Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Ndg. Edward Lowassa
Toleo la 279
30 Jan 2013
MASWALI mengi yalikimbizana mbio akilini mwangu — ukidhani yakicheza foliti — niliposikia kuwa mheshimiwa Edward Lowassa, aliyewahi kuwa waziri mkuu, anataka katiba mpya ifafanue rushwa ni nini katika chaguzi…
Swali la kwanza lililonijia ni: Hivyo kweli mwanasiasa huyu ambaye si mwanasiasa mbumbumbu bali ni mjuzi wa mambo anaitaka katiba imwambie rushwa ni nini katika chaguzi? Upeo wake wa kupima mambo umehamia wapi? Au anatusanifu na kulicheza shere taifa?
Si ni Lowassa huyuhuyu niliyemsikia akiita rushwa kuwa ni sawa na ‘kansa’ alipohojiwa mwishoni mwa 2012 na Radio moja ya kimataifa?
Mheshimiwa huyo alipendekeza katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni.
Gazeti moja lilimnukuu Lowassa akisema: “Katiba mpya iainishe ni matumizi gani ya lazima ambayo mgombea hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake, mfano kuwakusanya watu kwenda kupiga kura nani azibebe gharama hizo.”
Nimekuwa nikikuna kichwa na kujiuliza kwa nini mgombea uchaguzi awakusanye watu kwenda kupiga kura? Kwa nini alazimike kutumia fedha zake mwenyewe katika kampeni? Kwa nini awe yeye na si chama chake kinachogharamia kampeni kwa mujibu wa sheria ya nchi.
Lowassa aliongeza kwamba ufafanuzi huo utaondoa kikwazo kwa watu wenye fedha ambao hivi sasa wanawania uongozi.
Hakujitaja yeye binafsi lakini kwa matamshi hayo ya “watu wenye fedha ambao hivi sasa wanawania uongozi” niliona kama anasema “watu wenye fedha kama mimi ambao hivi sasa wanawania uongozi.”
Matamshi hayo yalinithibitishia kwamba Lowassa kweli ana nia ya kuwania urais 2015. Hiyo ni haki yake lakini hana haki ya kutumia fedha zake — au hata zisizo zake — kutimiza lengo hilo kwa njia za kifisadi za kuwalisha rushwa wapiga kura au kuwanunua viongozi wenzake walio tayari kununuliwa.
Ndiyo maana labda akataka katiba ya nchi ieleze wazi nini halali na nini haramu; asije akavuka mpaka na kuingia matatani.
Suala la matumizi ya fedha za watu binafsi katika kampeni za uchaguzi ni suala linalozihangaisha nchi nyingi hata zile zinazosemakana kuwa na demokrasia iliyokomaa.
Kashfa za ufisadi katika chaguzi zimeibuka mara kadha wa kadha nchini Marekani, Uingereza na Ufaransa ambako wanasiasa mashuhuri wamekuwa wakishtumiwa kuwa ‘waliruzukiwa’ na marais kadhaa wa Kiafrika katika kampeni zao za uchaguzi.
Hivi karibuni kuliibuka shutuma kwamba rais wa zamani wa nchi Ufaransa, Nicolas Sarkozy, alipewa dola za Marekani milioni 50 na kiongozi wa zamani wa Libya Mu’ammar Qadhafi kugharamia kampeni yake ya uchaguzi ya 2007.
CCM ni chama kinachonuka uvundo wa ufisadi. Mambo yalizidi kuchacha baada ya kurejelewa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ili kupigania uchaguzi wa 1995, wa mwanzo chini ya mfumo huo wa ushindani wa vyama vingi, chama cha CCM kililazimika kutumia kila mbinu na hila, za halali na haramu, kujipatia fedha za kuendesha kampeni zake.
Hapo ndipo kazi ya kukitafutia chama fedha ikawa pia ni kazi ya kujitajarisha binafsi kwa baadhi ya vigogo vya CCM.
Kashfa nyingi za ufisadi kwa jumla zilifuatia hapo. Wakati wa enzi ya Benjamin Mkapa tuliwashuhudia wanasiasa wa CCM wakiunda ‘mtandao’ wenye lengo la kutumia madaraka ya kisiasa kuwatajirisha baadhi yao na halafu kuutumia utajiri wao kujipatia au kujiongezea madaraka ya kisiasa.
Hayo ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa benki moja kubwa nchini Tanzania, ambayo hisa zake nyingi zikimilikiwa na wanamtandao. Ndiyo pia yaliyorahisisha kashfa ya rada na kampuni ya Uingereza ya BAE Systems; ile ya kampuni ya Meremeta na ile kampuni ya Richmond iliyohusika na ununuzi wa nguvu za umeme na ambayo ilimkaba Lowassa hata akabidi ajiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu.
Uchaguzi wa 2015 unapozidi kunyemelea ndipo suala la rushwa nalo linavyozidi kuwatia kizaazaa ‘wanamtandao’ wenye kushtumiwa kuwalisha wenzao ili wawachague. Hayo yanatokea wakati ufisadi ukizidi serikalini na wakati ambapo chombo cha taifa cha kupambana na rushwa TAKUKURU kimeshindwa kuchukua hatua zifaazo kuung’oa ufisadi.
Hapo awali wanachama wa kawaida wa CCM na raia wengine wa Tanzania walikuwa wakiona kwamba chama cha CCM kimelipa mgongo na kulinyamazia suala hilo la rushwa. Lakini viongozi wa CCM waligutuka baada ya raia kuanza kulalamika na baada ya vyama vya upinzani, hasa CHADEMA kuutia makali mkakati wao wa kuiandama serikali bungeni na hata katika mikutano ya hadhara juu ya suala hilo.
Viongozi wa ngazi ya juu kabisa wakiwemo Mwenyekiti Jakaya Kikwete wakajitoa kimasomaso na wakaamua kuujadili ufisadi hadharani.
Matokeo yake ni kwamba mkutano mkuu uliopita wa CCM uliichagua safu mpya ya viongozi wenye kusemekana kwamba wamepania kukisafisha chama chao ili kinusurike kisikabwe roho na jinamizi linaloweza kukizukia 2015.
Kuna viongozi kadhaa wa CCM waliokwishajiandaa kugombea urais 2015. Baadhi yao wamekwishaanza kujinadi na wengine wanapigana vijembe na kushtumiana bila ya kutajana majina. Nao ni pamoja na Lowassa na spika wa zamani wa Bunge Samuel Sitta ambaye sasa ni waziri wa masuala ya Afrika ya Mashariki na wakitajwa pia Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje, na Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli.
Kinyanganyiro hicho cha 2015 zamani kilizusha makundi ndani ya CCM ingawa wenyewe wenye kuhusika wanakataa kuwa makundi hayo yapo. Lakini tunavyoambiwa ni kwamba Lowassa ndiye mwenye kundi kubwa linalomuunga mkono.
Wiki iliyopita Sitta aliposema kwamba ana sifa za kuwa rais aliwaonya Watanzania wasimpe madaraka ya urais mgombea asiye mwadilifu na mwenye kujilimbikizia mali. Sitta aliongeza kusema kuwa Watanzania ni werevu wa kuwatambua mafisadi.
Siku iliyofuatia ndipo Lowassa naye akanukuliwa kuyasema hayo aliyoyasema kuhusu katiba na ufafanuzi wa maana ya ‘rushwa’ katika chaguzi. Baadhi ya wachambuzi waliiona kauli yake kuwa ni ya kumjibu Sitta.
Ingawa kuna wanaomkebehi Lowassa kwa hiyo kauli yake lakini ina muhimu wake katika mfumo wa kidemokrasia kwani demokrasia ni kama kifurushi chenye michakato mingi. Penye majaaliwa tutalijadili kwa urefu wiki ijayo suala la matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi.
No comments:
Post a Comment