BAADHI ya wasomi nchini wameuponda utafiti uliofanywa na Shirika la Synovate huku miongoni mwao wakienda mbali zaidi kwa kusema: “Ulikuwa na ajenda ya siri.”
Utafiti huo pia umepondwa na wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amesema haziamini tafiti zinazotolewa na Syonovate akidai hazina ukweli wowote.
Licha ya matokeo ya utafiti huo wa Desemba mwaka jana kuonyesha kushuka kwa asilimia 25 kwa umaarufu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa pamoja na chama chake, lakini unaweka wazi kwamba kiongozi huyu angechaguliwa kuwa Rais kama uchaguzi huo ungefanyika sasa.
Dk Slaa anaongoza kwa asilimia 17, akifuatiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Katika maoni yao, baadhi ya wasomi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini walieleza wasiwasi wao kuhusu usahihi wa matokeo hayo na kuhoji mbinu zilizotumika wakisema inawezekana hazikuwa sahihi.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo ameuponda akisema haukufuata misingi ya sayansi ya siasa.
Dk Makulilo alisema alifanya utafiti kwa kampuni zinazofanya tafiti kama hizo kati ya mwaka 2010 hadi 2011 na kugundua udhaifu mkubwa katika kampuni hizo.
“Kwanza wanakosea, kwa mfano wanaposema kuwa utafiti huu ni mwendelezo wa ule uliofanyika Desemba 5 hadi 18, 2011. Ukichunguza utakuta data hizo hazipo. Zilizopo ni za Mei 2 hadi 19, 2011.”
“Kwa kawaida uelewa wa wananchi wa vijijini ni mdogo ukilinganisha na mijini kwa sababu mijini kuna vyombo vya habari. Kwa mfano, ukiangalia swali la nani anafaa kuwa Rais, mwaka 2011 walisema Dk Wilbrod Slaa alikuwa na asilimia 42, lakini sasa ana asilimia 17.
Vijijini wengi bado wanaikubali CCM kutokana na uelewa mdogo, iweje Dk Slaa ambaye chama chake hakina wafuasi wengi vijijini ashinde?” alihoji.
“Utafiti wa Synovate una dosari kubwa kisayansi, hauonyeshi tarehe wala wapi umefanyika. Waliohojiwa wameonyeshwa umri wao, lakini hawaelezwi maoni yao kulingana na umri, jinsia, wanatoka vijijini na mijini. Nilipofanya utafiti wangu niliwafuata wakakimbia…” alisema Dk Makulilo.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Gaudence Mpangala alisema nyakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu, tafiti nyingi hufanyika zikiwa na malengo ya kubeba watu au chama fulani.
Hata hivyo, alisema kilichofanywa na Synovate ni utafiti hivyo kwa kuwa yeye hajafanya utafiti ni vigumu kuupinga moja kwa moja... “Ila kwa mtizamo wa kawaida unatia shaka.”
Alisema kitendo cha utafiti huo kuonyesha kuwa CCM inakubalika zaidi kuliko Chadema kwa sababu kwa siku za karibuni chama hicho kimekuwa kikizungumzia zaidi mambo ya kitaifa, pia kunampa shaka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk Clavery Tungaraza alisema tafiti zinazofanywa na Synovate ni mara nyingi matokeo yake huwa hayaakisi uhalisia wa maisha.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk Clavery Tungaraza alisema tafiti zinazofanywa na Synovate ni mara nyingi matokeo yake huwa hayaakisi uhalisia wa maisha.
Dk Tungaraza alisema utafiti wa Sayansi ya Jamii ndiyo wenye kuaminika zaidi kutokana na kutobadilikabadilika tofauti na tafiti za Synovate ambazo hutegemea mtu aliyehojiwa yuko katika hali gani kwa wakati huo.
Msomi huyo alieleza kushangazwa na tafiti za taasisi hiyo ambazo alidai kuwa mara nyingi hufanywa wakati nchi inapojiandaa kuingia kwenye uchaguzi akisema ingekuwa ni uungwana kama zingekuwa zinafanywa kila mwaka ili kujiridhisha na uhalali wa matokeo yake.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Baraka Nafari alisema ana shaka na utafiti huo na kudai kwamba inawezekana umefanywa kwa lengo la kumsafisha mtu fulani.
Alisema kwa kawaida matokeo ya utafiti uliofuata kanuni na taratibu zote, unatakiwa mwingine akiufanya mara 100, apate majibu kama yale ya utafiti wa awali mara 95.
“Hiyo inaitwa confidence level, (namna ya kujiaminisha, kuwa na imani na majibu). Kwa mfano, wanasema Watanzania hawaoni kuwa rushwa ni tatizo, wakati ukweli kwetu sisi rushwa ni janga, kuna shirika moja la kimataifa lilitaja nchi zenye rushwa Tanzania ikawa kwenye nafasi za juu sana,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema utafiti huo unaonekana kama chumba maalumu cha kuwasafisha baadhi ya watu na vyama vyao badala ya kusimamia kwenye ukweli... “Nautilia shaka kama uliandikwa kwa kuzingatia vigezo na siyo kwa lengo mahususi.”
Mhadhiri wa Chuo cha Mipango Dodoma, Dk Mark Msaki alisema kinachomtatiza ni kutoainishwa njia zilizotumika katika kufanya utafiti huo.
“Sikatai wala kukubali utafiti huu, lakini kwa kuwa ni jukumu la taasisi hizo kufanya tafiti nchini, zitekeleze hayo kwa kuzingatia haki kwa Watanzania wote na si vinginevyo,” alisema.
Dk Msaki pia alisema haridhishwi na taasisi za kisayansi kujikita katika kutafiti nani ana nafasi gani katika kupata urais wa Tanzania, huku nchi ikikabiliwa na changamoto nyingi zinazogusa moja kwa moja maendeleo ya jamii.
Alisema anaamini kuwa kitendo cha taasisi hizo kuibuka na tafiti zinazohusu urais, huku Uchaguzi Mkuu ukiwa bado takriban miaka miwili, ni ishara taasisi hizo kuhusika moja kwa moja katika kugeuza siasa ya Tanzania mchezo wa mpira wa miguu.
Wanasiasa wang’aka
Profesa Lipumba alisema: “Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Synovate walitoa utafiti ulioonyesha kwamba asilimia 94 ya Watanzania wako tayari kupiga kura lakini baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitoa takwimu zake zilizoonyesha kuwa waliopiga kura walikuwa asilimia 42 tu.”
“Inawezekana hata hao waliotoa utafiti huo wakawa wanamtengenezea mtu fulani njia tu kwa mtindo wa kumpigia debe, binafsi siwaamini hasa baada ya makosa yale ya mwaka 2010.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema matokeo ya utafiti huo yanaacha maswali kwani hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu methodolojia na sampuli iliyotumika.
Alisema matokeo ya utafiti huo yanakinzana na ripoti nyingine za mwaka wa 2012 hasa ule wa Economic Intelligence Unit ambao unaonyesha kuwa Chadema kinazidi kupanda.
Alisema matokeo ya utafiti huo yanakinzana na ripoti nyingine za mwaka wa 2012 hasa ule wa Economic Intelligence Unit ambao unaonyesha kuwa Chadema kinazidi kupanda.
Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Sam Ruhuza alisema kati ya vinara tisa wa urais waliotajwa, hakuna hata mmoja anayeweza kuwa Rais wa Tanzania na kuongeza kuwa ushahidi wa hilo ni huko kupanda na kushuka kwa umaarufu wao kisiasa.
“Huko kushuka na kupanda, ni ishara kuwa hakuna Rais kati ya hao, haiwezekani mtu anayependwa na kuungwa mkono aporomoke kutoka asilimia 42 mpaka 17 na huu ni mwaka mmoja tu. Ikipita miaka miwili si wengine watabaki na asilimia moja au sifuri?”
Imeandikwa na Fredy Azzah, Elias Msuya, Editha Majura, Fidelis Butahe, Joyce Mmasi, Dar na Veanance George, Morogoro.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment