Thursday, February 21, 2013

Tunasisitiza: Waziri Kawambwa ajiuzulu sasa

Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa 

LEO ni siku ya tatu tangu kutangazwa kwa matokeo ya kutisha na kuhuzunisha ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana. Kutangazwa kwa matokeo hayo ya aibu na ya kufadhaisha yameliacha taifa letu katika mkanganyiko mkubwa, huku wananchi wengi wakiyaona matokeo hayo kama janga la kitaifa.

Hivi sasa kila kona ya nchi ni vilio na huzuni kubwa. Lawama, ghadhabu na hasira za wananchi zinaelekezwa serikalini, huku wadau wengi wa sekta ya elimu wakikitaka kichwa cha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwa gharama yoyote.Hakika hayo ni matokeo ambayo yamemgusa kila mwananchi.
Matokeo hayo ya ajabu, kama takwimu za watahiniwa walioshinda na walioshindwa zinavyoonyesha, yameifanya nchi yetu kuwa kituko na kichekesho mbele ya jumuiya ya kimataifa. Tunawezaje tena kusimama kifua mbele kama moja ya mataifa yenye kutolewa mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki au Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye mfumo wa elimu wenye dira na mwelekeo?

Kwamba watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata daraja sifuri na watahiniwa 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne ni jambo lisiloingia akilini kama ambavyo halikubaliki. Kama tulivyosema jana kupitia safu hii, hili hakika ni anguko la kihistoria na ni kashfa kubwa iliyoiacha nchi yetu katika aibu na fedheha ya namna ya pekee. Hii ni sawa na kufikisha ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa kwamba mfumo wa elimu yetu haufai na kwamba shule zetu sasa ni vinu na mitambo ya kuzalisha ujinga.

Maana yake ni kwamba viongozi wametutengenezea mazingira ya kutoweza kushindana katika soko la ajira siyo tu hapa nchini, bali pia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kwingineko. Tujitayarishe kupokea wageni kuchukua nafasi za ajira hapa nchini, ambapo watoto wetu wanaohitimu masomo watakuwa wakiajiriwa tu kama manamba ambayo ni aina fulani ya utumwa.

Ndiyo maana tunasisitiza kwamba Waziri Kawambwa lazima ajiuzulu na kwamba afanye hivyo sasa, siyo kesho. Kama tulivyosema jana, waziri huyo ameonyesha udhaifu mkubwa katika kuisimamia wizara hiyo na tunaweza kusema bila woga kwamba amesimamia kuporomoka kwa viwango vya elimu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuchukua hatua ili mfumo wa elimu usivurugike na kufikia kiwango cha kutisha tunachokishuhudia sasa.

Tunashangazwa na ukimya wake kuhusu suala la kuwajibika kuhusu hali hiyo iliyotokana na uzembe wa kiutendaji katika sekta anayoiongoza. Badala ya kuwajibika kwa kujiuzulu bila shuruti, anaiweka mamlaka iliyomteua katika hali ngumu pasipo kutilia maanani ukweli kuwa, aibu na fedheha aliyoiletea nchi yetu haviwezi kuvumiliwa na mamlaka yoyote iliyo makini.

Tunaambiwa sasa kwamba juhudi za chinichini zinafanyika ili kuhamishia aibu hiyo kwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta). Hata hivyo, juhudi hizo haziwezi kushinda kutokana na rekodi ya uadilifu na uchapakazi uliotukuka wa Katibu Mtendaji, Dk Joyce Ndalichako. Ni siri iliyo wazi kwamba kiongozi huyo alikuta baraza hilo likiwa katika uozo mkubwa, ikiwamo kuuza na kuvujisha mitihani kwa kiwango cha kutisha mwaka hadi mwaka.

Wengi sasa wanaamini kwamba uimara wa Necta ndiyo umefichua uozo na mapungufu yaliyojitokeza katika wizara anayoiongoza Waziri Kawambwa. Msimamo wake siyo tu umewazuia wanasiasa kukivuruga chombo hicho, bali pia umekisaidia kusimamia viwango pasipo kuyumba, tofauti na zamani ambapo matokeo ya mtihani yaliyotangazwa mwanzoni mwa wiki yangechakachuliwa kwa shinikizo la wanasiasa.
Mwananchi

No comments: