ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 26, 2013

ETI WANANDOA, MBONA KILA MTU SIMU YAKE INA PASSWORD?-2

NI matumaini yangu kwamba mishemishe za Krismasi zinakwenda poa na kila mmoja amekuwa akifurahia kwa staili ya aina yake.

Mpenzi msomaji wangu, wiki iliyopita niliianza mada hii lakini kutokana na ufinyu wa nafasi nikaishia katikati hivyo wiki hii nitaimalizia.

Ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa asilimia kubwa ya wanandoa kila mmoja simu yake ina password hivyo kuwa ngumu kuwepo kwa ushirikiano kwa namna yoyote wa simu hizi za mkononi. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, kwa nini tunafikia hatua hiyo kama kweli tunapendana na kuaminiana?

Yawezekana kweli kila mmoja anafanya hivyo kwa sababu maalum aidha za kikazi au kuepusha maswali mengi lakini je kwa kufanya hivyo hatuoni kwamba tunaongeza mazingira ya kutokuaminiana?

Hivi ni nani ambaye atakuwa na imani thabiti kwamba mumewe/mkewe ameweka simu yake password kwa nia njema? Ni wachache sana watakaoamini hivyo, wengi watajua anayeweka simu yake password ana mawasiliano haramu na mtu mwingine ambaye hapendi mwenzake ajue.

Hii ni mbaya sana, nasema ni mbaya kwa kuwa kama mke atamuona mwenzake kaweka simu yake password hawezi kuwa na imani naye, atajua ana mke mwenzake hata kama ukweli unaweza usiwe hivyo.
Kibaya zaidi ni kwamba mke akiona hivyo hata kama yeye hana mawasiliano haramu naye anaamua kuweka password ikiwa ni kama anayesema; ‘kama hutaki niguse yako na yangu pia usiguse’.

Katika mazingira hayo kuna suala la mwili mmoja hapo? Kimsingi u-mwili mmoja hautakuwepo na hakika ndoa itakuwa inakwenda kibubusabubusa tu. Kila mmoja ataishi akijua ana mwenzake lakini anamezea ili mradi siku zinakwenda.

Kwenye hili naomba niseme tu kwamba, hakuna kitu ambacho kimekuwa kikitibua ndoa nyingi na hata wale walio kwenye uhusiano wa kawaida kama kutokuaminiana.

Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, unapokuwa na mtu hakikisha unamjengea mazingira yeye kukuamini kwamba huna mtu mwingine zaidi yake.
Kitendo cha wewe kuweka password kwenye simu yako lazima kimfanye mwenza wako akufikirie tofauti. Hawezi kujenga imani kwako na mara zote hata kama hatasema lakini atakuwa akiumia moyoni kwa kuhisi unamsaliti.

Kwa Uchunguzi ambao nimeufanya hivi karibuni nimebaini wengi walio kwenye ndoa wana katabia haka ka kutotaka wenza wao waziguse simu zao na asilimia kubwa wanafanya hivyo kutokana na ‘vimeo’ vilivyomo kwenye simu zao.

Ni wachache sana ambao wanafanya hivyo kwa nia njema. Utakuta mwanamke ana mwanaume mwingine ambaye anawasiliana naye na anajua mumewe akijua patachimbika, kukwepa matatizo anakuwa hampi nafasi mwenza wake aiguse na kuitumia kwa namna yoyote. Vivyo hivyo kwa wanaume. Matokeo yake sasa kila mmoja anajihami.

Nihitimishe kwa kusema kwamba, suala la simu lisiwe sababu ya wawili waliopendana kuishi kwa kutibuana kila siku. Kama mwenza wako ameona ni sahihi kwake kuweka simu yake password, mwache afanye hivyo. Kama na wewe pia unadhani una sababu za msingi za kufanya hivyo, fanya kisha yaacheni maisha yenu yaendelee kuwepo.

Kikubwa ni kujua kwamba wengi wanaweka simu zao password kwa nia ya kuziweka salama ndoa zao kwa namna wanazozijua wenyewe, mengine ukitaka kufuatilia sana utajipa vidonda vya tumbo bure au kushangaa ndoa inavunjika wakati bado unampenda.

GPL

No comments: