ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 29, 2013

Baraza Kuu latoa Ruksa Brigedi mpya kwenda DRC na kutumia nguvu

Baraza Kuu la Usalama katika Kikao chake kilichofanyika jana Alhamisi ambapo lilifungua ukurasa mpya kwa kuridhia upelekaji wa Brigedi maalum ( Intervention Brigade) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Brigedi hii inayoundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi, pamoja na mambo mengine imepewa "ruksa" ya kutumia nguvu pale itakapobidi kukabiliana, kuwadhibiti na kuwapokonya silaha makundi ya wanamgambo wenye silaha na ambao wamekuwa wakiendelea kuifanya hali ya eneo la Mashariki ya Kongo kutokuwa na amani na usalama wa kudumu. Azimio hilo lilipitishwa bila ya kupingwa na wajumbe wote 15 wakiwamo P5 wanaounda Baraza hilo. Azimio hilo lililopewa namba 2098 ( 2013) pia limeiongezea dhamana MONUSCO ili kwa kushirikiana na Brigedi hiyo mpya iweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu mkubwa.

Na Mwandishi Maalum
 Katika hali ambayo haijawahi kutokea  katika  Operesheni za Ulinzi wa Amani  za Umoja wa Mataifa. Baraza Kuu la Usalama  ,  jana (Alhamisi), kwa kauli moja,  limepitisha  azimio linaloidhinisha   kupelekwa kwa Brigedi mpya ( Intervention Brigade)   itakayokuwa na uwezo wa kutumia nguvu pale inapobidi kuyakabili, kuyadhibiti na kupokonya silaha  makundi ya wanamgambo yenye silaha katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,
 Hii ni mara ya kwanza kwa Baraza Kuu kupitisha Azimo la namna hiyo na kutoa idhini ya utumiaji wa nguvu za ziada katika shughuli za  operesheni za ulinzi wa amani  ambazo kwa  muundo na  malengo yake  ya asili ni kulinda amani na si kupigana au kutumia nguvu za ziada.
Brigedi hiyo mpya inayokadiriwa kuwa na wanajeshi 3,069 inaundwa na wanajeshi kutoka  Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi na  inatarajiwa  wakati wowote mara baada ya kupitishwa kwa Azimio   hili lililopewa namba 2098 (2013) kwenda  DRC ambako  itaungana na  walinzi wengine wa amani  waliopo huko chini ya  Misheni Maalum ya  Kutuliza  Amani maarufu  kama MONUSCO.

Uwepo wa Brigedi hiyo mpya itaiongezea uwezo MONUSCO kwa kuongeza idadi ya walinzi kufikia  19,815
Makundi ya wanamgambo yanayotarajiwa kudhibitiwa na Brigedi hii maalum na ambayo yamenyoshwa  kidole   na Azimio hilo,  ni pamoja na  kundi la M23,   Jeshi la Kidemokrasia la Ukombozi wa Rwanda ( FDLR)  na makundi mengineyo ambayo yamekuwa yakihatarisha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kongo.
 Kwa lugha nyepesi  Baraza Kuu    linatoa ruska kupitia Azimio hilo,  kwa  Brigedi hii maalum,  yenyewe kama ilivyo au kwa kushirikiana na Jeshi la Kitaifa la  DRC  kutumia  nguvu  kubwa na kwa uhodari  wa  hali ya juu    kuyakabili makundi ya waasi.
Upitishwaji wa Azimio hili na ambalo  pia limeungwa  mkono na Katibu  Mkuu  Ban Ki Moon,  linafungua  ukurasa mpya katika kushughulikia  hali tete ya  Mashariki wa DRC.Ulishuhudiwa na Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mhe, Rymond Tshibanda N’tugamulongo ambaye pamoja na mambo mengine alilishukuru  Baraza kwa kupitish azimio hilo muhimu kwa usalama na amani ya nchi yake na watu wake.
Azimio hilo   pamoja na mambo mengine linaainisha wazi kabisa  vigezo na  mipaka  ya  uendeshaji na dhamana ya Brigedi hiyo  itakayokuwa na batalioni tatu ya askari wa miguu,  kikosi cha mizinga na kikosi maalum cha upelelezi itakayokuwa na makao yake makuu katika mji wa Goma. Na kwa ujumla  imerejea na wajibu na dhamana wa MONUSCO kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Azimio ingawa Brigedi hii inadhama pana na uwajibikaji mkubwa    itakuwa ikiwajibika   kwa   Kamanda  Mkuu  wa  Misheni (Force  Commander) ya  MONUSCO
Ingawa Azimio hilo ambalo kimsingi liliasisiwa na  Ufaransa,  limeungwa  mkono  na wanachama wote 15 wanaounda Baraza  wakiwamo P5, hata hivyo kuna  baadhi ya nchi ambazo  licha ya kuunga mkono zilielezea waziwazi hofu yao  juu hasa dhanana kubwa ya matumizi ya nguvu iliyopewa Brigedi.
  Hofu ya nchi hizo ni pamoja na kwamba uwepo wa Azimio hilo siyo tu kulikuwa kunatishia madhumuni asilia ya  operesheni za  ulinzi wa amani lakini pia kuna hatari kubwa  kwa walinzi wa amani kutoka nchi zao walioko DRC kujikuta wakilazimika kutumia nguvu na hivyo kuhatarisha maisha yao, jambo ambalo ni kinyume na dhamana ya awali iliyowapeleka huko.
Nchi hizo  Guatamala, Pakistani,  Argentina na Morocco zilisema kwamba  Azimio hilo lilihitaji muda zaidi wa kujadiliwa  ili hoja za pande zote ziweze kusikilizwa na kuzingatiwa.  Zikatahadharish kwamba uamuzi huu wa kupeleka Brigedi itakayokuwa na uwezo wa kutumia nguvu, usijechukuliwa kama mfano wa kuingwa katika maeneo mengine bali  uamzi huu umetokana na mazingira tofauti ya eneo husika.

No comments: