ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2013

Raia wa Afrika Kusini kuingia nchini bila viza

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini,Radhia Msuya

Raia wa Afrika Kusini wanaopenda kuitembelea Tanzania hawatahitaji kutumia viza, badala yake watatumia pasi zao za kawaida za kusafiria, ubalozi wa Tanzania nchini humo ulieleza juzi.

Kadhalika, raia wa Tanzania wanaopenda kuingia Afrika Kusini nao hawatahitaji viza.

Taarifa ya ubalozi huo ilieleza kwamba fursa hiyo ni kwa Waafrika Kusini na Watanzania wanaopenda kutembelea nchi husika kikazi, kibiashara, binafsi, mapumziko ya sikukuu au wanaosafiri kuelekea nchi nyingine.

Hata hivyo, kibali hicho kipo kwa muda maalum wa siku 90 kuanzia Julai mwaka huu.

Katibu katika ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Habib Mohamed, alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya majadiliano na mamlaka husika za serikali za nchi hizo mbili.

Hatua hiyo imefikiwa pia kwa sababu nchi zote mbili ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), hivyo Watanzania watakaokuwa wanatembelea Afrika Kusini nao wameondolewa visa kwa siku hizo 90.

Awali, katika mahojiano, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, alisema nchi hizo mbili zimejadiliana namna ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizo hivyo wamekubaliana kubadilishana taarifa kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo uchumi, utalii, wahamiaji na wafungwa.

“Kwa sasa tunayo tume ya pamoja ambayo ni ngazi ya juu ya ushirikiano kati yetu...inajumuisha maeneo yetu yote ya ushirikiano,” alisema Msuya.

Alisema utekelezaji wa makubaliano hayo unafanywa na tume hiyo ambayo imepewa kazi ya kuangalia masuala muhimu kama uchumi, biashara, diplomasia, masuala ya kijamii na kisiasa.

Alisema kumekuwa na kikundi cha vijana wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakisafiri kila mwaka kuja Morogoro kwa ajili ya kujifunza uhusiano baina ya nchi hizo mbili hivyo angependa Watanzania nao wakaenda nchini humo kujifunza historia ya uhusiano kati yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: