Mtumishi wa serikali, Shabani Mrutu (57), amepigwa risasi tatu na kufariki dunia papo hapo na watu wasiojulikana, wakiwa kwenye pikipiki maarufu kama bodaboda eneo la Tegeta Magereji, jijini Dar es Salaam, jana.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 6:15 mchana ambapo mtumishi huyo alikuwa akipeleka gari lake gereji kwa ajili ya matengenezo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura, alisema kuwa wakati Mrutu akielekea katika eneo hilo la gereji, ghafla pikipiki yenye watu wawili ilikuwa ikimfuata kwa nyuma.
Alisema vijana hao walimtaka ateremke kwenye gari lake aina ya Toyota Mark II yenye namba za usajili T 508 ADY na baada ya kushuka ndipo walipomshambulia kwa risasi.
Alisema marehemu alipigwa risasi tatu maeneo ya kichwani, kifuani na mguuni na kuanguka chini na kufariki dunia.
Wambura alisema baada ya kupigwa kwa risasi hizo, wafanyakazi waliokuwa eneo hilo la gereji walitawanyika na kukimbia.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo kwa kuwa hawajafahamu kama kuna mali zilizobwa.
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi na watakaobainika kuhusuka katika tukio hilo watachukuliwa hatua kali.
Kamanda alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment