
MPENZI msomaji, wiki hii ni kwa walio ndani ya ndoa na wale wanaotarajia kuingia huko. Wewe utakuwa ni shahidi kwamba, wapo ambao ndoa zao sasa wanaziona ni chungu na kutamani kutoka.
Wapo ambao hawataki kutoka kwa kuogopa kuchekwa lakini cha moto wanakiona. Wanaishia kugumia tu, vurugu kila kukicha na wengi sasa hivi wana makovu kibao kwa sababu ya ngumi za kila siku.
Jamani, wengi wanapenda sana kuingia kwenye maisha haya ya ndoa lakini wanachotarajia ni furaha. Wengi wao wanaamini ukishaingia kwenye maisha hayo na mtu uliyetokea kumpenda, ni raha kwa kwenda mbele lakini kwa baadhi yao inakuwa ni tofauti.
Ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa, sababu ya kuikosa ile furaha na kufikia hatua ya kuiona ndoa ni ndoana ni kushindwa kuzingatia zile nguzo kuu muhimu zinazoweza kuishikilia ndoa yao. Yapo mambo mengi yanayoweza kuidumisha ndoa yako lakini leo ngoja niwakumbushie machache.
Imani yako kwake
Kwa ulimwengu wa sasa kuna kila sababu kwa wanandoa kuaminiana kwa kiwango kinachostahili. Unaposhidwa kumuamini mwenza wako mara nyingi sana utakuwa ukidhani anakusaliti kwa kuwa na mtu mwingine hata kama unavyodhani vinaweza vikakosa ukweli ndani yake.
Hali hiyo inaweza kukufanya ukakosa raha kila mwenza wako anapokuwa mbali na wewe. Si kukosa raha tu anapotoka ama anapokuwa mbali na upeo wa macho yako bali pia anaporudi unaweza kushindwa kuonesha upendo wako kwake na kuweza kujenga chuki dhidi yake.
Suala la uaminifu limekuwa adimu sana kwa wanandoa wengi. Ni wachache sana ambao ni waaminifu kwa wenza wao. Wengine wakipewa uongo tu kwamba mwenza wake ana uhusiano na mtu mwingine wanakubali mara moja hata kama habari hizo hazina ukweli wowote.
Jenga imani kubwa kwake na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini wewe ni muaminifu kwake. Epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mwenza wako akadhani una uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine nje ya ndoa.
Waweza kufanya hivyo kwa kuwa makini na maneno yako pamoja na matendo yako ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kudhihirisha kwamba siyo muaminifu katika ndoa.
Kitendo cha kuchelewa kurudi kazini kila siku bila kuwa na sababu za msingi, kulala nje, kuwa na uhusiano wa karibu na watu jinsia tofauti bila kuwepo na sababu za msingi, kupunguza mapenzi, kutokuwa na heshima ni baadhi ya matendo yanayoweza kuonesha siyo mwaminifu hivyo ni vyema ukaepukana navyo.
Kuwa mpole ila usiwe zoba
Watu wana tabia tofauti. Kuna wengine wana tabia ya kuwa wakali na wabishi hata katika mambo ambayo wanastahili kuwa wapole. Ukali kwa mweza wako bila sababu za msingi ni kuonesha kuwa humpendi, ubishi usiokuwa na sababu ni ishara ya kutokuwa na heshima kwake.
Kwa maana hiyo, jitahidi sana kuwa mpole kwa mwenza wako, nyenyekea pale inapobidi lakini usiwe zoba wa kukubali kupelekeshwa katika jambo ambalo unaona wazi siyo sawa.
Itaendelea wiki ijayo, usikose.
GPL
No comments:
Post a Comment