ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 30, 2013

Wanaume waongozana na wake zao kliniki

Mume na mke wapo kliniki wanahudumiwa
Na George Ramadhani.
Kuna dhana imejengeka nchini miongoni mwa wanaume kwamba ni wanawake pekee ndio wenye wajibu wa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.Katika miaka ya karibuni kuna kampeni kubwa ya kuwataka wanaume waongozane na wenza wao kliniki ili kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi. Makala hii yafafanua zaidi

“KUTOKANA na mila na desturi, binafsi nilipanga kuzaa watoto watano. Hata hivyo, mume wangu anaonekana kuwa kinyume na mawazo yangu na amekuwa mara zote akisisitiza kwamba angependa tuzae watoto watatu tu,” anasema Mecktrida Masumbuko (30) mkazi wa kijiji cha Bukongo katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza..  Mecktrida wakati wa mahojiano haya alikuwa kwenye foleni ya kusubiri huduma ya kliniki katika hospitali ya wilaya ya Ukerewe, anasema kwamba hadi sasa yeye na mume wake ambaye ni mvuvi wamefanikiwa kupata watoto wawili ambao wametofautiana kwa miaka miwili.Anasema kwamba, tangu alipoolewa amekuwa na mawazo ya kuzaa watoto watano akiamini kwamba atakuwa amezingatia uzazi wa mpango. Katika familia yake wamezaliwa watoto 12.

Hata hivyo anasema kwamba ,anaona kila dalili kuwa ndoto yake ya kuzaa watoto watano huenda isitimie kutokana na msimamo wa mume wake.

Anabainisha kuwa, chanzo cha mume wake kuwa na msimamo wa kuzaa watoto wasiozidi watatu ni baada ya kuhudhuria kliniki na kushauriwa kufanya hivyo.

“Unajua siku hizi akina mama tunapohudhuria kliniki tunashauriwa kufuatana na wenza wetu. Nilipomuambia mume wangu alikubali bila kusita,”anasema.

Anaongeza kuwa, tangu siku ya kwanza alipohudhuria kliniki, mume wake ameonekana kufanyia kazi ushauri waliopewa na wataalam wa afya ya uzazi ikiwemo kuzaa idadi ndogo ya watoto watakaoweza kuwatunza.

Anasema kwamba licha ya kutumia muda mwingi akiwa katika shughuli zake za uvuvi, lakini anapokuwa nyumbani mume wake hufuatana naye kwenda kliniki kwa ajili ya kupima ujauzito au mtoto na hufundishwa jinsi ya kuzuia maambukizo ya Virusi vya Ukimwi kutoka mama kwenda kwa mtoto.

Kwa mujibu wa Mecktrida, hatua hiyo ya mumewe kukubali kuambatana naye kwenda kliniki imeimarisha ndoa yao kwa sababu kila kitu kuhusu uzazi wanakifanya kwa kushirikiana na kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam.

“Unajua wanaume wengi wana hulka ya kutopenda kujihusisha kwa karibu na masuala ya afya ya uzazi.Wanapenda kutuacha sisi wanawake twende kliniki peke yetu. Inakuwa vigumu kufanyia kazi ushauri wote tunaopewa kwa sababu wengi wetu hatuna kauli kwa waume zetu,”anasema.

Anafafanua kwamba, kwa mila na desturi za wenyeji wa wilaya ya Ukerewe mwanamke hana mamlaka ya kumpa maelekezo mumewe, hivyo imekuwa vigumu wanawake kufikisha ushauri waliopewa kliniki kwa wenza wao.

Hata hivyo anasema kwamba, kwake hali ni tofauti kwa sababu uamuzi wa mumewe kukubali kuongozana naye kwenda kliniki kimemsaidia kupata ushauri moja kwa moja kutoka kwa wataalam na amekuwa akiufanyia kazi.

“Mimi na mume wangu tunaishi kwa maelewano hasa linapokuja suala la afya ya uzazi. Hakuna mahali tunabishana kwa sababu kila mtu anajua wajibu wake kwa kuzingatia ushauri tunaopewa kliniki. Sasa sina simanzi tena kuhusu mapenzi kwa sababu namuamini mume wangu na yeye ananiamini,”anasisitiza.

Yohana Makene (19) mkazi wa kijiji cha Nkilizya wilayani Ukerewe, ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka jana (2012) alionekana ameongozana na msichana mdogo wa rika lake kwenda katika kliniki ya hospitali ya wilaya hiyo.

Yohana alisema amefika kliniki kwa ajili ya kumsindikiza mwenza wake mwenye ujauzito wa miezi sita.

Anasema kwamba, kimsingi wao si mume na mke kama ambavyo ingeweza kudhaniwa isipokuwa wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi tu huku kila mtu anaishi nyumbani kwa wazazi wake.
Yohana anasema amemaliza kidato cha nne mwaka jana, mwenza wake aitwaye Margareth Valentine ameishia darasa la saba, na walipoanza uhusiano wa kimapenzi wakajikuta wametengeneza ujauzito usiotarajiwa.

Hata hivyo, hali hiyo haijawa kikwazo kwa Yohana kushirikiana na rafiki yake huyo kulea mimba kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi ikiwemo kinga ya maambukizi ya VVU kutoka mama kwenda kwa mtoto.

Anasema kuwa, mara tu alipoambiwa na mwenza wake kwamba wanatakiwa kwenda pamoja kliniki, hakuhisi ubaya wowote badala yake alikubali, na siku ilipowadia wakaongozana kwenda kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi.

Anabainisha kwamba , licha ya kuambiwa na mwenza wake, kilichomsukuma kwenda kliniki ni taarifa kuhusu afya ya uzazi ambazo amekuwa akizipata kupitia matangazo mbalimbali ya redio, televisheni na machapisho.

“Nimekuwa nikisikia na hata kuona matangazo yanayosema kwamba mwanamke anapopata ujauzito tangu siku ya kwanza anapaswa kuongozana na mwenza wake kwenda kliniki, kwa hiyo hata mimi Margareth aliponiambia tuje niliona ni sawa tu,”anasema.

Anaongeza kwamba, kuongozana na mwenza wake kliniki kumemsaidia kufahamu mambo mengi kuhusu afya ya uzazi, kwa sababu kuna baadhi ya mambo hayapo kwenye matangazo lakini ukifika kliniki unayapata.

Aidha anasema kwamba, kitu kingine alichojifunza ni kwamba mjamzito anapoongozana na mwenza wake kliniki anahudumiwa kwa haraka zaidi tofauti na wale wanaokwenda bila wenza wao.

“Kuna kitu hapa kimenifurahisha kwani ingawa nimekuja na mwenzangu tukiwa tumechelewa kidogo lakini tulipofika tu mara moja tumepokelewa na kupewa huduma. Hali hii imenipa somo kwamba wanawake wanaosindikizwa kliniki na wenza wao hawapati adha ya kukaa kwenye foleni,”anasema.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Busunda wilayani Ukerewe Francisco China, anaunga mkono hoja hiyo kwamba, hata yeye wakati mke wake akiwa mjamzito hadi alipojifungua alijitahidi kumsindikiza kliniki ili kumuwezesha kupata huduma kwa haraka.

Anasema kwamba, licha ya kupata huduma kwa haraka lakini kuhudhuria kliniki na mke wake kumewasaidia kujua mbinu nyingi za kupanga uzazi ambazo hazina athari kwao wala kwa watoto.

“Nilipokuwa namsindikiza mke wangu kliniki nilijifunza mambo mengi sana, kwanza tulipokuwa tunafika tulihudumiwa kwa haraka bila kujali kama tumewakuta wengine wasio na wenza wao.Pia imetusaidia kupanga vizuri uzazi tofauti na huko nyuma nilipokuwa siendi kliniki.

Kuna mambo mengine tulikuwa hatuyazingatii kwa sababu haikuwa rahisi kwa mke wangu kukumbuka na kuniambia kila kitu alichoelezwa na wataalam,”anasema China.

Sophia Donald (25) mkazi wa Bukongo wilayani Ukerewe anasema kwamba, ingawa inatokea mara chache, lakini anapoongozana na mumewe kliniki hujisikia fahari sana mbele ya wanawake wenzake.

“Natamani muda wote anapokuwa nyumbani tuongozane kwenda kliniki kwa sababu najisikia fahari.Lakini pia kuna ushauri kuhusu afya ya uzazi tunaopewa pamoja inakuwa rahisi kuutekeleza,”anasema.

Muuguzi Kiongozi katika kliniki iliyopo hospitali ya wilaya ya Ukerewe Leticia Petro anasema kwamba siku zote wamekuwa wakiwasisitiza wanawake wajawazito na wenye watoto kuambatana na wenza wao pindi wanapofika kliniki.

Anasema sababu kubwa ni kuwezesha wenza wote wawili kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi ikiwemo uzazi wa mpango na kinga ya maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Anasema kwamba, wakati wa kliniki akina mama hufanyiwa vipimo mbalimbali vikiwemo vya magonjwa ya zinaa na wale wanaobainika kuambukizwa hupatiwa matibabu bure.

Kwa msingi huo, anasema kwamba mama anapokuwa ameongozana na mwenza wake inakuwa rahisi kupewa ushauri wa kitaalam ili kuzuia maambukizo zaidi.

“Kuna baadhi ya kina mama tunapowapima tunabaini wameambukizwa magonjwa ya zinaa. Kwa sababu wanakuja peke yao inakuwa vigumu kupata tiba sahihi hata kama tukimtibu yeye bado akirudi kwa mumewe anaweza kuambukizwa tena,”anasema.

Anatoa mfano kwamba, hivi karibuni mama mmoja alipimwa na kukutwa ameambukizwa ugonjwa wa kaswende, wakamshauri akamlete mumewe ili naye apimwe kisha wapatiwe tiba kwa pamoja.

Hata hivyo anasema kwamba, mama huyo alipokwenda kumwambia mumewe kuwa anahitajika kliniki aligoma kwenda huku akidai kuwa hajisikii kuumwa chochote.

Anabainisha kuwa, ndiyo sababu mara zote wamekuwa wakiwasisitiza akina mama kuongozana na wenza wao ili kama kuna jambo lolote linalohitaji ufumbuzi wa pamoja iwe rahisi kulifanyia kazi.

“Mara nyingi wanaume wanaposhindwa kuja kliniki huwa hawazingatii ushauri tunaowapa wake zao hali ambayo huchangia sio tu kuzaa watoto bila mpangilio lakini pia maambukizo zaidi ya magonjwa ya zinaa na hata virusi vya Ukimwi,”anasisitiza.

Anaongeza kwamba, wanawake ambao hawaongozani na wenza wao kliniki imekuwa vigumu kupata huduma nzuri katika kipindi cha ujauzito au malezi ya mtoto kwa sababu anayemiliki uchumi (mume) anakuwa hajui chochote kuhusu afya ya uzazi.

“Hapa Ukerewe wanaume wengi ndio wanaomiliki uchumi, hivyo wanaposhindwa kuja kliniki inakuwa vigumu kuwahudumia kikamilifu wake zao katika kipindi cha ujauzito kwa sababu hawana elimu kuhusu afya ya uzazi, matokeo yake baadhi yao hupoteza maisha wakati wa kujifungua,”anasema.

Anaongeza kwamba ili kuhakikisha wanawake wanakwenda kliniki na waume zao, wameweka utaratibu kwamba anayekwenda na mwenza wake anapewa kipaumbele katika huduma, hata kama amewakuta wenzake atahudumiwa kwanza.

Anashauri kwamba, wanaume wajitahidi kuongozana na wenza wao kliniki kwa sababu inasaidia kupatikana kwa huduma ya uhakika na haraka hospitalini na nyumbani, na kwamba kliniki ni kwa ajili ya baba, mama na mtoto.

Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani Ukerewe, Moshi Mugono anasema kwamba, wanaume wengi katika wilaya hiyo hawana mwamko wa kuwasindikiza wake zao kliniki.

Wachache ambao wamepata mwamko wa kuwasindikiza wake zao kliniki anasema, wamekuwa na mafanikio makubwa katika suala zima la afya ya uzazi hata kumudu kuzaa watoto wachache wanaoweza kuwatunza na kuzuia mapema maambukizo ya VVU kutoka mama kwenda kwa mtoto.

Anasema kwamba wanaume wasiohudhurii kliniki na wake zao wamejikuta wakizaa watoto wengi wanaoshindwa kuwatunza kwa kuwapa chakula bora na kuwapeleka shule.

“Hapa Ukerewe kuna mtazamo kwamba kuzaa watoto wengi ni fahari, hivyo utakuta wanawake wengi wenye umri kati ya miaka 25 hadi 40 tayari wamebeba mimba kati ya mara 6 hadi 8, na wengine mara 10 hadi 13,”anasema.

Hata hivyo, anasema kwamba wengi wao wamejikuta mimba zikitoka kutokana na kushindwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi.

1 comment:

Anonymous said...

ndo inavyo takiwa hivi ujuwe hasa kinachomsibi mwenzako siyo unamuacha aende peke yake klinik na pia waruhusiwe wakati wanapokuwa katika chumba cha kujifungulia wakina mama wakiwa nanajifungua wanaume wao wawepo its time for tanzania guys to be really parners in marrige sio leo huyu kuwa bwana mkubwa na kitambi chake na mwingine mfuate mkiaa