Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akizungumza wakati Bunge lilipokaa kama kamati kwa ajili ya kupitisha mafungu ya fedha ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2013/14, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Maji jana ilipita kwa mbinde baada ya kukwama mara mbili bungeni.Imepita baada ya Serikali kuongeza Sh184.5 bilioni kama Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ilivyokuwa imependekeza na kuungwa mkono na wabunge wengi.
Awali, Bajeti hiyo ilikwama kupitishwa tena katika kipindi cha jana asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kukatiza mjadala wake kutokana na wabunge kuibana Serikali kwa kukiuka vipengele kadhaa wakati ilipowasilisha upya hoja hiyo.
Mara ya kwanza Bajeti hiyo ilikwama wiki iliyopita baada ya wabunge kushinikiza kuongezwa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza maji vijijini.
Jana asubuhi, Makinda alisitisha shughuli za Bunge saa 5.45 asubuhi ikiwa mapema kabla ya muda wa kawaida wa kumalizika kwa vipindi vya asubuhi ya Bunge ambao ni saa 7.00 mchana baada ya wabunge kupinga utaratibu wa uwasilishaji upya wa Bajeti hiyo.
Licha ya Serikali kuongeza Sh184.5 bilioni, bado baadhi ya wabunge wa Chadema waliomba Bajeti hiyo iahirishwe kujadiliwa wakisema nyongeza hiyo haina ushahidi wa utekelezaji.
Baada ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuwasilisha kauli ya Serikali kuhusu kuongeza fedha kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kusoma marekebisho ya bajeti yake na kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alihoji sababu za Serikali kuwasilisha kauli ya kuongeza fedha bila kuwagawia wabunge nakala kama kanuni zinavyotaka.
“Mwaka juzi tulitaka fedha ziongezwe Wizara ya Uchukuzi na Serikali ikasema imeongeza Sh94 bilioni na tukapiga makofi sana hapa, lakini haikuongezwa hata senti moja.”
Pia, Zitto alisema mwaka 2011 walikubaliana fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa kupelekwa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), lakini hakuna kilichopelekwa mpaka sasa.
Kutokana hali hiyo, alitaka hoja hiyo kutolewa kwa maandishi na wabunge wapewe nakala zake ili waibane Serikali pale itakaposhindwa kutekeleza.
Kutokana hali hiyo, alitaka hoja hiyo kutolewa kwa maandishi na wabunge wapewe nakala zake ili waibane Serikali pale itakaposhindwa kutekeleza.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye alitinga bungeni baada ya kutumikia adhabu ya kusimamishwa kwa siku tano, alisema kwa mujibu wa taratibu za Bunge, kauli za Serikali lazima zisambazwe kwa wabunge tofauti na kauli ya Waziri wa Fedha akisema hata Spika hakuwa na nakala yoyote huku akisema Waziri alitoa kauli hiyo akiwa hana anachokisoma.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alitaka hoja hiyo kuondolewa mezani kwa sababu Waziri wa Maji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, hakutoa jedwali linaloonyesha matumizi ya fedha hizo.
Akitoa mwongozo wake, Spika Makinda alisema Waziri wa Fedha alitoa tamko la Serikali bila wabunge kuwa na nakala kutokana na haraka iliyokuwapo... “Tuliona haiwezekani Waziri wa Maji aseme peke yake juu ya ongezeko la fedha hizo, ndiyo maana Waziri wa Fedha akaja kutoa tamko hapa.”
Hata hivyo, Makinda alikubaliana na hoja ya Mnyika na kuahirisha Bunge huku akitaka jedwali linaloonyesha matumizi ya fedha hizo liandaliwe.
Hata katika kipindi cha jioni, Mnyika aliendelea na msimamo wake kwa kutoa hoja akitaka kupata hakikisho la Serikali kwamba fedha hizo zitakuwapo kweli na siyo danganya toto ili kupitisha bajeti hiyo hoja ambayo iliungwa mkono na kumlazimu Waziri wa Fedha kusimama na kutoa hakikisho hilo akisema: “ Serikali itahakikisha fedha zinazopitishwa zinapatikana.”
Akiahirisha Bunge, Spika Makinda alisema fedha hizo zitatoka ndani ya Bajeti hiyo inayoendelea kujadiliwa na hazitatoka nje.
Hatua hiyo ilifanya bajeti hiyo kuondolewa kwa mara ya pili bungeni na hivyo kuingizwa kwenye kumbukumbu za bajeti zilizowahi kuondolewa kwa sababu ya kutokidhi matakwa ya hoja za wabunge.
Awali, Dk Mgimwa akitoa tamko la Serikali alisema wameamua kufanya maji kuwa kipaumbele kutokana na umuhimu wake.
Alisema Serikali imetafuta fedha za ziada ambazo zimetoka kwenye matumizi mengine, hasa posho ambazo hazitaathiri uendeshaji wa Serikali.
Kwa upande wake, Profesa Maghembe alisema Serikali imeongeza Sh184.5 bilioni kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment