Friday, May 3, 2013

Tabia ya virusi yakwaza upatikanaji chanjo ya Ukimwi

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas),Profesa Ephata Kaaya.
Mojawapo ya vikwazo vinavyopelekea watafiti na taasisi za tiba duniani kutofanikiwa haraka kupata chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi ni Virusi vinavyosababisha ugonjwa huo kubadilika mara kwa mara.

Hayo yameelezwa jana na  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas),Profesa Ephata Kaaya, wakati wa mkutano wa sayansi wa tafiti za tiba juu ya kupunguza umasikini, uliowakutanisha watafiti mbalimbali wa magonjwa na madaktari bingwa.


Alisema kwa sasa watafiti kupata chanjo ya ugonjwa huo ni vigumu kutokana na virusi hivyo kubadilika kila siku licha wanasayansi kuendelea kila siku kupambana kupata tiba ya ugonjwa huo.

Alisema Muhas walianza kufanya utafiti wa kupata chanjo hiyo tangu miaka ya 1980, na kueleza kuwa mpaka sasa bado wanaendelea na mchakato huo, lakini zoezi hilo litachukua miaka mingi kutoka na sababu mbalimbali ikiwamo virusi kubadilika.

“Mikakati ya utafiti bado tunaendelea kuifanya, lakini bado hatujafikia sehemu kusema tumefanikiwa,” alisema Kaaya

Kaaya alisema sababu zingine zinazopelekea tafiti nyingi za tiba kutokamilika kwa wakati ni uhaba wa vitendea kazi pamoja na fedha na kwamba serikali inapaswa kutilia mkazo katika idara za tafiti za tiba nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocen Road, Profesa Twalib Ngoma, alisema nchi nyingi duniani zimeendelea kutokana na kufanya tafiti na kuiomba serikali kuekeza katika tafiti za kisayansi.

Alisema awali watafiti wengi walikuwa wakifanya tafiti katika kagonjwa yanayoambukiza na kuyasahau yale yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yamekuwa tishio kubwa duniani.

“Magonjwa kama Kisukari,Kifua Kikuu,Kansa,Shinikizo la damu, Moyo, ndo yamekuwa tishio kubwa duniani kote, watati awali hayakupewa kipaumbele katika tafiti,” alisema Profesa Ngoma.

Wakati huo huo, Muhas  inatarajia kutimiza miaka 50 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 kikijulikana kama  Shule Kuu ya Madawa Dar es Salaam.

Katika mkutano huo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: