ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 20, 2013

Tumeweza kudhibiti biashara ya nyanya na midoli kwa nini isiwe silaha- Ban Ki Moon

Nembo ya Mkutano Kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Biashara ya  Silaha,  zaidi ya wajumbe 2000 kutoka nchi 193 na  vyama visivyo vya kiserikali wanakutana hapa  Umoja wa Mataifa, katika Mkutano wa Mwisho unaotarajiwa kutoka na Mkataba ( ATT)
Silaha zaina hii na nyingineza zikiwamo  ndogo na nyepesi zimekuwa zikisababisha  madhara makubwa kwa maisha ya watu wasio na hatia pamoja na ubaribifu wa mali zao. takwimu zinaonyesha kwamba watu zaidi ya nusu milioni hufa kila mwaka ikiwa ni pamoja na wanawake 66,000 na wasichana kutokana na matumizi mabaya ya silaha. Aidha  kwa mujibu wa Ofisi  ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya silaha,  takwimu zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 2000 na 2010, karibu wafanyakazi 800 wa misaada waliuawa katika mashambulizi huku wengine 689 walijeruhiwa.

Na Mwandishi Maalum
Macho na Masikio ya Dunia yameelekezwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ( UM) ambako zaidi wa wajumbe 2000 kutoka  mataifa 193 wanakutana katika kile kinachoitwa mkutano wa mwisho kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa  kudhibiti  Biashara ya Silaha ( ATT).
Mkutano huu    umeanza siku ya jumatatu kwa kufunguliwa na  Katibu Mkuu  Ban Ki Moon. Akiwazungumza wajumbe hao, Mkuu huyo wa UM, pamoja na mambo mengine ameeleza kwamba kama  jumuiya ya kimataifa imeweza kuweka viwango vya kimataifa vinavyodhibiti utengenezaji wa T-shirt, midoli na  uzalishaji na uuzaji wa nyanya kwanini ishindikane  kudhibiti na kuweka viwango kwenye silaha.

Akasema Ban Ki Moon “  Tumeweka viwako karibu katika kila bidhaa kuanzia utengenezaji wa T-shirt, midoli  hadi kwenye nyanya, lakini si biashara ya  silaha” akahoji   Ban Ki Moon
Na kwa sababu hiyo amewataka washiriki wa mkutano huu kuonyesha dhamira ya kisiasa ya kukamilisha majadiliano ili hatimaye ifikapo Marchi 28 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya mkutano watoke na Mkataba, kama ilivyoainishwa  kwenye mkutano wa tisa kwamba mkutano huu ni wa mwisho.
Akaenda mbali zaidi kwa kuwahadharisha wajumbe kwamba  wanapokutana katika mkutano huu, hawaanzi upya majadiliano ya mkataba, majadiliano  ambayo yalifanyika tangu  mwaka 2006 wakati mchako wa ATT ulipoanza. Bali wanakuta  kukamilisha kazi ya kutoka na Mkataba.
Mkutano huu unafanyika ikiwa ni mwaka mmoja tangu  kumalizika kwa mkutano wa Kihistoria  uliofanyika mwaka jana ( 2012) ambapo kulikuwa na matumaini makubwa kwamba  mkutano ule ungemalizika kwa kutoka na Mkataba lakini hali haikuwa hivyo.
Ujumbe wa Tanzanzia katika mkutano huu  muhimu  unaongozwa na  Balozi  Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Ujumbe huu unawahusisha wataalam kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama,  Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, TRA na wajumbe wawili kutoka Asasi isiyo ya kiserikali.
Kwa ujumla ujumbe wa Tanzania umejipanga vema katika kufuatilia kila hatua ya majadiliano,  kutoa msimamo wa Tanzania na kuhakikisha kwamba maslahi ya nchi yanalindwa.
Akichangia majadiliano ya jumla,  Balozi Mwinyi alieleza bayana kwamba, nia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kwamba Mkataba huo  unalenga wanachama wote.
Aidha akafafanua zaidi kwa kusema Tanzania inaamini kwamba  lengo na madhumuni ya Mkataba huo ni kudhibiti biashara haramu ya silaha  bila ya kuathiri haki ya mataifa kujilinda kama ilivyoainishwa kwenye  Katiba ya Umoja wa  Mataifa.
Vilevile akaeleza kwamba  Mkataba huo hautaingilia   haki ya mataifa kuishi kwa amani na usalama, kufurahia uhuru wao na kujiletea maendeleo, lakini kubwa zaidi ni kwamba mkataba huo haulengi kupokonya silaha bali kudhibiti.
Baadhi ya wazungumzaji hususani wale wanaotoka nchi kubwa wameanza kuweka mikingamo yao kwa kutoa kauli za kutahadharisha kwamba hazita saini au kuridhia Mkataba huo kama hautakuwa na mashiko, dhaifu au kwa namna moja ama nyingine utakuwa unaingilia maslahi yao na masuala  yao ya ndani
Tayari washiriki wa mkutano huu wamekwisha  anza jukumu la kupitia kipengere kwa kipengere  Rasimu ya Mkataba. Hatua hii inazipa fursa nchi wanachama  kuchangia maoni yao  ya  kuiboredha rasmu hiyo kwa ama kupunguza baadhi ya vipengere,   kuongeza na hata kuondoa kabisa baadhi ya vipengere.


No comments: