ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 12, 2013

Dar yarejea enzi za ujima



Wakati nauli mpya za daladala, mabasi na treni zikianza kutumika rasmi leo, hali ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam imezidi kuwa mbaya kutokana na mabasi kuwa machache na hivyo kusababisha abiria kulazimika kusafiri kwa malori na magari mengi madogo huku wakitozwa nauli kubwa.
 
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa maeneo ambayo yamekumbwa zaidi na tatizo la usafiri ni kutoka Mwenge kwenda Tegeta, Mwenge-Kibaoni, Ubungo-Mbezi, Ubungo-Mbagala, Gongolamboto-Mwenge na Ubungo kwenda Mlandizi.
 
Kutokana na ukosefu wa daladala kwenye maeneo hayo, kwa takribani wiki moja sasa wananchi wamekuwa wakitumia malori, Toyota Noah, Bajaj, Pick Up, teksi pamoja na Toyota Coaster ambazo hazijasajiliwa kuchukua abiria jijini hapa.
 
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kutokana na ukosefu wa daladala, hali hiyo imetoa fursa kwa magari yaliyoanza kutoa huduma ya usafiri kwenye maeneo hayo kutoza abiria nauli kubwa ambayo haipo katika viwango vya nauli vilivyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra). Nauli inayotozwa na wamiliki magari hayo mfano kutoka Mwenge hadi Tegeta, Mwenge-Bunju, Mwenge-Kibaoni ni Sh.1,000 hadi 2,000 kwa mtu mmoja badala ya Sh. 300 au 400 ya sasa.
 
Kutoka Ubungo kwenda Mbezi, Ubungo-Mbagala, nauli zinazotozwa ni kati ya Sh. 500 hadi 1,000 badala ya Sh.300 wakati kutoka Ubungo-Mlandazi ni Sh.1,000 hadi 2,500.
Magari yaliyobainika kutoza nauli kubwa ni yale ambayo hayajasajiliwa na Sumatra kutoa huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na yaliyoiba njia.
 
Aidha, daladala ambazo zimesajiliwa kutoa huduma jijini hapa, zinaongoza kukatisha ruti (kuiba njia) na zinafanya hivyo ziweze kurejea mapema vituoni kuchukua abiria wengine hali ambayo inakuwa ni faida kwao. 
 
Mathalani, katika kituo cha Mwenge inapofika jioni, gari za ruti ya Tandika-Mwenge kupitia barabara ya Ali Hassan zimekuwa zikipakia Ubungo na kisha kushusha abiria wote na kupakia tena kwenda Bugurudi na zinapofika hapo hupakia kwenda Tandika.
 
Wakati mwingine, gari hizo zinapofika Ubungo hurudi tena Mwenge kupakia abiria.
 
Wakizunguma na NIPASHE kituo cha Ubungo, abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Mbezi Luis, walisema tatizo la usafiri limekuwa sugu na kwamba wakati mwingine wanachukua zaidi ya saa tano kupata gari.
 
Amon Kisimbo mkazi wa Mbezi Luis alisema tatizo la usafiri katika jiji la Dar es Salaam linasababishwa na msongamano wa malori na kwamba serikali inatakiwa kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowahi kutolewa mwaka 2009.
 
Kisimbo ambaye alidai alikuwa miongoni mwa watu walioshiriki kuandaa mapendekezo hayo katika tume iliyoundwa na serikali, alisema pendekezo walilotoa ni kutaka Bandari ya Dar es Salaam ihamishwe kutoka ilipo sababu inasababisha malori kupita katikati ya jiji na hivyo kusababisha msongano usiokuwa wa lazima. Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Kanda ya Mashariki, Conrad Shio, akizunguza na NIPASHE jana alisema kutokana na ukiukwaji wa sheria za barabara unaofanywa na wenye magari hayo, magari 74 yamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali.
 
Shio alisema magari 36 yamekamatwa kwa kukatisha ruti, 18 kwa kuiba ruti na magari 20 yamekamatwa kwa kutoza nauli kubwa.
 
Alisema magari ambayo yamekamatwa kwa kosa la kukatisha ruti wamiliki wake watatakiwa kwenda Sumatra na mkataba wa madereva wengine na hao waliosababisha kosa hilo hawataruhusiwa kufaya kazi ya udereva mahali popote nchini.
 
Alisema tatizo la ukosefu wa magari katika baadhi ya maeneo linatokana na kwamba Sumatra imesimamisha usajili katika ruti ya barabara ya Ali Hasani Mwinyi-Kilwa kwa sababu kuanzia Julai mwaka huu wamiliki wa daladala watatakiwa kujiunga katika kampuni ili kutoa huduma ya usafiri kwenye ruti hiyo.
 
Alisema siyo kweli kwamba daladala zimeadimika na kwamba baadhi ya wamiliki wanakwepa kusajili magari yao kwenye njia zenye foleni kubwa kama Mbezi-Kimara hadi Kivukoni au Kariakoo.
 
MWAKYEMBE ABARIKI NAULI
Serikali imebariki ongezeko jipya la nauli za mabasi yanayotoa huduma mijini, ya masafa marefu na treni hivyo kuziruhusu kuanza kutumika rasmi leo.
 
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliwaambia wanahabari jana mjini Dodoma kuwa nauli mpya imeongeza Sh. 50 kwa mwanafunzi na Sh. 100 kwa watu wazima; hivyo daladala zitatoza Sh. 400 badala ya 300 na wanafunzi Sh. 200 badala ya Sh. 150.
 
Alisema  serikali imeridhia ongezeko la nauli lililotangazwa na Sumatra, baada ya kuhakiki na kujiridhisha kuwa ongezeko hilo lilizingatia mchakato wa kupandisha nauli na viwango viliridhiwa na wadau wanaowakilisha maslahi ya wanaotoa na wale wanaotumia huduma hiyo.
 
“Mimi kama Waziri wa Uchukuzi sina tatizo na ongezeko hili dogo la nauli za daladala tatizo langu ni tabia ya Watanzania kukacha vikao halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kusubiri kuja kulalamika baadaye,” alisema Dk. Mwakyembe.
 
Alisema hayo akiwakosoa wananchi na asasi nyingine kulalamikia nauli nje ya utaratibu licha ya vikao vya kuwataka kutoa maoni kupitia Sumatra kutangazwa na kuwataka wananchi wajitokeze wakati maombi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri ya kupandisha nauli yalipokuwa yanajadiliwa.
 
Waziri Mwakyembe alisema maombi ya kuongezwa nauli hiyo mpya yalitolewa baada ya wadau wakiwamo Baraza la Taifa la Walaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Sumatra, Chuo cha Usafirishaji, vikiwamo vyama vya watoa huduma vya madereva vya kutetea abiria na wanahabari, kuridhia.
 
“Kulikuwa na mvutano mkubwa wamiliki wakitaka nauli iongezeke na wawakilishi wa abiria wakitaka nauli ibakie ile ile iliyotangazwa mwaka 2011. Ndipo maamuzi  ya nyongeza ya nyongeza ndogo yakawa Sh. 100 na Sh. 50 kwa mwanafunzi yakaafikiwa,” alisema.
 
Aliongeza kuwa wawakilishi wa abiria na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji waliamriwa kuwa iwapo kuna upande usioridhia ukate rufaa kwenye Baraza la  Ushindani, lakini hakuna aliyefanya hivyo.
 
Wiki iliyopita Waziri Mwakyembe alisema wizara hiyo itapitia nauli hizo kutokana na malalamiko mengi kutolewa na wananchi wakipinga nyongeza hiyo.
Imeandikwa na Gaudensia Mngumi, Dodoma na Thobias Mwanakatwe, Dar
CHANZO: NIPASHE

No comments: