Binti mmoja aliyefahamika kwa jina la Khadija Idd anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Morogoro akidaiwa kumtupa barabarani mtoto wake mwenye umri wa miezi 6 baada ya mwanaume aliyezaa naye kumkataa.
Shuhuda wetu ambaye ni dereva wa bodaboda aliyefahamika kwa jina la Shabani, alisema tukio hilo lilitokea Juni 11, mwaka huu maeneo ya Mafiga karibu na Msikiti wa Mahita ambapo Khadija alichukua uamuzi huo baada ya mwanaume aliyezaa naye kumgomea mtoto kwa madai ana nywele za Kiarabu hivyo si wake.
“Huyu dada alifika kwenye kijiwe chetu akiwa amembeba mtoto mgongoni na kukodi pikipiki ili nimpeleke mjini.
“Tulipofika kwenye msitu uliopo karibu na mashamba ya SUA, aliniambia niendeshe spidi kuna mtu anamuwahi.
Nilitii amri lakini tulipofika mbele kidogo nikashangaa anamtupa yule mtoto.
“Nilipoona vile nilisimama na kumhoji kwa nini anafanya vile, akawa hajibu. Nikamchukua na kumpeleka kituo kikuu cha polisi akiwa hana mtoto. Baadae wasamaria wema walimuokota mtoto akiwa ameumia na kumfikisha polisi,” alisema mtoa habari huyo.
Mwandishi wetu alifika katika kituo hicho cha polisi na kufanikiwa kumkuta Khadija akiwa chini ya ulinzi mkali huku mwanaye akitokwa na damu usoni na alipoulizwa kulikoni alisema:
“Jamani naomba msamaha, nimefanya hivyo kwa hasira baada ya baba wa mtoto kudai si wake, eti ni Mwarabu wakati yeye ni Mngoni wa Songea, nisameheni sitarudia tena.”
Akizungumza na mwandishi wetu, Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Morogoro, Tausi Mbalamwezi alisema mwanamke huyo amefanya kitendo kibaya na sasa wanamsaka baba wa mtoto ili amlee huku mtuhumiwa akisuburi taratibu nyingine.
“Yupo hapa na tumemkuta na kadi ya kliniki ikionesha kuwa, baba wa mtoto anaitwa Costa Haule. Huyu hana nia njema na mtoto kwani alitaka kumuua kwa hiyo baada ya kumtibia tunawatafuta ndugu wa mwanaume au baba wa mtoto ili wamlee wakati tukiandaa utaratibu wa kumfikisha mahakamani,” alisema Afande Tausi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake