Ni ukweli usiohitaji mjadala kwamba nchi za Kenya na Tanzania zinatambuliwa duniani kote kwamba sio tu ndio chimbuko la Kiswahili, bali pia ndio walezi wakuu wa Kiswahili. Hii ni kwa sababu nchi zote mbili zinagawana pwani ya Afrika ya Mashariki ambayo ndio chimbuko la lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili.
Wakati utawala wa kikoloni wa Waingereza ulipounda Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki (1930) na kuipatia jukumu la kusanifisha Kiswahili, mojawapo ya mivutano mikali iliyoibuka miongoni mwa wanaKamati ilikuwa ni juu ya lahaja ipi kati ya Kimvita (Kiswahili cha Mombasa) na Kiunguja (Kiswahili cha Zanzibar) itumike kama msingi wa mchakato huo wa usanifishaji. Hoja ya watetezi wa Kimvita ilikuwa ni kwamba Kiugunja kilishachafuliwa sana kama sio kuchakachuliwa kutokana na mwingiliano wake mkubwa na Kiarabu (kumbuka kwamba Unguja ilikuwa ndio makao makuu ya himaya ya kisultani wa Oman kuanzia miaka ya 1840), yaani kilikuwa kimekopa maneno mengi kutoka Kiarabu. Watetezi hao wa Kimvita waliendelea kudai kuwa Kimvita kilikuwa bado kimehifadhi sifa nyingi za Ubantu. Hata hivyo Kiunguja kiliibuka mshindi baada ya kura kupigwa (utafiti unahitajika kujua iwapo Masultani hakutoa kitu kidogo!). Pia ikumbukwe kuwa Kiunguja kiliishaenea sana katika koloni la Tanganyika. Kiswahili kinachozungumzwa Tanzania Bara msingi wake ni Kiunguja.
Tabia hii ya Kiunguja kukopakopa imeendelea kuathiri ukuaji wa msamiati kwa upande wa Tanzania kama ambavyo tabia ya kun’gang’ania ubantu ya Kimvita imeendelea kuathiri ukuaji wa msamiati kwa upande wa Kenya. Kila dhana mpya inapoingia katika jamii za wazungumzaji wa Kiswahili, Watanzania hupenda njia ya mkato – kutohoa wakati wenzao wa Wakenya hujaribu kushughulisha ubongo kwa kufukuafukua katika lugha za kibantu. Wakishindwa kupata jibu kutoka lugha za Kibantu, basi hujaribu kuunganisha vipande vya maneno ambayo tayari yanatumika katika Kiswahili (uundaji maneno). Mfano mdogo ni pale ilipoingia dhana ya “chombo cha idhaa kinachotoa sauti pamoja na kuonesha picha”, Wakenya wakakibatiza luninga (Tanzania wanasema runinga) lakini Tanzania wakatohoa na kupata televisheni. Ilipoingia dhana ya “mashine ya elektroniki ya kuhifadhi na kuchanganua taarifa zilizoingizwa, kukokotoa na kuongoza mitambo”, Wakenya waliunda neno tarakilishi (kutokana na maneno tarakimu na uwakilishi), Watanzania wakaingia katika njia ya mkato – kompyuta!
Maneno yote ni sanifu lakini hapa ni kwamba upatikanaji wake unadhihirisha tamaduni mbili tofauti, yaani kupata majibu kwa njia za mkato dhidi ya kupata majibu kwa njia za kushughulisha ubongo kwanza. Lugha si maneno tu, bali pia ni kiwakilishi cha utamaduni ulio dhahiri na usokuwa dhahiri. (cbwenge@ufl.edu)
No comments:
Post a Comment