ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 1, 2013

Malipo Muhimbili sasa kupitia benki

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dk Marina Njelekela akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam juzi. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa hospitali hiyo,Agnes Kuhenga

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, imeanza mkakati wa kudhibiti mianya ya ufisadi chini ya mpango utakaowawezesha wagonjwa, kulipia gharama za huduma kupitia benki.
Pamoja na mkakati huo, menejimenti ya hospitali hiyo kubwa nchini, imesema imebaini kuwa mrundikano wa wagonjwa, unachangiwa na udhaifu katika utoaji tiba kwenye hospitali za mikoa na wilaya.Akizungumzia mkakati wa kudhibiti mianya ya ufisadi, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela, alisema uchunguzi umebaini hatua ya kutumia benki katika kukusanya malipo ya gharama za huduma mbalimbali, itasaidia kuokoa zaidi ya asilimia 20 ya fedha zinazopotea.

“Kufanikiwa kwa mkakati huu, kutaiwezesha hospitali kuvuka lengo la kugharamia bajeti ya matuminzi ya kawaida, kwa kutumia mapato ya ndani kwa asilimi 40 kama sera ya mabadiliko ya taasisi za umma inavyoeleza,” alisema Dk Njelekela.

Alisema mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia benki, yataongeza uwezo wa kifedha kwa matumizi ya kawaida ya mapato ya ndani kutoka asilimia 58 hadi kufikia zaidi ya asilimia 72 katika mwaka wa fedha wa 2013/14.

Mkurugenzi huyo alisema tayari hospitali imeingia makubaliano na Benki ya NMB, ili kutekeleza mkakati wa kukusanya mapatio yake na kwamba hatua hiyo itaanza rasmi Machi 11 mwaka huu.

“Mfumo huo utamwezesha mgonjwa kupata hati ya gharama ya malipo ya huduma itakayokuwa inatolewa na mfanyakazi wa hospitali katika kituo cha karibu na huduma ,’”alisema

Kuhusu hospitali kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa, mkurugenzi alisema udhaifu katika utoaji wa huduma za tiba na hasa hospitali za mikoa na wilaya, unachangia kwa kiasi kikubwa.
Alisema kama Seriklai itaboresha huduma katika hospitali hizo kwa kuzipatia madaktari wa kutosha na wataalam, tatizo hilo litapungua kama si kumalizika kabisa .

Alisema Shirika la Afya la Dunia (WHO,) litaka daktari mmoja kuwahudumia wagonjwa 10,000 lakini kwa Hospitali ya Muhimbili madaktari wake wanatoa huduma kwa zaidi ya idadi hiyo.

Akizungumzia tatizo la wagonjwa kulala sakafuni, mkurugenzi alisema tatizo si upungufu wa vitanda na kwamba tatizo ni nafasi ya kuweka viwanda vya wagonjwa.

Alisema majengo ya hospitali yalijengwa kwa uwezo wa kuwekeza vitanda 35 tu.
Mwananchi

No comments: