Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete wakikagua chai ikichambuliwa katika Kiwanda cha Chai cha Ikanga, Njombe, ikiwa ni sehemu ya sherehe za uzinduzi wa Mkoa mpya wa Njombe, Ijumaa iliyopita. Picha na Ikulu
Njombe. Wananchi wa Kijiji cha Makoga Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe jana walisimamisha msafara wa Rais Jakaya Kikwete na kumweleza kero zao mbalimbali ikiwamo ya kutaka gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya zahanati ya kijiji hicho.
Wananchi hao walifurika saa nne asubuhi kandokando ya barabara na kuomba msafara wa Rais Kikwete usimame.
Msafara wa Rais Kikwete ulikuwa unatokea Makete kuelekea Njombe na ndiyo ukakutana na wananchi hao waliokuwa na shauku ya kueleza matatizo hayo kwa Rais.
Rais Kikwete alikubali kushuka na ndipo baadhi ya wananchi mmoja mmoja wakaanza kutaja kero zinazowakabili katika Kijiji cha Makoga.
Wananchi waliomba kuboreshwa kwa huduma ya maji pamoja na kuwahishiwa pembejeo za kilimo.
“Mheshimiwa Rais pia tunaomba gari la wagonjwa kwani tunapata shida sana kuwapeleka wagonjwa wetu hospitali,” alisikika mmoja wa wananchi hao akisema.
Majibu ya Rais Kikwete
Akijibu kero hizo za wananchi, Rais Kikwete aliwaahidi kuwa Serikali yake itatafuta fedha kwa ajili ya kuwaletea gari la wagonjwa.
Kuhusu pembejeo za kilimo, alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza pembejeo za kilimo mwakani. Kuhusu maji alisema kijiji hicho kipo kwenye mpango wa vijiji 10 vitakavyopatiwa huduma ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Pia Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema kijiji kipo kwenye mpango wa kuletewa umeme hivi karibuni.
Ahimiza tohara
Pia Rais Kikwete aliwataka wanaume nchini kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata tohara kama moja ya njia za kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi.
Akisalimia wananchi katika Kijiji cha Kipengele kilichoko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, ambako anaendelea na ziara yake kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, Rais pia amewapongeza wanaume ambao mpaka sasa wamejitokeza kupata tohara ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alizindua Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) katika Wilaya ya Makete ikiwa ni chuo cha kwanza katika mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo cha ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanapata fursa kujifunza ujuzi mbalimbali.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Zebedayo Mushi alisema chuo hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Veta na Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment