwa Tanzania itafuzu kucheza fainali za AFCON za 2015 haitushangazi Nipashe, hatahivyo.
Haitushangazi Nipashe kwa sababu imekuwa ni kawaida ya makocha wa Taifa Stars kuwapa Watanzania ahadi zilizojaa matumaini lakini wakarudi kuwataka kuwa wavumilivu, bila hata kuomba radhi, pale timu hiyo inapoendeleza kawaida yake ya kuwa msindikizaji katika kila michuano ya awali, baada ya michuano mingine ya awali.
Tunakumbuka, Nipashe, kwamba palikuwa na ahadi ya kurudi na Kombe la Chalenji na hata wakati timu ikienda kucheza mchezo wa kirafiki nchini Ethiopia, mashabiki wa Taifa Stars walijazwa matumaini ya matokeo mazuri kama ya mechi dhidi ya Zamabia B.
Lakini matokeo mazuri yatakuja vipi wakati, kwanza tu, lugha ya mawasiliano ya mwalimu ni tofauti na ya wachezaji?
Imewahi kuthibitisha katika ngazi ya juu kabisa ya mashindano ya soka -- Kombe la Dunia la FIFA -- kwamba ni vigumu kwa timu kupata mafanikio pale ambapo lugha ya kufundishia mazoezini ni tofauti na pia si fasaha kama lugha ya kwanza ya wachezaji.
Na ndiyo maana hata katika ngazi ya klabu, kwa mfano, kwa wenzetu ambao masuala ya ufundi yamewekewa mkazo zaidi kuliko ahadi hewa za nyakati za maandalizi, walimu na wachezaji wa kigeni hulazimika kujifunza kwanza lugha ya nyumbani ya timu husika na wakaifahamu.
Kiingereza, kwa mfano, kinachotumiwa na Poulsen, ni lugha ya kimataifa lakini je, ni asilimia ngapi ya wachezaji 21 walioitwa kujiunga na kambi ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Cameroon, kwa mfano, wanaijua kwa ufasaha?
Hivyo tuna uhakika Nipashe kuwa mapokeo ya maelekezo kwa wachezaji wakati wa mazoezi uwanjani si kamilifu hata kama yatakuwa yakitafsiriwa kwao na mwalimu msaidizi kwa sababu ripoti ya maagizo siku zote hupoteza asilimia fulani ya usahihi wake.
Hivyo badala ya kocha kuahidi mafanikio ya miaka 33 iliyopita ambayo kama angefanya utafiti angegundua kuwa yalitokana na kocha mzalendo aliyekuwa akitumia Kiswahili kazini, mwalimu huyo ambaye ana zaidi ya miaka miwili nchini angejikita katika kujifunza lugha ya taifa kwanza ili kuwa na uhakika kuwa mafunzo yake hayo yanapokewa kwa utimilifu.
Badala ya kuahidi kwamba Taifa Stars itakwenda AFCON 2015 ni vizuri mwalimu akaahidi kwamba kuanzia sasa ataweka mkazo, kwanza, katika kujifunza lugha yetu.
Badala ya kuahidi kwamba Taifa Stars itakwenda AFCON 2015 ni vizuri mwalimu akaahidi pia kuanza kufuatilia mechi nyingi zaidi za ligi kuu ya Bara, kufika mara kwa mara kwenye viwanja vya ligi kuu ya Zanzibar na ikiwezekana baadhi ya mashindano ya ndondo kwa ajili ya kutafuta wachezaji wenye vipaji.
Tuna hakika, Nipashe, Taifa Stars, haitakwenda fainali nyingine za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kujaza wachezaji wa Simba na Yanga kwenye kikosi.
Na wala Stars haitakwenda fainali nyingine za Kombe la Mataifa ya Afrika bila kwanza kutiliwa mkazo zaidi, na hatimaye kuvuna matunda yatokanayo na uwekezaji katika soka la vijana wa ngazi zote.
Hivyo Poulsen asihadae Watanzania kwamba Taifa Stars itakuwa Morocco baada ya miaka miwili ijayo kwa sababu, tunajua, tutashika vichwa tena wakati ratiba ya michuano ya awali itakapopangwa Juni 4, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake