Friday, May 3, 2013

Loliondo: Waziri ageuka mbogo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.

  Asema kamwe serikali haiendeshwi na Ngo'
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, jana aligeuka mbogo kuhusiana na mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Akijibu hoja za wabunge kabla ya makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/14 yaliyowasilishwa bungeni Jumanne wiki hii kupitishwa jana jioni, Kagasheki alisema Serikali ya CCM haiwezi kuendeshwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanachochea mgogoro huo.


“Nimekwenda Loliondo mara nne na kimsingi hizi Ngo's ndiyo zinachochea mgogoro huo, tutakula nao sahani moja,”  alisema. Alisema madai yaliyotolewa na Msigwa kwamba yeye (Kagasheki), alikwenda Loliondo kwa kutumwa na Rais Kikwete, siyo ya kweli kwani alikwenda huko kama waziri mwenye dhamana na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Aliongeza kuwa suala la Loliondo zimeundwa tume nyingi katika kutafuta mwafaka, lakini kwa kuwa sasa limefikishwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wananchi wavute subira wakati serikali inatafuta suluhisho la kudumu.

“Hata kama tunafanya siasa unaposema wabunge ambao wengine ni Wamasai wamewasaliti Wamasai unakuwa unawaonea, tusitake umaarufu wa kuumizana, watu wanapokuwa katika matatizo tusipende kutengeneza siasa, siyo sahihi,” alisema.

Kagasheki alisema eneo la Loliondo kinachoangaliwa ni uhifadhi tu na kwamba hakuna mwekezaji yeyote atakayepewa ardhi kwa ajili ya kumilikishwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Aliongeza kuwa suala la CCM kuunda tume au kamati siyo dhambi na kwamba baada ya viongozi wa chama hicho kufanya ziara Loliondo ripoti itaandikwa na itajadiliwa katika vikao vya chama.

Waziri Kagasheki alisema kuwa  suala hilo atalitolea maelezo Waziri Mkuu. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema uamuzi wa mwisho kuhusu suala la Loliondo litatolewa na Waziri Mkuu, Pinda wakati wa kuahirisha mkutano wa  Bunge la bajeti unaoendelea.

Mgogoro huo jana ulitawala mjadala bungeni, baada ya Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, kuliambia Bunge kwamba serikali haiwezi kuutatua kwa kuwa umetengenezwa na Ikulu kiasi cha kumtia doa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kabla ya mgogoro huo kulelewa na serikali ya awamu ya tatu na ya nne.

Utawala wa serikali ya awamu ya tatu uliongozwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, na kufuatiwa na awamu ya sasa ya nne, unaoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo ya Msigwa, ambayo ilionekana dhahiri kuiudhi serikali, ilimfanya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Christopher Ole Medeye, kusimama na kuliambia Bunge kwamba, hakufurahishwa nayo kwa kuwa imelenga kuwadhihaki marais hao wastaafu.

Msigwa, ambaye ni Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alitoa kauli hiyo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

“Mgogoro wa Loliondo ulitengenezwa na Ikulu. Na katika mambo yanayomtia doa Mwinyi ni pamoja na mgogoro wa Loliondo. Ukalelewa na awamu ya tatu na nne,” alisema Msigwa.

Hata hivyo, wakati Msigwa akiendelea kuzungumza, huku akiitaja Ikulu na Rais, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisimama na kumtaka awe mwangalifu katika kutumia jina la Rais kwa sababu Rais ni taasisi.

Baada ya Mhagama kueleza hivyo, aliketi na Msigwa aliendelea kuzungumza na kusema Rais Jakaya Kikwete, ndiye aliyemchagua Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, kuunda timu ya kuchunguza mgogoro wa Loliondo na ndiye huyo huyo aliyemteua wakati mwingine Waziri Kagasheki kuushughulikia na kuwapa maagizo tofauti.

“Hilo linaonyesha kuwa aidha kuna tatizo kwenye taasisi ya Rais, au Kagasheki ni mwongo au wale waliotumwa kwenye chama ni waongo…Kiongozi anawatuma tofauti tofauti na maagizo tofauti,” alisema Msigwa.

Alisema hali hiyo imesababisha kuwatelekeza watu wa Loliondo kwa sababu tu kutafuta kura za urais mwaka 2015.

Msigwa alisema hashangazwi kuona serikali ikishindwa kuipatiwa mgogoro wa Loliondo ufumbuzi kwa sababu ndiyo hiyo hiyo, ambayo muda wote imekuwa ikiwavua Utanzania watu wa kabila la Wamasai kwa kutamka kwamba, ni watu wanaotoka nchini Kenya.

“Mwangunga aliwahi kusema hivyo wakati nyumba zao (Wamasai) zilipochomwa moto,” alisema Msigwa.

Hivyo, aliwataka Wamasai kutoukubali mgogoro huo, na kuitaka serikali kuusitisha mara moja.

“Wamasai nawaomba walikumbuke suala hili ili walinde ardhi yao, mgogoro wa Loliondo mmeutengeneza wenyewe, hivyo hamuwezi kuutatua…kiwango cha mgogoro wa Loliondo hakiwezi kupatiwa ufumbuzi,” alisema Msigwa. Alisema baada ya kusoma hotuba ya kambi rasmi ya upinzani, kuhusu bajeti ya wizara hiyo Jumanne wiki hii, alipata vitisho mara mbili kupitia simu alizokuwa akipigiwa na watu wasiojulikana kwa kutumia namba ya siri (private number).

Akijibu hoja za Msigwa, Ole Medeye alisema hakufurahishwa na kauli yake ya kuwataja marais wastaafu kwa kuwa imelenga kuwadhihaki bila kujali michango yao mizuri kwa taifa.
 “Ni lini (Msigwa) alipata taarifa ya kutendeka vitendo hivyo?, kwanini asiseme kipindi hicho?” alihoji Ole Medeye na kulitaka Bunge kueleza hatua, ambazo zitachukuliwa dhidi ya wabunge, ambao wana taarifa za uhalifu, lakini wanazificha.

Pia alilitaka Bunge kumbana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aonyeshe viliko viwanda nchini alivyosema vinafanya kazi ya kusaga meno ya tembo kabla ya kusafirishwa kiharamu nje ya nchi.

Alisema Mbowe anapaswa kuonyesha viwanda hivyo ili kuisaidia serikali kuwachukulia wahusika hatua zinazostahili.

Kuhusu hoja ya Msigwa kwamba, Wamasai hawana viongozi wa kuwatetea, Ole Medeye alisema Wamasai siyo bidhaa, bali ni Watanzania kama wengine na kwamba, hawajawahi kuomba msaada kwa wapinzani wawatetee.

Hivyo, aliliomba Bunge kupiga marufuku wabunge kutumia makabila kupiga kampeni za kisiasa na kusema kama kuna kero yoyote inayowasumbua wananchi, basi suluhisho lake linapatikana kwenye serikalini.

“Waliowasilisha suala la meno ya tembo, hawajui sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji. Iandaliwe semina mahsusi kuelimisha juu ya taratibu za kupakua na kupakia mizigo bandarini,” alisema Ole Medeye.

Awali, Mbowe, alisema tatizo la ujangili nchini ni la kutisha, lakini linafanyiwa utani na kwamba  watu waliopo kwenye biashara hiyo wamejipanga, hivyo kuna ulazima wa kufanyika kwa maamuzi magumu ili kuokoa maliasili za Watanzania.

Alihoji kama tembo wataisha nchini, ni kipi, ambacho serikali itawaonyesha watalii na kuongeza kuwa wanaovuna meno ya ndovu wanajulikana na wako kwenye mfumo, lakini wanaogopwa. Hivyo, alipendekeza wanaoendesha ujangili dhidi ya ndovu kupewa adhabu ya kifo.

“Tuweke sheria ya kunyongana. Sasa hivi wanasaga meno ya tembo, tofauti na zamani walikuwa wakichukua mazima. Kuna viwanda vya kusaga meno ya tembo na vinajulikana. Kuna viongozi wanashiriki katika biashara hii. Baadhi wanaondoka na meli, lakini wengine wanaondoka kwa ndege kwa sababu (meno) yanasagwa,” alisema Mbowe.

Alisema biashara hiyo imekuwa kubwa kwa kuwa kilo moja ya meno ya tembo inauzwa kwa Dola za Marekani kati ya 3,500 hadi 4,500.

“Jeshi letu la wanyamapori halishindwi kuzuia ujangili huu, lakini tatizo ni utashi wa kisiasa. Serikali yenu inajisikiaje kuelezwa kuwa ifikapo miaka saba hakutakuwa na tembo? Kama hatutakuwa na sheria ya kunyongana, tatizo hilo halitaisha. Serikali ichukue maamuzi magumu,” alisema Mbowe.

Alisema katika kuchukua maamuzi magumu, anajua kwamba, serikali italaumiwa na mashirika ya kimataifa, lakini akasema haiwezekani biashara hiyo kuachwa kuendelea, kwani tembo wanazidi kuisha katika mbuga mbalimbali nchini.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, aliomba Mwongozo wa Spika na kusema kauli ya Msigwa kwamba, wabunge Wamasai wamewatelekeza wananchi wao, mbali ya kuwa ni ya kuudhi, pia imepotosha ukweli.

Sendeka alisema yeye pamoja na Mbunge mwenzake wa Ngorongoro (CCM), Kaika Telele, kwa miaka saba ya kuwapo kwao bungeni, hawajawahi kuacha kuzungumzia mambo yanayowagusa wananchi wa Ngorongoro.

Alisema zaidi ya hivyo, katika moja ya michango yake bungeni, aliwahi kupendekeza kuundwa kwa kamati, ikaundwa Kamati ndogo iliyoongozwa na Mbunge Kongwa, Job Ndugai, kuchunguza tatizo la Wamasai.

Pia alisema robo tatu ya hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni iliyosomwa na Msigwa bungeni, ni nukuu ya ripoti ya Timu ya Nchemba, ambayo ndani yake pia kuna Wamasai.

Hivyo, akaomba kiti cha Spika kitoe mwongozo juu ya mbunge anapodanganya bungeni, huku akijua kuwa anatafuta umaarufu kutoka kwa Wamasai, ambao mara zote huwa hawamtumi mtoto, bali mtu mzima.

CHANZO: NIPASHE


No comments: