Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiendelea na mchakato wa mafunzo ya ukakamavu kwa kikundi chake cha Red Brigade, siri ya mafunzo hayo imebainika katika maeneo tofauti.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini kuwa Chadema, pamoja na kutangaza azma hiyo, tayari mafunzo kama hayo yamekuwa yakitolewa na vyama vingine vyenye nguvu kubwa kisiasa hapa nchini.
Vyama vinavyotajwa katika utekelezaji wa mafunzo kama hayo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). CCM inatajwa kuwa na kikundi cha Green Guards wakati CUF ikimiliki kile cha Blue Guards.
Inaelezwa kuwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, vijana kadhaa walishiriki makambi maalum yaliyofanyika katika mikoa kadhaa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Vyanzo kadhaa vya gazeti hili kutoka vyama hivyo, zilieleza kuwa, mathalani, wakati vikundi hivyo vikianzishwa na kujiimarisha, Blue Guards ilifikiwa kuwa mlinzi wa msafara wa viongozi wakuu wa CUF.
“Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, msafara wa viongozi wa CUF na mikutano ya chama hicho kule Zanzibar hasa kisiwani Pemba, vimekuwa vikilindwa na Blue Guards, sasa mnajua walipata vipi mafunzo hayo,” kilihoji chanzo chetu.
Ilielezwa kuwa Blue Guards hao walipata mafunzo kama yaliyotangazwa na Chadema, yakitolewa na maofisa waastafu wa majeshi ya ndani.
“Walikuwa vijana wakakamavu, walidhibiti kila aina ya vurugu na ikumbukwe wakati huo, hapakuwa na uhusiano mzuri kati ya Serikali ya CCM na CUF huku Zanzibar,” ilielezwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, vijana wa Blue Guards walisambazwa eneo lote ambapo msafara wa viongozi wa CUF walipita na kuhutubia mikutano ya hadhara.
“Hata taratibu na itifaki za misafara ya viongozi zilipangwa na kusimamiwa na Blue Guards, wakiwa wameivishwa kimafunzo na hawakuwahi kukosea hata siku moja,” kilieleza chanzo kingine ambacho kama kilivyo cha awali, hakikutaka jina lake kutajwa.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa, wakati huo, mfumo wa mafunzo ya chipukizi wa CCM yaliboreshwa na kuhusisha vijana, lengo likiwa ni kuwawezesha kukabiliana na Blue Guards wa CUF.
“Hapo ndipo hila ovu zilipoanza kwa mifumo ya vikundi hivyo, lakini jambo la ajabu ni kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa na kila kitu kilifanywa kwa usiri mkubwa,” ilibainika.
Hata hivyo, uchunguzi huo ulibaini kuwa hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya vijana wanaoaminika kuwa wa Green Guards, kushiriki vitendo vya kuwashambulia na kuwajeruhi wafuasi wa upinzani.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wakati huo Chadema haikuwa katika wakati mzuri wa kuimarisha kikundi hicho, sababu kuu ikiwa ni kukosa nguvu kubwa za ushindani dhidi ya CCM.
Hivyo, ilipotangaza kuanza kuboresha mafunzo ya ukakamavu kiasi cha kuibua mjadala kwenye jamii, vyanzo visivyoweza kutajwa gazetini vimeeleza kuwa ni hatua nzuri.
“Kilichofanywa na Chadema ni kutangaza kile kilichofanywa na wenzake (CCM na CUF) kwa siku nyingi, lakini kikubwa zaidi wameliweka hadharani tatizo hilo ili lishughulikiwe,” alieleza mtoa taarifa wetu.
CHADEMA: TUNAFUATA KATIBA YETU
Kwa upande wake, Chadema imesema mafunzo wanayotoa kwa vijana wao ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema mafunzo yanayotolewa si ya kijeshi bali ni ya ukakamavu, kiitifaki na uongozi.
CCM: TUNAWATUMA KAZI NDOGONDOGO
Kwa upande wake, CCM imesema kuwa mafunzo yanayotolewa kwa Green Guard ni kwa ajili ya kuwaandaa kuwa viongozi, na kuwa tayari kutumwa `kazi ndogondogo’ pale kiongozi wa chama anapotembelea eneo husika.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema suala la vijana hao kuitwa walinzi, ni dhana ya kikazi, lakini si kwamba wamepewa mafunzo ya kijeshi.
POLISI: NI KOSA
Jeshi la Polisi, kupitia kwa msemaji wake, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Advera Senso, lilisema uanzishwaji wa vikundi hivyo ni makosa na hatua zinaweza kuchukuliwa dhidi yake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
1 comment:
Huu ni upuuzi na ni childish behaviour kwanini tusiwe na standard moja mikutano yote ya hadhara iwepo sheria iwepo Ambulance moja kwa ajili ya medical emergency na polisi wachahe kwa ajili ya usalama FINISH
Post a Comment