ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 25, 2013

Bobby Williamson atajwa Yanga

Ernie Brandts
Baada ya uongozi wa Yanga juzi kusitisha rasmi mkataba na Ernie Brandts kwa kumpa 'notisi' ya mwezi mmoja, Kocha anayeinoa Klabu ya Gor Mahia ya Kenya, Robert " Bobby" Williamson ametajwa kuwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Mholanzi huyo, imefahamika.

Yanga ilisitisha mkataba na Brandts ikiwa ni siku mbili tu baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba katika mechi ya 'Nani Mtani Jembe' iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Tangu Yanga itoe notisi hiyo kwa Brandts, huku ikifanya siri kubwa kwa kocha atakayerithi mikoba yake, yamezuka majina mengi yakihusishwa na nafasi hiyo, huku juzi pasipo kutajiwa jina, Nipashe likielezwa kwamba atakayeinoa timu hiyo ni kocha ambaye aliwahi kuinoa TP Mazembe ya DR Congo na Vital'O ya Burundi.

Hata hivyo, jana chanzo chetu kingine ndani ya Yanga kililiambia gazeti hili kuwa Bobby Williamson mzaliwa wa Glasgow, Scotland anakotoka aliyekuwa Kocha wa Man United, Sir Alex Ferguson, ndiye atakayerithi mikoba ya Brandts na kwamba uongozi ulifanya naye mazungumzo wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika Desemba 12, mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.

Kilisema Mscotland huyo atakuwa akisaidiwa na Boniface Mkwasa ambaye naye mazungumzo kati yake na Yanga yanaendelea, huku Felix Minziro siku zake za kuifundisha timu hiyo zikihesabika kabla ya kutupiwa virago.

"Bobby ndiye atakayeinoa timu yetu, akisaidiwa na Mkwasa nakuhakikishia mazunguzo yamefikia pazuri, wewe subiri utaona kitakachotokea," kilisema chanzo chetu huku kikiomba hifadhi ya jina lake.

Bobby Williamson aliyezaliwa Agosti 13, 1961 (miaka 52), kabla ya kutua Gor Mahia alikuwa akiinoa timu ya Taifa ya Uganda kuanzia 2008-2013.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Klabu ya Clydebank, Rangers na West Bromwich Albion aliyoichezea kuanzia 1986-1988 na kuifungia mabao 11 katika mechi 53 alizoichezea kabla ya kujiunga na Rotherham United 1988–1990 na kushuka dimbani mara 93 huku akifumania nyavu mara 49, ni kati ya makocha wenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika.

Mbali na Uganda na Gor Mahia, timu zingine alizowahi kuzinoa ni Rotherham United (1996–2002), Hibernian (2002–2004), Plymouth Argyle (2004–2005) na Chester City (2007–2008).

Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, alisema Brandts amepewa notisi ya mwezi mmoja kwa mujibu wa taratibu za ajira na baada ya hapo atakuwa nje ya benchi la Ufundi la klabu hiyo na kwamba kutimuliwa kwake hakukutokana na kipigo dhidi ya Simba.

“Brandts mwanzoni alipandisha kiwango cha timu yetu, kwa kweli kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye ili tusake mbadala wake,” alisema Bin Kleb.

Kuhusu wasaidizi wa Brandts, Bin Kleb alisema taratibu nyingine zinafuata na wakati huo klabu ikisaka mwalimu mwingine atakayerithi mikoba ya Brandts.
CHANZO: NIPASHE

No comments: