ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 10, 2013

Kesi dawa za kulevya ziundiwe mahakama- Balozi Liundi

Mwanadiplomasia wa siku nyingi, Balozi Christopher Liundi, ameshauri kuwapo kwa mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za madawa ya kulevya nchini ili kupambana na tatizo hilo linaloendelea kushamiri kwa kasi.

Alisema juhudi hizo ziende pamoja na kuboresha na kuvipa uwezo wa kuharakisha uchunguzi vyombo vinavyosimamia udhibiti wa mihadarati kama polisi, kitengo na kamisheni ya kudhibiti madawa hayo.

Balozi Liundi ambaye alikuwa akiongea kwenye mahojiano maalumu na NIPASHE Jumamosi, alitaka serikali kuchukua hatua za haraka na za makusudi kurekebisha wimbi la uwezekano wa taifa kugeuzwa kituo cha kupitishia na kusambazia dawa za kulevya.

Alisema dawa za kulevya si suala la kupuuza kwani linadhalilisha heshima ya nchi kwenye jumuiya za kimataifa.

Alishauri vyombo hivyo vifanyekazi kikamilifu ili kuipa mahakama hiyo ufanisi wa kazi zake ambazo zitafanywa kwa haraka na matokeo yaonekane ambayo ni kutoa hukumu na kuadhibu genge lililohusika na uhalifu huo.

Alionya kuwa ni aibu Tanzania kugeuzwa kuwa kimbilio la wahalifu na kusisitiza kuwa wakati umefika wa kuushughulikia kikamilifu mtandao wa wauza mihadarati ambao ni genge linaloweza kujidai kuwa lina fedha.

Hivi karibuni wasanii wa muziki wa kizazi kipya Melisa Edward na Agnes Gerald - Masogange, walikamatwa Afrika Kusini wakiwa na kilo zaidi ya 150 za dawa za kulevya.


Huko Hong Kong China kwenye uwanja wa ndege wa HKIA Watanzania kadhaa walikamatwa mwezi uliopita wakitokea Dar es Salaam na shehena ya mihadarati .

Wasafiri wawili mmoja akiwa na miaka 26 alinaswa na kiloa 1.6 za heroin alizokuwa amezificha ndani ya sanduku dogo ‘briefcase ‘ na kwamba kama angeuza angepata bingo ya Dola milioni 1.28 (Sawa na Sh bilioni 2.1).

Katika mkasa mwingine siku hiyo, uwanjani hapo Mtanzania mwingine mwenye umri wa miaka 45 alikamatwa akiwa ameficha tumboni pipi kadhaa za heroine zenye gramu 204 ambazo thamani yake ilikuwa Dola za Marekani milioni 0.16 (sawa na Sh. milioni 260).

Balozi Liundi alisema habari hizo si njema na inaonyesha kuwa Tanzania inakuwa kituo cha kusambaza na kupitishia mihadarati lakini pia Watanzania nao ni vifaa vya kubeba madawa hayo.

Aliwataka wanasiasa, viongozi wa dini, shule na jamii na kila mmoja kuzungumzia ubaya wa madawa ya kulevya na kupinga matumizi yake ili kupunguza uwezekano wa taifa kuangamizwa na dawa hizo..
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hakuna haja ya kuunda mahakama maalumu ya madawa ya kulevya. Inaelekea hatujui tatizo ni nini?

Suala siyo mahakama, suala ni law enforcement, suala ni rushwa. Kuunda mahakama mpya ni kuifanya serikali iwe kubwa zaidi.

Kama hatuna sheria za kutosha kudhibiti madawa ya kulevya tunaweza kuunda sheria mpya.