Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiwapungia mkono walimu walioshiriki katika hafla ya harambee ya kuchangia Saccos ya walimu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi, jana. Picha na Dionis Nyato.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwa ana ndoto kwamba siku moja sekta ya elimu itapewa kipaumbele cha kwanza nchini na kuzikomboa rasilimali za taifa la Tanzania zinazowanufaisha wageni na kuacha wananchi wakiambulia faida kidogo.
Huku akimtaja Dk Martin Luther King aliyekuwa mwanaharakati wa haki za Wamarekani weusi aliyefariki kabla ya kuuona utimilifu wa ndoto yake, Lowassa alisema kuwa anamwomba Mungu asimwondoe duniani ili aweze kushiriki kuifanya ndoto hiyo kuwa kweli itakayokamilika siku si nyingi ambapo viongozi watakubali kuwa elimu bora ndiyo itakayowasaidia Watanzania kuchimba madini yao na kuyauza kwa faida duniani.
Akizungumza wakati wa kuchangia SACCOS ya walimu ya Moshi Vijijini, Ushirika wa Stadium jana, Lowassa alisema kuwa katika ndoto yake anawaona viongozi wakikubali kwamba elimu bora ndiyo italisaidia taifa kuumiliki utalii na kunufaika nao, badala ya kuwaachia wageni wanufaike nao, huku Watanzania tukiambulia makombo.
Wakati Lowassa akieleza ndoto yake hiyo, Mwenyekiti wa TLP na mbunge wa Vunjo Augustine Mrema amesema: “Biashara ya urais imenishinda namwachia Lowassa kwani mimi nimeamua kurudi kwenye biashara ya rejareja.”
“Ninayo ndoto kuwa siku si nyingi zijazo, elimu itapewa kipaumbele cha kwanza nchini Tanzania.
Na namwomba Mwenyezi Mungu asiniondoe duniani, kabla sijauona utimilifu wa ndoto hii kama Dk King (Martin Luther) alivyoondolewa kabla hajaiona ndoto yake ikitimia, bali namwomba anipe muda na nguvu, niweze kushiriki katika kuifanya ndoto hiyo iwe kweli,” alisema Lowassa.
Katika harambee hiyo ambapo zilipatikana jumla ya Sh1.3 bilioni , kati ya hizo fedha taslimu zilikuwa Sh250 milioni, Lowassa alifafanua kuwa itafika wakati ambapo elimu ya Tanzania itakuwa bora na kuwavutia majirani zake kuja kuwasomesha watoto wao nchini.
Akizungumzia kudorora kwa elimu nchini, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kuwa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu imekuwa ikitegemea fedha za wahisani kwa asilimia 70 na kwamba jambo la kusikitisha wahisani hao hawatoi fedha zote wanazoahidi, badala yake hutoa asilimia kati ya asilimia 40 na 50 ya fedha walizoahidi.
“Bajeti yetu ya maendeleo ya sekta ya elimu kila mwaka haitekelezeki kwa upungufu wa asilimia 30-35. Kwa hali hii tutapataje maendeleo katika sekta ya elimu?” alihoji Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli mkoani Arusha na kuongeza: “Mwaka 1992 tulikuwa na Watanzania asilimia 15 tu wasiojua kusoma na kuandika, ilihali hivi sasa tuna Watanzania takribani asilimia 31 wasiojua kusoma.”
Lowassa alisema kuwa wakaguzi wa shule za msingi na sekondari kushindwa kukagua shule zote nchini huchangia kushuka kwa elimu, akibainisha kwamba asilimia 20 pekee ya shule zote ndizo hukaguliwa kwa mwaka.
Alisema ili kufikia mafanikio yatakayoletwa na elimu, Serikali inapaswa kumjali mwalimu kwa kumpa motisha na mazingira mazuri ya kufundishia.
Akijibu hoja za watu wanaosema kuwa kuboresha huduma za walimu haiwezekani kutokana na idadi yao kuwa kubwa, alinukuu sehemu ya hotuba ya Rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt akisema: “ Kitu kimoja tunachopaswa kukiogopa ni woga wenyewe.”
Lowassa alisema Watanzania wanapaswa kuuogopa woga unaowafanya waone kuwa pamoja na madini walionayo, gesi, mbuga nyingi za wanyama na ardhi nzuri ya kilimo, hawawezi kusimamia rasilimali hizo na kupata mapato makubwa yatakayowawezesha kuwalipa walimu vizuri.
Naye Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba alimuunga mkono Lowassa kwa kuitaka Serikali kuwekeze katika elimu, pamoja na kuboresha maisha ya walimu.
Akizungumzia mchango wa Lowassa katika elimu, Makamba alisema kuwa anamfahamu kiongozi huyo kama mtu asiyeogopa, huthubutu, hasa wakati aliposimamia ujenzi wa shule za sekaondari za kata nchini.
“Nakumbuka jinsi alivyompeleka mbio baba yangu Mzee Makamba alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, “alisema Makamba.
Kwa upande wake Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) alimsifu Lowassa akisema kuwa ni mchapakazi mahiri aliyefahamiana naye wakati wote walipokuwa mawaziri.
“Alipokuwa Waziri na mimi nilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ni hodari sana, nakuombea Mungu akujaalie katika maisha yako,” alisema Mrema.
Mwananchi
Muheshimiwa Lowassa, wewe ni miongoni mwa watu wliotufikisha hapa kwani hata leo bado ni mfanyakazi wa serikali. Sera za Tanzania katika kila sekta zinatokana na mchango wako Lowassa sasa sijui hiyo ndoto unamuotea nani wakati umewahi kuwa na hadi leo upo katika nafasi inayokuwezesha fanya mabadiliko makubwa sana Tanzania.
ReplyDeleteDr King alisema inawezekana ndoto yake ikamilike wakati yeye ameisha ondoka lakini alikuwa radhi kuwa watu wake wafaidike na matunda ya ndoto yake. Lakini wewe unataka ndoto yako ikamilike na uione kama siyo ubinafsi ni nini?
Mwisho, kumbuka kuwa uatajiri wa Tanzania unahujumiwa na familia si zaidi ya kumi na familia yako ni mojawapo. Sijui unasubiri nini zaidi ya kurudisha mapesa uliyopora toka kwa watanzania? Acheni kuwafanya wadanganyika kuwa ni wajinga