ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 19, 2013

Wamiliki vituo vya utangazaji wataka muda zaidi kujenga miundombinu



Wamiliki wa vituo vya utangazaji nchini, wamesema hawapingi mfumo wa kuhama kurusha matangazo ya televisheni kutoka analogia kwenda digitali, badala yake wanapendekeza teknolojia zote mbili zitumike kwa manufaa ya wananchi maskini pamoja na wamiliki hao kupata muda zaidi wa kujenga miundombinu ya mfumo huo.
 
Wamesema siyo rahisi kwa mmiliki wa televisheni kupinga mfumo wa digitali kwa kuwa tayari wamekwishawekeza mamilioni ya dola za Marekani kwenye ujenzi na ununuzi wa vifaa vya kurusha matangazo kwa mfumo wa digitali.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Dk. Reginald Mengi, alisema mfumo wa digitali ni mzuri, lakini hakuna haraka yoyote kwa Tanzania kuzima analojia kwa kuwa bado kuna muda wa kujiandaa na kufanya vizuri zaidi.
 
Alisema lengo la wamiliki kuomba mifumo yote iende kwa pamoja ni kuwasaidia wananchi maskini ili mfumo wa digitali uwe wa manufaa kwa pande zote.
 
Dk. Mengi ambaye alifuatana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Media Group Ltd (Star TV), Samuel Nyalla, Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na Rais wa Wapo Mission International, Askofu Sylivester Gamanywa, alikuwa akitoa ufafanuzi wa maoni ya wamiliki wa televisheni kuhusu maombi ya kutumia analojia na digitali kwa pamoja ambayo waliyaeleza wiki iliyopita.
 
Alisema leseni za kufunga mitambo ya digitali zilianza kutolewa mwaka 2010 japokuwa mchakato wa mpango huo ulianza mwaka 2006. Alisema muda wa miaka miwili wa kuanza kujenga miundombinu na teknolijia za kisasa kwa ajili ya mfumo huo hautoshi.
 
Alitolea mfano kwamba nchi tajiri duniani kama Japan ilichukua miaka minane kuzima mfumo wa analojia wakati Marekani ilitumia miaka 11 na Uingereza miaka 14.
 
"Hapa Tanzania tulipata leseni ya kujenga miundombinu ya digitali mwaka 2010, tunaweza kufanya haraka iwezekanavyo lakini tujiulize tuna nini wakati nchi kama Marekani ilichukua miaka 11?" alihoji.
 
Alisema kwa mujibu wa azimio la mkutano wa Geneva wa mwaka 2006 na ule wa Mawaziri wa Sadc wa mwaka 2011, nchi zote zinapaswa kuhamia digitali ifikapo Juni 17, mwaka 2015, hivyo Tanzania ina fursa ya kufanya vizuri zaidi.
 
Alisema athari za serikali kuzima mfumo wa analojia kwenda digitali ni dhahiri, kwa kuwa wananchi wengi waliokuwa wanamiliki televisheni hawana tena fursa ya kuangalia taarifa ya habari wala matangazo mengine.
 
Alisema utafiti wao umebaini kwamba televisheni milioni saba zinamilikiwa na watu mbalimbali hapa nchini, lakini ving'amuzi ambavyo hadi sasa vimeshauzwa havifiki nusu ya idadi hiyo.
 
Alisema tv milioni 2.5 zinatumiwa na wakazi wa Dar es Salaam ambao walikuwa na uwezo wa kuangalia habari na matangazo mengine wakati wa mfumo wa analojia lakini hivi sasa asilimia 75 ya wakazi hao hawana tena fursa hiyo baada ya serikali kuzima mitambo ya analojia na kuingia digitali.
 
"Hao wanaosema kwamba tunapinga digitali nina hakika wanafahamu kwamba siyo kweli au pengine wanapotosha ukweli kwa makusudi, sisi tuliomba muda ili wananchi wengi zaidi waendelee kupata habari na wamiliki wajenge miundombinu ya mfumo huu," alisema.
 
Alisema muda wa miaka miwili waliopewa wamiliki wa televisheni hautoshi kujenga miundombinu pamoja na kuagiza ving'amuzi vya teknolojia ya kisasa.
 
Mengi alisema bado wamiliki wa televisheni wana imani na serikali kwamba itayafanyia kazi maoni yao kwa manufaa ya Taifa zima. 
 
Alisema wamiliki wanataka kutumia teknolojia ya kisasa ya utangazaji na ambayo ni toleo la mwisho ya DVBT2 ambayo ni mfumo mzuri wa kuhamia digitali.
 
Kwa upande wake, Nyalla wa Sahara Media Group, alisema awali walifanya majadiliano na serikali lakini baada ya kuona athari za kuzimwa kwa mfumo wa analojia ndipo walipowasilisha kilio chao kupitia vyombo vya habari.
 
"Bado kuna nafasi ya kuendelea kutoa habari kwa wananchi, tunaweza kuwa na muda wa kubadilisha huu mfumo. Tujiulize kwanza Tanzania ilikuwa ya kwanza kuingia kwenye televisheni, tujiulize kwa nini wenzetu hawajakimbilia huku," alisema.
 
Alisema baada ya kupata leseni za digitali, pamoja na mambo mengine, waliagiza ving'amuzi na walikuta teknolojia mpya na ya kisasa ambayo ilikuwa toleo jipya hivyo walilazimika kuagiza kwa oda maalum.
 
Aidha, katika mkutano huo, takriban waandishi wa habari 60 kutoka vyombo mbalimbali walieleza kutoridhika na mfumo wa sasa wa digitali kwa kuwa wakati mwingine picha zinakatika na mara nyingine sauti haisikiki.
 
Bakari Kimwanga, ni mwandishi wa gazeti la Mtanzania ambaye alieleza kwamba amekumbana na tatizo la king'amuzi chake kusumbua kwa kuwa mara kwa mara kimekuwa kikipoteza sauti na picha kutoonekana vizuri wakati wa taarifa ya habari.
 
"Kama jana nilikuwa naangalia taarifa ya habari iliyohusu klabu yangu ya Simba, lakini wakati inasomwa, sauti na picha vilipotea kwa hiyo binafsi ninaona mfumo huu ni bado, serikali iutazame upya," alisema.
 
Mwandishi wa EATV, Noah Laltaika, alisema amekuwa akipata wakati mgumu pindi anapofanya mahojiano na wananchi mitaani kwa kuwa hukataa kuhojiwa kwa sababu hawatajiona kwenye televisheni wakati wa habari au kwenye kipindi husika.
 
Machi 11, mwaka huu, wamiliki hao walizungumza na waandishi wa habari na kuiomba serikali iruhusu kwa muda matumizi ya mfumo wa utangazaji wa analojia na digitali ili wananchi wasiokuwa na uwezo waendelee kupata habari kupitia runinga.
 
Walisema kuharakishwa kwa uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya analojia nchini, kunawakosesha wananchi wengi wa kipato cha chini haki ya Kikatiba ya kupata habari kupitia televisheni kwa kushindwa kumudu bei ya ving’amuzi, huku vituo vya televisheni vikikabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na kupungua kwa kasi ya matangazo ya biashara.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: