Hayo ni baadhi ya maoni yaliyotolewa na viongozi mbalimbali jana kwenye mdahalo ulikuwa unajadili 'Changamoto za kuongoza mabadiliko', ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi Tanzania.
Akifungua mdahalo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema mabadiliko yanapaswa kusimamiwa kikamilifu ili yalete matokeo yaliyokusudiwa.
"Kwa maana hiyo tunahitaji mabadiliko yatakayotusaidia kusonga mbele...unahitajika uongozi imara wenye uwezo wa kutafakari na kubuni mwelekeo," alisema.
Alisema kuongoza mabadiliko kuna changamoto na fursa nyingi na pia ukosoaji kutoka kwa wananchi lakini kiongozi anapaswa kujiamini katika kuyasimamia kwa manufaa ya umma.
Akizungumza kwenye mdahalo huo, mbunge wa zamani wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alisema kumekuwa na kasumba ya kuwawezesha wageni wanaokuja kwa mgongo wa uwekezaji na kuwasahau wazawa.
Alisema ili nchi iendelee na kujitegemea ni lazima wananchi wake wawe wamewezeshwa kumiliki uchumi na rasilimali za nchi.
"Tunakoelekea tunawasomesha watoto wetu ili waje wafue nguo za ndani za wageni...hapa tunawawezesha na kuwaabudu wageni badala ya wazawa. Viongozi lazima mthubutu, kuagiza na kusimamia utekelezaji wake," alisema.
Mzindakaya ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali kama Ukuu wa Mkoa na Uwaziri, alisema wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, viongozi walikuwa wawajibikaji na watendaji wazuri lakini hivi sasa hata barua serikalini hazijibiwi.
Alitoa mfano wa kitabu kimoja kilichochapishwa mwaka jana akisema kimeandikwa na 'mzungu' akieleza kwamba hivi sasa Afrika ndiyo inakopesha dunia kutokana na utajiri wa rasilimali zake.
Alisema utajiri huo unapaswa kumilikiwa kwa asilimia kubwa na wazawa badala ya inavyofanyika sasa kwamba wawekezaji wengi wamewekeza kwa nia ya kuzinyonya.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika, Dk. Getrude Mongella, alisema mabadiliko ni mapambano hivyo kiongozi yeyote anayetaka mabadiliko lazima ajitoe mhanga.
Hata hivyo, alisema kasoro nyingi zinazoonekana kwenye uongozi hasa kutoheshimiana ni kutokana na viongozi wengi kupata nafasi walizonazo bila kutegemea.
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema ili mabadiliko chanya yatokee lazima kuweka malengo na kuwa na uwajibikaji wa pamoja.
"Hili jambo kwa sasa ni kama halipo maana tunaona Mawaziri wakilalamika hadharani, mfano mdogo ni huu wa kodi ya simu ambayo tunashuhudia mawaziri wakilaumiana wakati tunaamini kwamba walikubaliana pamoja kwenye baraza lao," alisema.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema ili mabadiliko yatokee viongozi wanapaswa kuwashirikisha watu kubuni, kuweka vipaumbele na kusimamia utekelezaji wake na siyo kuwatawala.
Awali, akiwakaribisha washiriki wa mdahalo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alisema lengo ni kuwakutanisha viongozi wa serikali wa sasa na waliostaafu, sekta binafsi, wanasiasa na watendaji wengine ili wajadiliane, kutafakari na kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto za mabadiliko na namna ya kukabiliana nazo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment