Mkwasa atoa masharti yakitekelezwa kutua

Mbelgiji Luc Eymael
Kocha wa zamani wa timu ya AFC Leopards ya Kenya, Mbelgiji Luc Eymael, amekubali kuwanoa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, ameeleza.
Akizungumza na NIPASHE jana, Eymael, alikiri kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kurithi mikoba ya Ernie Brandts, na kufafanua kuwa wamefikia katika hatua nzuri.
Kocha huyo ambaye alikuwa Afrika Kusini akijaribu kusaka timu ya kuifundisha, alisema yuko tayari kukabiliana na changamoto mpya katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo itaendelea tena kuanzia Januari 25, mwakani.
Alisema Yanga ni moja ya timu nzuri na yuko tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali endapo atafanikiwa kujiunga nayo, huku akieleza kuwa ni timu yenye ushindani na yenye uzoefu katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
"Ni kweli nimeshafanya mazungumzo na viongozi wa Yanga na niko tayari kufanya kazi kama watakubaliana na mahitaji yangu," aliweka wazi kocha huyo ambaye aliiacha AFC Leopards tangu Agosti mwaka huu.
Aliongeza kuwa, kwa sasa hana timu ya kuifundisha licha ya kufanya mazungumzo pia na klabu ya Ismailia ya Misri.
Alisema kusimama kwa ligi ya Misri ni sababu nyingine iliyomfanya akatae ofa ya kujiunga na Ismailia.
"Niko tayari kujiunga na Yanga na kukutana na changamoto mpya, ni timu nzuri na siwezi kukataa ofa yao kama watanihitaji, ni kazi yenye heshima," aliongeza Eymael.
Mbelgiji huyo alifanikiwa kuipa matokeo mazuri AFC Leopards katika msimu wa kwanza baada ya kuikuta na matokeo yasiyoridhisha na kuiacha ikiwa ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Kenya na baadaye kuchukuliwa na James Nandwa na kumaliza ya pili nyuma ya vinara Gor Mahia.
Baada ya Yanga kufungwa mabao 3-1 na watani zao Simba Jumamosi iliyopita, ilitangaza kumtimua kocha wake, Ernie Brandts kwa kumtangulizia notisi ya mwezi mmoja na sasa inasaka kocha mpya.
AFC Leopards na Gor Mahia ni watani wa jadi kwa Kenya na kama ilivyo hapa nchini Simba na Yanga. Tayari Simba imeshamnasa kocha wa zamani wa mabingwa hao wapya wa ligi ya nchi hiyo, Zdravok Logarusic.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Binkleb, jana hakuweza kupatikana kuzungumzia mchakato wa kusaka kocha mpya ulipofikia.
Lakini Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alipoulizwa alisema bado klabu hiyo inaendelea na zoezi hilo, muda muafaka ukifika watatoa taarifa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa, amekiri kufanya mazungumzo na Klabu ya Yanga na kueleza kwamba kuna baadhi ya masharti amewapa viongozi wa klabu hiyo kabla ya kuamua kuingia mkataba wa kuitumikia.
Hata hivyo, Mkwasa hakuwa tayari kuweka wazi masharti ambayo amewapa Yanga na wakikubaliana nao atamwaga wino na kuanza kuwafundisha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Habari za ndani za Yanga zinaeleza kwamba Mkwasa anaweza kupewa kibarua cha muda Yanga wakati uongozi ukiendelea kusaka kocha wa kigeni na watakapompata atakuwa kocha msaidizi.
Mkwasa aliliambia gazeti hili kwamba yeye ni mwalimu wa mpira na atakuwa tayari kufanya kazi katika timu yoyote kama pande hizo mbili zitakubaliana.
Kocha na mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, alisema kwamba kabla ya kukubali kujiunga na Yanga ni lazima kwanza ahakikishe maslahi yake yanalindwa.
"Ni kweli wamenifuata, ila kuna mambo yanafanyiwa kazi, yakienda vizuri wao ndio watatangaza rasmi," alisema kwa kifupi Mkwasa ambaye alijiuzulu kuifundisha timu ya soka ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars).
Mapema wiki hii Yanga ilitangaza kusitisha mkataba wake na Mholanzi, Ernie Brandts, ikisema kwamba ameshindwa kukipandisha kiwango cha timu yao.
Kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Binkleb, alisema Yanga ilionyesha kiwango kibovu ilipokutana na watani zao Simba na siku hiyo hata kama ingekutana na timu inayoburuza mkia kwenye ligi ingepoteza mchezo.
Yanga sasa inapokea maombi ya makocha mbalimbali wenye lengo la kutaka kuifundisha timu hiyo ambayo mwakani itashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.
Kikosi cha Yanga kimepewa mapumziko na kitarejea tena kwenye mazoezi kesho Ijumaa kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Januari Mosi mwakani Visiwani Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment